John Shibuda Amkingia Kifua Rais Magufuli


Katibu Mkuu wa Chama cha Ada Tadea, John Shibuda amesema Rais John Magufuli “ni katili kwa wahujumu wa ustawi na maendeleo ya Taifa na rafiki kwa waadilifu”, na kuwataka Watanzania kumuunga mkono kwa ukatili huo ambao amesema unabezwa na baadhi ya watu.

Shibuda, ambaye alikuwa mbunge wa Maswa Magharibi kwa tiketi ya Chadema na CCM kwa vipindi tofauti, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Shinyanga.

Alisema wanaodai Rais Magufuli ni dikteta hawajui viwango vya ubora wao katika kutoa hukumu hiyo na kuwataka kuchagua kupendezesha waadilifu ili kwenda peponi au waovu waliojipanga kwenda jehanamu.

“Ndugu zangu ukweli haulogeki. Mahimizo ya Rais si udikteta, bali ni dhamira ya kuibua msisimko wa uhuru na maendeleo na uhuru ni kazi na asiyefanya kazi asinufaike na jasho la Watanzania,” alisema Shibuda ambaye anasifika kwa uwezo wake wa kutumia vizuri lugha ya Kiswahili.

 Shibuda alisema kama Magufuli ni katili, basi dini zote ni katili kwa kuwa zina amri za Mungu ambazo zinawakataza watu kufanya mambo wanayoyapenda.

Alisema ndiyo maana viongozi wa dini nao wamekuwa wakisisitiza uadilifu, jambo ambalo Rais Magufuli analifanya.

“Napongeza ukatili wa Rais kukemea maovu,” alisema Shibuda.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imekuja katika dunia ya mabadiliko ya mila, jadi na utamaduni wa utendaji wa umma na kukomesha uzembe katika uwajibikaji, ufisadi na kuleta msisimko unaoshangiliwa na jamii na kuondoa zomeazomea dhidi ya Serikali.

Kiongozi huyo wa upinzani alisema ajenda ya vyama vya upinzani imenyauka na kuvitaka kuacha kutafuta mfereji wa kutorokea.

 Badala yake, alivitaka vyama vya upinzani kujipanga upya ili viwe na mtazamo mpya wa utendaji wa shughuli za kisiasa.

Aliifananisha Serikali ya Awamu ya Tano na mabadiliko ya tabianchi duniani, akisema Taifa limepata Rais mwenye utumishi changamfu na kugusa hisia za jamii.

“Vyama vya upinzani viache siasa za mipasho na vijembe. Siasa hizi hazitatui kero za umaskini, ujinga, uchumi wa kaya na wananchi,” alisema Shibuda.

“Wanasayansi walianza na dawa ya panado zakutuliza maumivu, lakini leo kuna dawa tatu na mseto kwa kuwa walishindana kugundua dawa bora, basi na wapinzani wawe na vikosi kazi vya kubuni tiba mbadala ya kutengua utumishi wa Rais Magufuli,” alisema Shibuda.

Alisema hakuna chama chochote cha kisiasa Tanzania ambacho kipo kwa masilahi ya kukweza chama kingine, bali kila chama kipo kwa ajili ya kugombania kushika hisia za jamii na kuwa na dola na wala chama hakilazimishwi kufungamana na tafsiri ya chama kingine kwani kina sera zake zaidi ya kufungamana siasa na itikadi ya chama chenyewe.

Alisema vyama vinaweza kuwa na ushirikiano wenye dhamira sahihi ya kukuza masilahi ya jamii, ndiyo maana chama chake cha Ada Tadea kinashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Shibuda aliwataka wanasiasa kuwa na mawazo makini ya kunufaisha fikra za Watanzania.

John Shibuda Amkingia Kifua Rais Magufuli John Shibuda Amkingia Kifua Rais Magufuli Reviewed by WANGOFIRA on 00:47:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.