Sakata la Oparesheni UKUTA Lailazimu Tume ya Haki na Utawala Bora Kuandaa kikao cha pamoja kati ya Chadema, CCM na Jeshi la Polisi


Tume ya Haki na Utawala Bora imeandaa kikao cha pamoja kati ya Chadema, CCM, Jeshi la Polisi na taasisi nyingine tatu, wakati joto la Operesheni Ukuta likizidi kupanda kwa viongozi wa Serikali na vyama vya siasa kutoa kauli zinazotofautiana. 

Chadema imetangaza kufanya mikutano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi katika operesheni iliyobatizwa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ikidai Serikali ya Awamu ya Tano inakandamiza haki na demokrasia nchini. 
Kabla ya kikao hicho, viongozi wa upinzani wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuwapo maridhiano katika suala hilo pamoja na Ukawa kususia vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, lakini kumekuwa hakuna harakati zozote zaidi ya majibizano. 
Hali hiyo ilizidi baada ya Chadema kutangaza operesheni hiyo ambayo imesababisha viongozi wa Serikali, hasa wakuu wa mikoa kuanza kutoa matamko ya kupiga marufuku mikutano yote ya Ukuta kwenye maeneo yao huku chama hicho kikisisitiza kuwa kitaendesha operesheni yake bila ya kujali amri ya kuizuia kwa kuwa kina haki kikatiba. 
Katika kile kinachoonekana ni jitihada za kutuliza hali hiyo,  Tume ya Haki na Utawala Bora imeandaa mkutano utakaohusisha taasisi sita, likiwamo Jeshi la Polisi lililozuia mikutano, CCM inayoendesha Serikali na Chadema inayopinga maamuzi ya Serikali kwa madai kuwa yanakandamiza demokrasia na kukiuka misingi ya utawala bora. 
Habari tulizozipata  zinaeleza kuwa wanaotakiwa kuhudhuria kikao hicho ni makatibu wakuu wa vyama hivyo, Abdulrahman Kinana (CCM), Vincent Mashinji (Chadema) na Ernest Mangu (Mkuu wa Jeshi la Polisi). 
Wengine ni Jaji Francis Mutungi (Msajili wa Vyama vya Siasa), George Masaju (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) na katibu mkuu wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). 
Habari hizo zinasema kuwa mwenyekiti wa Tume, Bahame Nyanduga,  ndiye ambaye amewaita viongozi hao Jumatano ijayo jijini Dar es Salaam. 
Tume ya Haki na Utawala Bora ina jukumu la kuhamasisha hifadhi ya haki za binadamu, kuchunguza jambo lolote, kutoa ushauri kwa Serikali na vyombo vingine vya umma na kuchukua hatua za kukuza, kuendeleza, usuluhishi na suluhu miongoni mwa watu na taasisi. 
Kutokana na hali ya kisiasa ilivyo sasa, mkutano huo hautaweza kumalizika bila ya kuzungumzia majibizano yanayoendelea kuhusu operesheni Ukuta na madai ya ukandamizwaji demokrasia unaodaiwa kufanywa na Serikali. 
Alipoulizwa   kuhusu mkutano huo, Nyanduga alimtaka mwandishi  kuwahoji kwa kina watu waliotoa habari hizo kwa sababu yeye hakutoa taarifa yoyote kwa vyombo vya habari kuhusu ajenda za mkutano huo.
 “Sikutoa mwaliko wala taarifa kwenu (wanahabari),” alisema Nyandyga alipoulizwa  kuhusu ajenda za mkutano huo. 

“Aliyekwambia (suala hilo), akupe taarifa kamili. Nikisema tunajadili nini, haitakuwa na maana ya kuitisha mkutano.” 
Mwezi mmoja uliopita, Rais John Magufuli alitangaza kuzuia mikutano ya kisiasa wakati akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu uliopita, akisema wanasiasa watafanya siasa mwaka 2020 wakati wa uchaguzi mwingine, akisema wakati huu ni wa kazi na asingependa kuona “mtu yeyote akinizuia kutekeleza ahadi nilizozitoa kwa wananchi wakati wa uchaguzi”. 
Ndani ya kipindi hicho, Chadema imezuiwa kufanya mkutano wa hadhara Kahama mkoani Shinyanga, imezuiwa kufanya hafla ya wahitimu wa vyuo vikuu vya Dodoma na ACT Wazalendo imezuiwa kufanya mkutano wake wa ndani kujadili bajeti ya 2016/17. 
Hatua hizo zilisababisha Chadema kufungua kesi Mahakama Kuu ikitaka itoe tafsiri baada ya polisi kuzuia mkutano Kahama na baadaye kuzuia viongozi wa chama hicho kuingia ofisi za Chadema za wilaya hiyo. 
Wiki iliyopita akiwa njiani kuelekea Kahama, Rais Magufuli alifafanua kauli yake kupiga marufuku mikutano ya kisiasa, akisema waliozuiwa ni wale walioshindwa kwenye Uchaguzi Mkuu na kwamba wale walioshinda wafanye mikutano kwenye maeneo yao na wasialike mwanasiasa kutoka sehemu nyingine. 
Ufafanuzi huo uliotolewa siku chache baada ya Chadema kutangaza operesheni hiyo ya Ukuta, umeibuka mjadala mpya, huku Jeshi la Polisi na wakuu wa mikoa wakitangaza kupiga marufuku mikutano ya Ukuta, huku wakizuia mwaliko wa wanasiasa kwenye mikutano itakayopata kibali. 
Chadema inasema kuwa ina haki ya kufanya mikutano popote pale kwa kuwa hakuna sehemu ambayo Sheria ya Vyama vya Siasa inakataza kufanya siasa baada ya uchaguzi. 
Takriban wiki mbili zilizopita, Mbowe alitangaza mikakati mitatu iliyoazimiwa na Kamati Kuu ya Chadema, ikilenga kupinga kile ambacho chama hicho inakiita kuwa ni ukandamizaji wa haki na demokrasia unaofanywa na Serikali. 
Mbowe alisema moja ya mikakati hiyo ni kufanya maandamano na mikutano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu, kama ishara ya kupinga kauli ya Rais na polisi kuhusu mikutano na maandamano. 
Mbali na mkakati huo, Chadema imeanzisha operesheni Ukuta, ikitaja matukio 11 inayodai kuwa ya ukandamizaji wa demokrasia nchini na mengine 24 kuwa yamesababisha kuanzishwa kwa operesheni hiyo.

 Mikakati hiyo ya Chadema ilipingwa na viongozi wa CCM na Jaji Mutungi kwa madai kuwa imejaa uchochezi. 
Wakati CCM ikiwataka Watanzania kutafakari kabla ya kuamua kuungana na viongozi wa Chadema kudai demokrasia na kugeuka kafara kwa vyombo vya ulinzi na usalama, Jaji Mutungi alisema kauli za chama hicho cha upinzani ni kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa. 
Wiki moja iliyopita, Jeshi la Polisi lilitoa kibali kwa Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kufanya mkutano wa hadhara jimboni kwake likizuia wanasiasa kutoka maeneo mengine na pia kuzungumzia chama kingine na kuisema Serikali. 
Mkutano mwingine uliofanyika Ikungi na kuhutubiwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, uliisha salama lakini muda mfupi baadaye mwanasheria huyo wa Chadema alimakatwa na Polisi na kusafirishwa hadi Dar es Salaam ambako amefunguliwa kesi ya uchochezi.
Sakata la Oparesheni UKUTA Lailazimu Tume ya Haki na Utawala Bora Kuandaa kikao cha pamoja kati ya Chadema, CCM na Jeshi la Polisi Sakata la Oparesheni UKUTA Lailazimu Tume ya Haki na Utawala Bora Kuandaa kikao cha pamoja kati ya Chadema, CCM na Jeshi la Polisi Reviewed by WANGOFIRA on 00:44:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.