Utekelezaji Zuio la Kusafirisha Mchanga wa madini Nje ya Nchi kuchukua Muda


Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuzuia usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda kuuchenjua nje ya nchi akitaka shughuli hizo zifanyike nchini, imeelezwa kuwa utekelezaji wa dhamira hiyo utachukua muda mrefu kutokana na mchakato wake.

Juzi, Rais Magufuli alinukuliwa na vyombo vya habari wilayani Kahama akisema katika uongozi wake hataki kuona mchanga huo ukisafirishwa.

Alisema katika nchi zote zenye madini, Tanzania ndiyo pekee inayosafirisha mchanga kwenda nje hivyo akaagiza shughuli hiyo ifanyike nchini.

Agizo hilo limekuja wakati utafiti juu ya uwezekano wa Tanzania kuwekeza katika mtambo wa kuchenjua mchanga wa dhahabu ya uliofanywa na Wakala wa Ukaguzi Madini Tanzania (TMAA) Februari 2011, ukionyesha kuwa ni uwekezaji unaohitaji fedha nyingi. 
Ripoti hiyo ilisema gharama za usimikaji mtambo kamili wenye uwezo wa kuchenjua wastani wa tani 150,000 kwa mwaka, ingeweza kufikia Dola za Marekani 500 milioni hadi Dola 800 milioni (sawa na Sh1.1 trilioni hadi Sh1.74 trilioni za sasa).

Ripoti hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kuangalia uwezekano wa kuchenjua mchanga unaosafirishwa na kampuni ya Acacia inayomiliki migodi ya dhahabu ya Buzwagi na Bulyanhulu, ilieleza kuwa baadhi ya mataifa yanayosafirisha mchanga huo kwenda Japani na China ni Chile, Indonesia, Peru, Marekani, Australia na Canada.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mgodi wa Barrick (sasa Accacia) huzalisha na kusafirisha kati ya tani 25,000 na 50,000 za mchanga huo kwa mwaka ili kuchuja kiwango cha madini yaliyomo.

Akitoa maoni yake binafsi kuhusu agizo hilo, Makamu wa Rais wa Acacia, Deo Mwanyika alisema msimamo wa Rais Magufuli ni sahihi lakini utekelezaji wake utahitaji maandalizi kutokana na ukubwa wa gharama za uwekezaji wa mtambo huo.

Huku akisisitiza kuwa maoni hayo ni yake binafsi, Mwanyika alisema ipo haja ya Serikali na sekta binafsi kukaa pamoja kwa ajili ya kujadili shughuli za uwekezaji huo hapa nchini.

“Nimemsikiliza Rais na nimemwelewa dhamira yake lakini hajamaanisha amezuia rasmi, haiwezekani kuzuia ghafla shughuli hizo. Pia sisi (wazalishaji) ni tofauti kabisa na sekta hiyo ya uchenjuaji, kwa hiyo itabidi kujadili nani awekeze, upatikanaji wa mikopo itakuwaje na mambo mengi yanayohusiana,” alisema.

Serikali iliwahi kulieleza Bunge wakati ikijibu swali la aliyekuwa Mbunge wa Kahama, James Lembeli, Aprili 2007 kuwa suala hilo ni la kisera kwa kuwa wawekezaji wameruhusiwa na Serikali ilikwishajitoa kwenye biashara.

Akijibu swali hilo ambalo Lembeli alitaka kujua kwa nini mtambo huo usijengwe nchini, aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Lawrence Masha alisema hali hiyo imetokana na Serikali kukosa wawekezaji au wawekezaji kuchelewa kufanya hivyo hapa nchini.

Masha alilishauri Bunge lishirikiane na Serikali kuendelea kuwakaribisha na kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza katika mtambo huo wa kuchenjua mchanga, akibainisha kuwa uwekezaji huo unahitaji mtaji mkubwa.

Miaka kadhaa iliyopita, aliyekuwa Mkurugenzi wa Ukaguzi, Uzalishaji na Biashara ya Madini wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Liberatus Chizuzu alikaririwa akisema  kuwa gharama za uwekezaji wa mtambo huo ni kubwa ikilinganishwa na thamani ya mapato yanayopatikana kupitia uchenjuaji wa madini yaliyopo.

Chizuzu alisema miongoni mwa masharti ya uwekezaji wa mtambo huo ni upatikanaji wa umeme wa uhakika, jambo ambalo ni changamoto hapa nchini.

Angalizo la Lisu 
Juzi, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alitoa angalizo kuhusu hatua hiyo ya Rais akisema Kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hao wanalindwa kisheria na kimkataba.

Mwanasheria huyo mkuu wa Chadema alisema kwa mujibu wa Sheria ya Madini na Mikataba ya Uendelezaji Madini (MDA), madini yote yanayochimbwa  ni mali ya wawekezaji.

Alisema kwa kuzingatia kwamba wawekezaji hao wanalindwa kisheria na kimkataba, hatua hiyo inaweza kuwafanya wawekezaji hao kwenda mahakama za usuluhishi za kimataifa.

Alisema Rais alitakiwa kufanya kama mwenzake, Evo Morales wa Bolivia ambaye nchi yake ilikuwa na mikataba kama ya Tanzania lakini alipochaguliwa Desemba, 2006 aliiondoa kwanza kwenye mikataba hiyo iliyokuwa inailazimisha kuingia kwenye migogoro ya uwezekaji na baada ya hapo ndipo akabadilisha sheria na mikataba ya uwekezaji iliyoipa Bolivia sehemu kubwa ya umilikaji wa gesi na mafuta ya nchi yake.
Utekelezaji Zuio la Kusafirisha Mchanga wa madini Nje ya Nchi kuchukua Muda Utekelezaji Zuio la Kusafirisha Mchanga wa madini Nje ya Nchi kuchukua Muda Reviewed by WANGOFIRA on 21:11:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.