Watafuta ajira Dubai sasa wabebeshwa cocaine!Dar es Salaam. Magenge ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya yameendelea kubuni mbinu mpya, na sasa raia wa Watanzania, bila ya kujua, wanabebeshwa dawa hizo ili wazisafirishe kwenda Hong Kong, wakitumia Uwanja wa Ndege wa Dubai.

Taarifa kutoka Dubai na Hong Kong zinaeleza kuwa zaidi ya watu 20 wameshahukumiwa kifungo na wengine wanasubiri hukumu baada ya kukamatwa wakiwa na dawa hizo walizobebeshwa na “wazungu wa unga” kutoka kwa Wanigeria na Watanzania wenzao.

Chanzo chetu cha habari kinaeleza kuwa Watanzania wengi wanaitwa kufanya kazi Dubai, lakini wakifika huko hubebeshwa dawa za kulevya bila kutaarifiwa na kujikuta wakikamatwa wanapowasili Uwanja wa Ndege wa Hong Kong.

Wakati Dubai inatumika kupitishia dawa za kulevya kutokana na udhaifu wa ulinzi, Hong Kong inachukuliwa kama njia ya kuingizia dawa hizo China kwa kuwa haina adhabu kubwa kwa makosa yanayohusu biashara hiyo haramu.

“Wanaitwa Dubai kufanya kazi, lakini wakiwa kazini wanatumwa kupeleka mzigo tuseme wa nguo au pipi, lakini kumbe kwenye pipi hizo kuna dawa za kulevya. Hawaambiwi kama wanabebeshwa dawa na hivyo hawajifichi wala kuwa na wasiwasi, lakini hukamatwa Airport ya Hong Kong,” alisema mpashaji habari kutoka Hong Kong ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.Masharti ya kupata ajira kwenye kampuni hizo si magumu, kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi.

Mwandishi wa Mwananchi aliyejaribu kuomba kazi za ndani kwenye moja ya kampuni (jina linahifadhiwa) zinayotafuta vijana wa kufanya kazi Dubai, aliambiwa kwanza awe na hati ya kusafiria.

Sharti jingine kwa mujibu wa kampuni hiyo ni kujua Kiingereza, ujuzi wa kutumia vifaa vya umeme vya kufanya usafi na apime afya.

“Baada ya hapo unasubiri kuitwa wakati ajira itakapotokea,” alisema mwakilishi wa kampuni hiyo.

Chanzo chetu cha habari kinaeleza kuwa genge hilo linawatumia watu hata wasiowafahamu wanaokwenda Hong Kong kwa kuwaomba wawasaidie kubeba vitu kama chokoleti au nguo, ambazo ndani yake hufichwa dawa za kulevya.

“Kundi hilo lipo pale Emirates Departure Lounge (sehemu ya wasafiri wanaoondoka). Na kama ujuavyo, ulinzi pale Dubai ni mdogo sana,” alisema.

Padri wa Kikatoliki anayehudumia wafungwa katika magereza za Hong Kong, John Wotherspon alituma barua pepe akisema Watanzania wengi wamekamatwa wakati wakitokea Dubai.

“Wengi wanatumia udhaifu wa ulinzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Dubai na wanawaita Watanzania kwa kuwadanganya kuwa wanawatafutia kazi, hasa za udereva, upishi na ufundi wa magari,” alisema.

Mtanzania mmoja aliyehukumiwa kifungo cha miaka 20 kwenye moja ya magereza ya Hong Kong, ameandika barua na kueleza jinsi alivyorubuniwa na Mtanzania na raia wa Nigeria kuwa atapata ajira Dubai, lakini baadaye akabebeshwa dawa za kulevya bila kujua.

“Nilimlalamikia mtu mmoja kuwa niko vibaya kiuchumi, wakaniambia watanisaidia. Mwanamume mmoja Mtanzania alinipeleka Dubai ambako aliniambia nitakutana na mtu mwingine atakayenisaidia,” inasema barua hiyo ambayo Mwananchi imeona nakala yake. Katika barua yake, Mtanzania huyo anasema alipofika Dubai alikutana na mtu huyo na baada ya siku kadhaa alitumwa kupeleka mzigo asioufahamu China kupitia Hong Kong.

“Nilikamatwa bila kujua nimebeba nini. Nawaasa Watanzania wenzangu kuwa hata kama ni maskini kiasi gani, wasikubali kubeba dawa za kulevya au kurubuniwa kwa namna yoyote. Nimeiacha familia yangu inateseka zaidi,” inasema barua hiyo.

Mwanamke mwingine Mtanzania aliandika barua akijuta baada ya kukamatwa Julai 17 kwenye Uwanja wa Ndege wa Hong Kong.

Katika barua yake, Mtanzania huyo anaeleza jinsi alivyorubuniwa akiwa Tanzania na kufika Dubai ambako alipewa dawa za kulevya kwa ajili ya kuzisafirisha kuelekea Hong Kong.

Katika barua yake, mwanamke huyo anaeleza kuwa kabla ya kukamatwa alikuwa anafanya biashara ya bidhaa za watoto alizokuwa anazitoa China na kuzileta Tanzania.

“Nilipofika Airport ya Hong Kong, maaskari walikagua mizigo yangu. Baadaye wakataka kukagua mwili wangu na wakanipeleka Hospitali ya Queen Elizabeth na nikakutwa na dawa za kulevya tumboni,” inasema barua hiyo.

Kamishna wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya, Mihayo Msikhela alisema ofisi yake ina takwimu za kuanzia Januari hadi Aprili zinazoonyesha Watanzania kadhaa waliokamatwa Hong Kong wakitokea Dubai.

“Sina idadi kamili, lakini tunazo hizo taarifa na zinaeleza hicho unachokisema,” alisema.

Alisema ofisi yake itafuatilia na kwenda mpaka Hong Kong na Dubai ili kujua kwa kina tatizo hilo.

“Siwezi kuwahukumu Dubai, lakini nchi nyingi zinazotumia uwanja huo, zinaeleza kuhusu udhaifu wa kiusalama pale,” alisema.
Watafuta ajira Dubai sasa wabebeshwa cocaine! Watafuta ajira Dubai sasa wabebeshwa cocaine! Reviewed by Unknown on 20:55:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.