RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 27


MTUNZI: ENEA FAIDY

...... MR ALOYCE alibaki kimya akiwa ametulia kimya kama vile amegandishwa na gundi ngumu. Haja ndogo ilipita taratibu katikati ya mapaja yake na kushuka chini ardhini. 

Alitamani ardhi ipasuke ili walau akajifiche chini ya ardhi kuliko kuendelea kushuhudia tukio lililokuwa linaendelea kwa wakati ule. Akili ilisimama, mwili ulinyong'onyea kwani hakuwa na lolote la kuweza kufikikiria kwa wakati ule. "Nimekamatika kwenye mtego" ndilo wazo pekee lililomjia akilini mwake.

Chatu yule aliendelea kujiviringisha kwa madaha na mbwembwe nyingi mwilini mwa Mr Aloyce na kumfanya mwanaume yule ajihisi mfu aliyebakisha roho yake tu kabla ya mazishi. 


"Nisaidie Mungu wangu" Mr Aloyce alisali kimoyo moyo akiamini kwamba huenda Mungu atasikia maombi yake na kumkumkumbuka katika Mateso yake. Machozi hayakumtoka hata chembe kwani hofu ilimzidia mpaka chozi lilimkauka.

Akiwa katika hali hiyo ngumu isiyoelezeka Mr Alloyce hakuona mtu yeyote wala dalili ya kiumbe chochote katika eneo lile. Ghafla upepo mkali ukapuliza eneo lile, ulikuwa kama kimbunga kinachoweza kuleta maafa kwa makazi ya watu.


 Mr Aloyce alijishangaa sana kuona mwili wake ukiwa mwepesi sana tena umejiachia kupita kiasi. Moyo wake ukafurahi na akatumia nafasi hiyo kujitazama mwilini mwake, akagundua yule chatu hayupo tena mwilini mwake Bali amesogea pembeni kidogo na kujituliza kama gogo.
Macho yalimtoka kama njugu akimtazama yule Chatu, ghafla akapigwa na mshangao wa ajabu baada yule chatu kubadilika umbile na kuwa na umbo la mtu. Mr Alloyce akamkazia macho MTU yule aliyetokana na chatu.

 Hakuamini macho yake pale alipogundua mtu yule alikuwa mkewe, Aloyce alitetemeka sana. Ndipo mwanamke yule alipoachia kicheko kikali sana huku akimsogelea Mr Aloyce. "Nilikukumbuka sana mume wangu.. Ila nasikitika unaniogopa" alisema mwanamke yule mwenye sura na umbile la mama Eddy. 

Mr Aloyce alitetemeka sana, akapiga hatua za kinyumenyume kumkwepa mwanamke yule.
"Mume wangu! Mbona unaniogopa?" Alisema mwanamke yule.


******

Dorice alimtazama Mansoor na kumsikiliza kwa umakini huku akiwa na hamu kubwa ya kutaka kujua njia nyingine ya kuweza kuondoka katika himaya ile ya kijini na kurudi duniani ili kumkomboa Eddy mpenzi wake wa dhati.

Mansoor alimtazama Dorice kwa unyonge sana, sura yake ilidhihirisha huzuni aliyokuwa nayo moyoni mwake. Akasogeza mkono wake na kuushika mkono wa Dorice kisha akausogeza karibu kabisa na midomo yake mizuri. Akaachia mabusu mazito mfululizo huku chozi likimdondoka. Kisha akainua macho yake na kumtazama Dorice.


"Dorice kwanini hunipendi?" Aliuliza Mansoor. Dorice alimtazama Mansoor bila kujibu chochote.


"Kwanini hunipendi?" Aliuliza tena Mansoor huku macho yake yakizidi kuwa mekundu kama pilipili. Kisha taratibu machozi yake yalianza kubadilika rangi na kuwa kama damu.


"Dorice! Naumia sana moyoni mwangu kumpenda mtu asiyenipenda! Najilaumu sana ingawa sio kosa langu ila ni kosa la moyo wangu ambao haukumchagua yeyote ila wewe..


 Natamani ungejua thamani ya upendo wangu kabla haujaenda duniani ili unikumbuke moyoni mwako" alisema Mansoor huku machozi mekundu yakizidi kudondokea kwenye mikono mizuri na laini ya Dorice. Maneno Yale yaliugusa moyo wa Dorice, akahisi ni mkosaji sana kwa kuutesa moyo wa Mansoor. 

Machozi yalimlengalenga machoni mwake akajikuta anamkumbatia Mansoor na kumtakia maneno ambayo hakuwahi kumtamkia hata Mara moja.

"NAKUPENDA SANA MANSOOR" alisema Dorice huku midomo yake ikibusu shingo ya Mansoor kwa huba, na mikono yake ilitembea taratibu mgongoni kwa Mansoor na macho yake yalikuwa yamefumba na kumpa nafasi zaidi ya kuzitafakari kwa kina hisia za mapenzi zilizokuwa kichwani mwake.


"Asante sana mpenzi wangu... Nakupenda na nitazidi kukupenda milele.." Ilisikika sauti iliyojaa huba na mahaba mazito ya Mansoor.


"Asante mpenzi... Lakini naomba unisaidie kwa lile suala langu.. Na umesema kwamba kuna njia nyingine.." Alisema Dorice akiwa bado amemkumbatia Mansoor.


Swali lile lilikuwa kero kwa Mabsoor kwani alijua Dorice hatozungumzia tena suala lile baada ya kumpa maneno matamu zaidi ya asali.
"Mh! Nitakusaidia... " alisema Mansoor.
"Lini?"
"Kuwa na subira... Wala usijali... " Mansoor alimwondoa shaka Dorice. Baada ya muda mfupi Mansoor alimuaga Dorice kisha akatoweka machoni pake huku akimuahidi kuwa atarudi baada ya muda mfupi tu. 


Hazikupita dakika nyingi Mansoor alijitokeza tena kwa Doreen lakini alikuwa na kitu kilichomshtua Doreen na kumfanya aogope sana.


******

Siku ya kwanza ndani ya nyumba ya mama Pamela iliisha vizuri sana wakiwa na Doreen. Usiku majira ya SAA NNE baada ya kula na kutazama televisheni huku wakipiga soga za hapa na pale wakaagana na kila mmoja alienda kulala kwenye chumba chake. Usiku ule Mama Pamela alihisi kuna utofauti ambao hakuuzoea kabisa. 


Paka walilia Mfululizo na kumfanya Mama Pamela ahamaki kidogo, sauti ya paka kutoka batini ilisikika ikilia kama mtoto mchanga jambo ambalo lilimtisha mama Pamela. Na haikuwa hivyo kwa mama Pamela tu bali pia hata kwa Pamela kwani alikuwa anaogopa kupita kiasi.


Ghafla usingizi wa ajabu ukampitia Mama Pamela, macho yalikuwa mazito kiasi kwamba alishindwa hata kuyafumbua ingawa akili yake bado ilikuwa inaendelea kuwaza akajishangaa na kujiuliza usingizi ule ulikuwa wa aina gani kwani kwa kawaida mtu akilala hata akili pia inalala. 


Ghafla kitu kizito kilimkalia juu yake, akashindwa kupumua vizuri na kila alipojaribu kujiinua alishindwa. Akahisi anakabwa sana shingoni na kila alipojaribu kuinua mkono wake ili ajiokoe alishindwa. Akazidi kuhema kwa nguvu.

Nusu SAA nzima hali ile ilizidi kumsumbua mpaka aliposhtuka na kukaa kitandani huku jasho likimtoka kwa kasi kama vile yupo jijini Dar kumbe yupo Mbeya kwenye baridi Kali. Alikaa kitandani huku akihema sana ghafla akasikia kishindo kikali sana kilichomshtua na kumfanya atahamaki. 


"Mamaaaa! Mamaa " sauti ya Pamela ilimshtua sana Bi Carolina. Akatamani ainuke kitandani pale ili akamtazame mwanaye, Mara taa ikazimwa. Akajua umeme umekatika lakini kilichomshangaza ..........


ITAENDELEA....
RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 27  RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 27 Reviewed by WANGOFIRA on 22:33:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.