RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 24 & 25

MTUNZI: ENEA FAIDY

..Baada ya kutazama kioo cha simu Mr Alloyce alishtuka kidogo baada ya kukuta namba ya shemeji yake. Aliitazama kwa muda, huku akitafakari jibu la kumpa shemeji yake kwani tayari alimtaarifu kwamba aje kesho yake asubuhi. Aliamua kupokea simu ile huku akivuta pumzi ndefu na kuishusha taratibu sana.

"Halloo Shem! mbona ulikata simu kabla hujaniambia kuna tatizo gani?" Alisema Bi Sandra Dada wa mama Eddy.
"Ah..ah..Shem.. Usije kesho... Nimetatua ..tayari Shem!" Mr Aloyce alijikuta anapata kigugumizi cha ghafla kwani hakuwa na jibu sahihi la kumjibu shemeji yake.
"Umetatua SAA ngapi? Mbona sikuelewi shemeji? Si umesema nije kesho?" Sandra alishangaa.
"Ha..hapana Shem usije kwanza.. Usije!"
"Shem sikuelewi.. Nitakuja kesho.."
Alisikika Sandra kisha simu ikakatika.

Usiku ulikuwa ni mrefu sana kwa familia ile ya Mr Aloyce, walikesha wakiwa sebuleni yeye na mwanae. Usingizi ulimpitia kwa dakika chache kisha akashtuka. Akatazama saa yake ya mkononi ilikuwa tayari ni Saa kumi na moja alfajiri.
 
Mr Aloyce aliinuka kitini na kwenda bafuni, alioga haraka kisha akaingia chumbani na kubadili nguo.
Hakutaka kujichelewesha sana, akarudi sebuleni na kumuaga Eddy.
"Naondoka Eddy!"
"Baba naogopa kubaki peke yangu!"
"Jitahidi Mwanangu, siwezi kuondoka na wewe!"
"Twende wote baba!"
 
Eddy alizidi kumkazania baba yake lakini Mr Aloyce hakukubali hata kidogo kuondoka nae kwani alihofia misukosuko ambayo ingejitokeza wakiwa huko.
"Baki na mlinzi basi!"
Eddy aliinuka na kutoka na baba yake, nje kulikuwa bado hakujapambazuka vizuri hivyo kulikuwa na kigizagiza ingawa walisaidiwa na mwanga wa taa.

Mr Aloyce alichukua gari yake nyingine na kuiwasha haraka kisha akapiga honi ili mlinzi afungue geti.
"Bosi mbona usiku? Unaenda wapi?" Aliuliza mlinzi.
"Hayakuhusu.. Fungua geti nitoke, baki na Eddy!"
"Sawa bosi wangu.. Samahani kwa maswali!" Alisema mlinzi kisha akafungua geti Mr Aloyce akatoka na kuelekea kule alikopotelea mkewe.

Eddy alibaki na mlinzi wao pale nje, alikuwa na mawazo mengi sana kichwani hivyo alikuwa amejiinamia kimya tu bila kuzungumza chochote.

"Eddy mbona unawaza sana?" Aliuliza mlinzi. Lakini Eddy hakujibu kitu akabaki kimya amejiinamia.
"Eddy si naongea na wewe husikii au?" Aliuliza tena kwa sauti ya ukali kidogo. Safari hii Eddy aliinua kichwa na kumtazama.
"Demu wako amekutosa nini? Maana sielewi elewi humu ndani.. Mara mtoke mara muingie kimaajabu ajabu siwaelewi kabisa.!"
 
"Yanakuhusu?"
"Yanaweza kunihusu kwa sehemu.. !" Alisema mlinzi yule kwa masikhara.
"Sitaki kelele.." Alisema Eddy na kujiinamia.
"Sikia Eddy... Mnanionaga chizi chizi sana ila nina akili zangu... Tatizo lako nalijua na ninaweza kukusaidia.... Sasa endelea hivohivo... Ila jua mficha uchi hazai..!" Alisema mlinzi kisha akasogea pembeni na kuchukua shuka lake ili ajifunike.
"Anko! Umesemaje?"
"Sijasema chochote ..!"
"Anko nisamehe.. Umesema unaweza kunisaidia tatizo langu?"
"Ndio na ni kazi ndogo... Ila endelea kunifanya mwehu kila siku....!"
Eddy alimtazama mlinzi wao kwa mshangao wa hali ya juu.

********
Bi Carolina hakuwa tayari kumuacha Doreen abaki peke yake kwenye kituo cha mabasi ilhali alimuahidi kumsaidia. Hakujali kabisa maneno ya mume wake kwani alijua tu kuwa mumewe hapendi wageni nyumbani kwake.
Bila kuchelewa wakabeba mizigo na kufuata taxi iliyokuwa mbele yao kisha wakapanda.
"Mnaelekea wapi?"
"Forest Mpya.."
 
Dereva aliondoa gari haraka kuelekea Forest Mpya. Doreen alikuwa amekaa karibu kabisa na dereva wa taxi. Macho ya dereva yalikuwa hayakauki usoni kwa Doreen kwani kila mara alimtazama kiwizi binti yule.
"Mama! Hivi huyu ni mwanao!?" Aliuliza Dereva taxi.
"Ndio! Kwani vipi?"
 
"Daaah Mama umezaa mtoto mzuri kuzidi malaika.. Kha! Kuna wazuri ila huyu mwanao kazidi!" Alisema dereva taxi na kumfanya Doreen atabasamu huku akiinamisha kichwa chini kwa aibu.
"We dereva bwana.." Alisema Bi Carolina na kucheka.
"Ningekuwa sijaoa ningekuja kuchumbia huyu mtoto..!" Alizidi kutania dereva yule ingawa utani wake ulikuwa na ukweli ndani yake.
"Oa mke wa pili!" Alitania Bi Carolina.
"Mke wangu atajinyonga.. Maana ana wivu sana, tena akigundua Bi mdogo kamzidi uzuri ndo basi tena"

Wakati wakiendelea kuzungumza hayo walikuwa tayari wamefika eneo la Mbeya Carnival na muda mfupi baadae walifika kwenye jumba moja la kifahari, lililovutia sana.
"Tumefika dereva!"alisema Bi Carolina dereva akapaki gari wakashusha mizigo. Kisha Bi Carolina akatoa pesa na kumpa dereva.
"Asante mama.. Ila nitunzie huyo bibie..!"
Wote wakacheka kisha wakaingia ndani na kuiacha taxi ile ikiondoka kwa fujo.

"Karibu Doreen hapa ndo nyumbani jisikie uko nyumbani... Sawa mama?" Alisema Bi Carolina huku wakiingia ndani.
"Asante mama kwa ukarimu wako"
 
"Wala usijali.." Bi Carolina alimkaribisha vizuri sana Doreen bila kujua kuwa alikuwa akimkaribisha shetani mbaya mwenye kila sifa ya kuitwa katili. Alikuwa kama fisi anayekaribishwa buchani kwa ukarimu sana wakati nyama ikiwa imejaa. Doreen alifurahi sana moyoni mwake alijua ushindi wake upo karibu.

Waliingia ndani na kumkuta baba Pamela akiwa ameketi kwenye sofa akitazama televisheni huku akiwa ameshika rimoti na kubadili Chanel.
"Za kutangulia mume wangu.." Alisema Bi Carolina.
"Mama Pamela!"
"Abee!"
"Hakuna heshima tens katika ndoa yetu sio?"
"Ipo mume wangu..!"
"Nimekuambia usije na huyo binti hujanisikia... Bila haya unaniambia eti 'habari za kutangulia?' Hivi una akili kweli?" Alifoka baba Pamela.
"Nisamehe mume wangu ila inabidi utumie utu sio kila wakati unakuwa na roho mbaya!"
 
"Ok sawa.. Naheshimu maamuzi yako ila ipo siku utanikumbuka..!" Alisema Baba Pamela mbele ya Doreen kisha akaondoka zake na kwenda chumbani.
Bi Carolina hakuzielewa kauli za mumewe aliona kama ana roho mbaya isiyojali wageni wala kuwathamini wanyonge. Aliamua kuachana na maneno ya mumewe badala take akamkaribisha kiti Doreen na baada ya kupumzika kwa muda akampeleka kwenye chumba kimoja ndani ya nyumba yao na kumkabidhi Doreen.
"Utalala humu.. Na hiki kitakuwa chumba chako.." Alisema Bi Carolina akitabasamu.
"Ahsante.. Mama naomba niulize kidogo..!"
"Uliza tu usijali.."
"Dada Pamela yuko wapi?"
"Pamela yupo kwa shangazi yake.. Atarudi kesho kutwa mtakuwa pamoja!"
"Asante"

Bi Carolina aliingia jikoni na kuandaa chakula kizuri. Wakala kisha wakaenda kulala.
Wakiwa chumbani baba Pamela hakutaka kuzungumza lolote na mkewe mpaka usingizi ulipowachukua wote wawili.
Majira ya SAA kumi alfajiri Baba Pamela aliishtuka usingizini na kumshtua mkewe kwa nguvu.
"Vipi?"aliuliza Mama Pamela kwa sauti ya nyono kwani bado alikuwa na usingizi.
"Amka nataka nikuambie jambo..!" Alisema baba Pamela.

********
Baada ya ndoa ya Mansoor na Dorice, maisha mapya ya ndoa yalianza. Penzi zito la Mansoor kwa Dorice lilijidhihirisha rasmi na alimpenda kwa dhati mkewe. Furaha take aliyoitafuta kwa muda mrefu sasa ilitawala moyoni mwa Mansoor kwani tayari alishampata ampendae. Dorice hakuwa na furaha sana na ndoa yake kwani mawazo yake yote yalikuwa juu ya uhai wa mpenzi wake wa Moyo Eddy Alloyce. Kila mara alimfikiria Eddy, na aliona amefanya kosa kubwa sana kufunga ndoa na jini.
Wakiwa wametulia tuli katika pozi la mahaba, Dorice na Mansoor. Dorice alifungua kinywa na kuyasema Yale yanayomsibu, masuala yanayousumbua moyo wake kwa kipindi kirefu.
 
"Mansoor..!"
"Niite Mume wangu.." Alisema Mansoor, Dorice akacheka kidogo.
"Mume wangu!"
"Naam! Hapo sawa mke wangu.!"
"Nataka nikukumbushe kitu."
"Sema tu mpenzi wa roho yangu!"
"Vipi kuhusu ahadi yako ya kunipeleka duniani na kumwokoa Eddy?"
Maneno hayo yaliupasua moyo wa Mansoor na kuiyeyusha ghafla furaha yake. Hakutamani wala hakuwa tayari kuwa mbali na mkewe, alimpenda sana na alitamani awe wake daima milele. Kwake, Doreen alikuwa kama chanda ambayo bila hiyo Pete haina uthamanu wowote, machozi yalimlenga machoni mwake.
 
"Unataka kuondoka?"
"Ikumbuke ahadi yako..."
"Mke wangu unataka kunitenga? Unadhani ukienda duniani utakuwa wangu tena????"alisema Mansoor. Dorice akamtazama kwa mshangao.

=======SEHEMU YA 25==============

 ..DORICE alimshangaa Mumewe Mansoor kwa maneno yake. Machozi yalimlengalenga machoni mwake kisha akajiondoa kifuani kwa Mansoor na kujitenga kando.
"Vipi mke wangu?"
"Najuta Mansoor.. Najuta sana kukukubalia, sikujua kama hautakuwa mwaminifu kwa ahadi zako!" Alisema Dorice kwa hasira.
 
"Sina maana mbaya mke wangu mpenzi.. Usinielewe vibaya tafadhali...Nakupenda sana!"
"Unanipenda? Unanipenda nini uongo mtupu..!" Alisema Dorice kwa hasira huku machozi yakimshuka mashavuni mwake. Alijikuta anamchukia Mansoor kupita kiasi. Hakutaka hata kumsogelea karibu.
"Baby! Nimekuelewa basi naomba uwe na amani moyoni mwako" alisema Mansoor huku akimsogelea Dorice na kutaka kumkumbatia lakini Dorice alimsukumia kando Mansoor na kuongeza kilio chake.
"Sitaki uniguse mpaka utakaponiambia ni lini utatimiza ahadi yako"
 
"Baada ya wiki moja nitaitimiza ahadi yako..!" Alisema Mansoor kwa huzuni kwani alijua ni kiasi gani Dorice alimpenda Eddy na alijua kwamba endapo angemrudisha Dorice duniani basi angemsahau Yeye na kuponda raha na Eddy. Kila alipofikiria hilo Mansoor aliumia sana moyoni mwake. Hakutamani kumkosa Dorice lakini hakuwa na jinsi zaidi ya kutunza uaminifu wa kutimiza ahadi yake.
"Una uhakika utanipeleka baada ya wiki moja?" Aliuliza Dorice akimtazama Mansoor.
 
"Ndio.. Usijali!" Mansoor alijibu kwa unyonge sana.
"Hapo umenifurahisha!" Alisema Dorice na kumkumbatia Mansoor.
"Lakini kabla haujaenda huko kuna kitu muhimu unatakiwa ufanye!" Alisema Mansoor akiwa bado amemkumbatia Doreen.
"Kitu gani?" Aliuliza Dorice.
Mansoor alimuachia Dorice kisha akanyoosha mkono wake na kumuonesha Dorice kiganja cha mkono wake. Kwa mshangao kidogo, Dorice akatazama kiganja cha Mansoor.
"Unaona nini hapa?"
"Sioni kitu.."
"Huoni kitu? Hebu tazama vizuri"
"Naona Pete" alijibu Dorice kwa mshangao.

*********
Eddy alimtazama kwa mshangao mlinzi wao. Alimkazia macho huku akimwomba msamaha kwa kumjibu vibaya hapo mwanzo.
"Usijali.. Najua matatizo yako yanakufanya uwe hivyo" alisema mlinzi.
"Sasa utanisaidiaje? Maana nateseka sana!"
"Nitakusaidia tu wala usiwe na haraka... "
"Lazima niwe na haraka Anko maana mpaka sasa hivi sijawahi hata kukojoa!"
 
"Mmh! Haraka zilimponza chura zikafanya awe na mabaka. Vuta subira tu maana umefanyiwa mchezo mbaya sana." Alisema mlinzi yule huku akijifunika vyema shuka lake na kujigesha ukutani ili amalizie usingizi wake. Lakini ghafla akapigwa Kofi zito shavuni, aliruka kama kuku aliyeona hatari. Kabla hajakaa sawa Kofi lingine zito lilitua shavuni kwake, akajishika shavu na kutazama kama alikuwa amechanika lakini haikuwa hivyo kwani hakukuwa na damu yoyote ile.
 
Mlinzi yule akatazama huku na kule lakini hakuona Mtu aliyempiga makofi Yale mazito yaliyotua shavuni kama radi wakati wa mvya Kali.
"Vipi Anko?"
"Ah.. Hanna kitu.. Niko sawa tu.."
"Mbona umeruka sana?"
"Usijali Eddy.. Mimi nimeaga kwetu Musoma.. Niliwaaga wajita wenzangu..!" Alisema Mlinzi huku akisikilizia maumivu makali ya vibao alivyopigwa.
"Sikuelewi Anko ."
"Nimeaga.. Hakuna wa kunichezea!" Alizidi kuropoka mlinzi yule kisha akatulia kimya. Mawazo tele yakamjaa kuhusu vibao vile alivyopigwa kiuchawi. Aliwaza sana kwani alikuwa ana zindiko kubwa sana, sasa kwanini apigwe vile wakati ana kings anayoiamini? Alijiuliza sana bila kupata jibu.

Kulipambazuka kabisa, kimwanga kidogo cha jua kilianza kuchomoza kwa mbali. Wakati huo Mr Alloyce alikuwa kwenye gari take kuelekea msituni alikopotelea Mama Eddy.
Kichwani mwake alifikiria sana jinsi ya kutatua matatizo yanayoikumba familia yake. Hakupata njia kamili ya kuweza kutatua matatizo yake.
 
Aliendesha gari kwa mwendo wa SAA moja na nusu hatimaye akawasili kwenye eneo alilotakiwa kufika, akashuka kwenye gari na kuangaza macho yake huku na kule kuona kama atamwona mkewe.

******
"Amka mama Pamela kuna jambo nataka nikuambie"
"Bwana utaniambia asubuhi"
"Huu ndo muda mzuri wa kukuambia lakini kama hutaki basi.. " Alisema baba Pamela kwa sauti ya utulivu sana . Licha ya ubishi aliokuwa nao mama Pamela katika suala la kuamka lakini ilimbidi tu aamke ili amsikilize mume wake. Kwani alijua huenda ana jambo muhimu anataka kumueleza wakati ule.
"Niambie basi mume wangu!" Alisema mama Pamela huku akipiga miayo ya uchovu wa usingizi.
"Asubuhi ya Leo nina safari kikazi.."
"Unaenda wapi?" Aliuliza mama Pamela.
"Naenda Arusha mke wangu... Nilitemea nikuambie Jana ila uliniudhi mpaka nikashindwa kukuambia"
"Mmh! Utakaa muda gani?"
"Mwezi mmoja!"
"Mwezi mzima? Mbona mrefu hivyo?"
"Ndio hivyo mke wangu ni masuala ya kazi tu, sina jinsi"
"Imekuwa ghafla!"
"Ndio nimepewa taarifa juzi jioni, lakini...."
"Lakini nini?" Alishtuka mama Pamela
"Nikiondoka tu, na huyo mgeni wako atoke hapa nyumbani kwangu"
 
Alisema Baba Pamela kwa sauti ya msisitizo sana akidhihirisha kuwa alimaanisha kile alichokisema.
"Baba Pamela utaniudhi.. Sitaki maudhi yako na hiyo roho mbaya yako"
"IPO siku utafahamu kwanini nasema hivo.. Kaa vizuri na Mungu utafahamu mengi!" Alisema Baba Pamela kisha akajifunika vizuri na kulala ili aamke baada ya nusu saa.

Mama Pamela alibaki na mawazo mengi sana ila katu hakuwa tayari kumwacha Doreen aende zake. Alimwonea huruma binti yule kwani alishamwambia historian nzima ya maisha yake.' Mime wangu sijui yukoje siku hizi.. Ana roho mbaya.. Simfukuzi ng'oo Doreen. Mtoto ana adabu tena mstaarabu' aliwaza Bi Carolina.

Asubuhi na Mapema Baba Pamela alijiandaa na kuwahi uwanja wa ndege, Bi Carolina alimsindikiza mumewe hadi uwanja wa Songwe Airport Kisha akamuaga.
"Ila tekeleza nilichokuambia"
"Sawa !" Alijibu Bi Carolina kisha akaingia kwenye gari na kuondoa gari kuelekea nyumbani kwake.
Haukupita muda mrefu Bi Carolina alitia timu nyimbani kwake, akapaki gari na kuingia ndani. Lakini alipoingia ndani alikutana na hali ya utofauti.

Itaendelea.....
RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 24 & 25 RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi - (A Wizard Student) - Sehemu ya 24 & 25 Reviewed by WANGOFIRA on 20:40:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.