Umetendwa, hutamani tena mapenzi? SOMA HAPA!



WIKI iliyopita nilikuta na rafiki yangu  m oj a . Akanisimulia historia ya uhusiano wake. Akanieleza kwamba kutokana na mwenendo aliopitia, hatamani tena kupenda. Ile ladha ya mapenzi ambayo wengi wanaipata, yeye alishasahau.

Mapenzi anayasikia kwa watu. Akisikia mtu anampenda mpenzi wake hadi anakosa usingizi anamshangaa. Anamuona kama punguani hivi. Rafiki yangu huyo aliniambia kwamba mwanamke aliyekuwa naye amempa adhabu kubwa maishani.

Alimuacha katika hatua ambayo yeye hakuitarajia. Kipindi ambacho alikuwa akimhitaji kuliko wakati mwingine wowote, yeye ndipo alipopata mwanaume mwingine na kuolewa. Alisema aliumia kwa sababu ndoto zao ilikuwa ni kuja kuishi kama mke na mume. Alimpenda, alimuamini na alimpa moyo wake wote. Japo rafiki yangu huyo hakuwa na kipato kikubwa wakati huo lakini upendo wa dhati aliokuwa anaupata kutoka kwa mpenzi wake ulikuwa ukimpa faraja maishani:

 “Nilimpenda sana, nilimuamini sana. Tulikuwa tukiishi kwa raha sana. Kipindi hicho sikuwa na kazi, kwangu haikuwa shida. Penzi lake la dhati kwangu lilinifanya nisahau hata matatizo yangu.

Kila akili yangu ilipokuwa ikifikiria mwanamke, nilikuwa nikimuona yeye tu. “Sikuona mwanamke wa kufanana na yeye. Yeye alikuwa ndiye daktari wangu. Alipokuwa mbali, kwangu mimi ilikuwa ni changamoto Nilitamani kila wakati awe karibu yangu. Ni mtu ambaye alinielewa kwa jinsi nilivyo. Hakuwa mtu wa kuhadaika na watu wenye fedha, alinipenda mimi tu japo nilikuwa sina fedha.

 “Alinitia moyo pale maisha yalipokuwa yakinipiga. Aliniambia nisimame kama mwanaume, nisitetereke kwani ipo siku nitafanikiwa. Alinifanya nijisikie nimeshiba hata kama nina njaa. Kwa jinsi nilivyomwamini, sikuwahi kuwaza kama kuna siku atakuja kubadilika.

“Kuna wakati nilijiona sistahili kupendwa kiasi ambacho alikuwa akinipenda mpenzi wangu. Nilitamani sana aje kuinjoi mafanikio yangu pale Mungu atakaponijalia na mimi nikipata kazi au maisha yakininyookea. “Bahati mbaya sana wakati mimi napata kazi, mwenzangu akaniacha kwenye mataa. Sijui aliingiwa na mdudu gani. Katika kipindi ambacho nilikuwa naiona nuru, yeye akaolewa na mtu mwingine. Niliumia sana. Nilijiuliza maswali mengi bila kupata majibu.

“Hapo ndipo nami mfumo wa maisha yangu ulipobadilika. Nilikuwa sinywi pombe nikajikuta nimekuwa mnywaji mzuri. Nikawa mtu wa kurudi nyumbani saa nane au tisa usiku. Wakati mwingine nilirudi kukiwa kumepambazuka. Ilikuwa ni mwendo wa pombe, pombe na mimi. “Niliwachukia wanawake wote.

Kila niliyemuona mbele yangu nilijua ni walewale. Hata pale nilipobahatika kukutana na mwanamke mwingine, bado sikuona sababu ya kumpa moyo wangu. Naye namuona ni kama yule tu. Anaweza akanifanya nizame kisha kuniacha solemba. “Kiukweli nampa shida sana huyu mpenzi wangu wa sasa.

Anajitahidi kunionesha mapenzi ya dhati lakini mimi akili yangu haipo. Simpi umuhimu, akiwepo sawa na hata asipokuwepo pia hewala, simpi thamani yoyote maishani,” alinisimulia rafiki yangu huyo. Nini cha kufanya? Tunapaswa kutambua haijalishi umetendwa kiasi gani, maisha lazima yaendelee.

Hupaswi kuumia milele. Kitu cha msingi ni kuruhusu moyo wako ukubaliane hali iliyotokea. Usikurupuke kutafuta mtu mwingine haraka haraka. Usijindanganye kwamba ukiwa mlevi itakusaidia kuondoa mawazo, changamsha akili kwa kufanya mambo mbalimbali.

 Waweza kwenda ufukweni kupumzika, kukutana na marafiki zako ambao watakupa stori za utani na hata za maendeleo. Usiingie kwenye uhusiano na mtu kwa sababu tu ya upweke. Ingia kwenye uhusiano na mtu ambaye unaamini ni sahihi. Ana sifa zile unazozihitaji? Kama ndiyo, basi anzisha naye uhusiano na umpende.

 Asikudanganye mtu, kadiri utakavyowekeza mawazo na akili yako kwake ndivyo ambavyo utasahau kule ulikotoka. Itafika wakati utasahau, utaona kule ulikutoka ilikuwa njia na sasa umefika katika mikono salama. Hakuna sababu ya kuishi katika mateso kwamba hutapenda tena wakati yule uliyempenda tayari ameshachukuliwa na mtu mwingine. Amekusahau kabisa, wewe uishi unamkumbuka kila siku wakati yeye hakukumbuki hata robo siku.

 Chukua hatua na uanze upya, maisha yataendelea!
Umetendwa, hutamani tena mapenzi? SOMA HAPA!  Umetendwa, hutamani tena mapenzi? SOMA HAPA! Reviewed by WANGOFIRA on 21:47:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.