JESHI LA POLISI LIJIPIME UPYA KWA MAUAJI YA WENZAO YALIYOTOKEA MBANDE.

Awali ya yote nianze kwa kutoa pole kwa Jeshi la polisi, waziri wa mambo ya ndani ya Nchi ndugu Mwigulu Nchemba, ndugu na jamaa wa Askari polisi 4 waliouawa kwa kupigwa risasi maeneo ya mbande usiku Wa kuamkia jumatano ya Agosti 24.
Ni siku ya jumanne Usiku majira ya saa tatu kasoro hivi naona picha ya polisi akiwa chini akiwa amepigwa risasi huku damu nyingi zikiwa zimejaa chini na matumaini ya askari huyu kuamka tena yakiwa hayapo.
Na baadaye kidogo napokea ujumbe unaliandikwa Askari wanne wapigwa risasi maeneo ya Mbande wakiwa wanalinda benki ya CRDB. Taarifa hii inanishtua na kuamua kuuliza watu wangu wa karibu na kwenye makundi niliyanayo ya whatsApp ili nipewe namba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es salaam, Kamanda Sirro ili anipe uhakika wa tukio hilo. Lakini pamoja na juhudi zangu zote naambiwa kamanda Sirro yupo eneo la Tukio japo simu yake haikupokelewa tena baada ya kuambiwa kauli hiyo.

Huku nikiendelea kuwaza juu ya tukio hilo, taarifa ya awali inakuja ikiwataja kwa majina askari wanne waliofariki katika tukio hilo na cha kushangaza zaidi taarifa zinasema bunduki moja waliyokuwa nayo polisi imechukuliwa na watu hao wanaosadikika kuwa ni majambazi mara baada ya kutekeleza unyama huo.

Naingia kwenye mitandao ya kijamii husasani Facebook huku nakuta mjadala mkali huku wengi wakifurahia kile kilichowatokea askari hao. Kwa madai ya kuwa Askari polisi wamesahau jukumu lao kuu la kumlinda raia na mali zake na kugeuka kuwa vipaza sauti vya watawala na wanasiasa kutekeleza maagizo yao na kusahau kuwa sheria ni msumeno hukata mbele na nyuma.

Mjadala huo unaendelea huku zikiwa zimesalia siku chache kufika siku ya tarehe moja septemba iliyotangazwa siku za hivi karibuni na viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini cha Chadema.  Kuwa itakuwa siku maalum ambayo viongozi na wafuasi wake waandamana nchi nzima kupinga kile wanachokidai ni Udikteta unaofanya na serikali ya awamu ya tano na kutaka kuwaziba midomo wapinzani, huku wakiibatiza jina la Operasheni Ukuta yaani Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania.

Siku za hivi karibuni yameshuhudiwa makundi ya Askari polisi wakifanya mazoezi kikamilifu. Huku wakiwa na silaha za moto, magari na vifaa vingine vya hatari ikiwemo magari ya maji ya kuwasha, mabomu ya machozi, mbwa na mengineyo mengi. Ambapo taarifa ya Jeshi la polisi iliyotolewa kwa Umma kuwa ni mazoezi ya kawaida kabisa na kuwataka wananchi kuondoa woga kabisa.

Maonyesho haya ya polisi ambayo ni ya aina yake tangu nipate ufahamu na kujitambua kuyaona yakifanyika  mchana kweupe na katikati ya mji. Maana hata rais wa nchi hii Dr. John Magufuli anasema haiwezekani nchi ambayo tumejitawala kwa miaka zaidi ya 50 raia wake wakitaka kusafiri wanasindikizwa na askari polisi.




Lakini cha ajabu ni kuwaona askari hawa wakifanya mazoezi mjini na hadharani na kuonyesha mbinu mbalimbali za kijeshi walizofundishwa na ambazo kimsingi zinapaswa kufanyika katika kambi zao ambazo ninaamini kuwa zina maeneo makubwa na ya kutosha kabisa kufanya mazoezi hayo.
Maana hali hii haijazoeleka kabisa nchini hapa na hii imesababisha hofu kubwa kwa raia ambao wengi wao wanajiuliza kuhusu amani gani tunayoitaja huku polisi wanazurura mitaani na silaha za moto. Huku wakiwa wamejitayarisha tayari kupambana na adui au yeyote atakayejitokeza mbele yao.
Hali hii imezua maswali mengi sana miongoni mwa raia kujiuliza kweli wapo Tanzania nchi ambayo tunatamba na kujivunia amani au ndo ni maeneo ya Somalia, Sudan au Kongo ambayo vyombo habari kila siku vinaonyesha majeshi yakilandalanda mitaani na silaha za kivita wakilinda amani na kuwasaka mahalamia na magaidi.
Tukio hili la mauaji ambalo kwangu ni la kinyama na lisio na chembe ya ubinadamu hata kidogo linaumiza na limeacha simanzi kubwa kwa wazalendo Wa nchi hii, na jamii kwa ujumla. Japo kwa baadhi ya watu wamelipokea kwa furaha kutokana na hali halisi na tabaka ambalo lilianza kujitokeza na sasa. Ambapo polisi wanalalamikiwa kutumiwa na watawala na baadhi ya viongozi wa serikali kwa kile wanachokiita nguvu ya dola. 







Jambo hili ambalo kwa sasa limeifanya jamii kuwaona askari polisi kuwa adui machoni pao, na kuchangia jamii kuwa na ushirikiano mdogo kwani kwa maeneo mengi sasa polisi na raia wamekuwa kama paka na panya

Na hivyo kuchangia jamii kuwatunza waalifu au kushindwa kutoa ushirikiano kwa jeshi hili lengo jukumu la kulinda raia na mali zao. Na ndiyo maana matukio mengi ya kuvamiwa na kuchomwa moto kwa vituo mbalimbali vya polisi, na kuuliwa kwa Askari polisi yaliyotokea mwaka jana na baadhi ya bunduki kuchukuliwa na watu waliotekeleza matukio hayo yalichukua muda mrefu kwa watuhumiwa kukamatwa.

Hivyo basi ni muda mwafaka sasa kwa viongozi wa jeshi la polisi kuona umuhimu wa kujenga ushirikiano na jamii ili jamii iweze kutoa ushirikiano wa kutosha kuwafichua waalifu hasa wale wanaotekeleza mashambulizi dhidi yao, na kuua askari polisi na baadhi ya wanaovamia au kufanya uhalifu katika vituo vya polisi.

Hivyo basi kwa mauaji ya askari wanne waliouliwa huko Mbande ambapo katika mitandao ya kijamii wahalifu wameugwa mkono na watumiaji wengi ya mitandao hii. Ni kipimo tosha kwa jeshi la polisi kujitafakari upya uhusiano wake na raia wanao walinda na kuwahudumia.

Itakumbukwa kuwa Askari polisi ni ndugu zetu, ni mama, baba,Shangazi na wajomba zetu, lakini pia wengine ni watoto, wadogo, kaka na Dada zetu.

Kwa nini tupigane, kwa nini tusishirikiane ili tuweze kujenga taifa Bora na thabiti, kuliko kuendeleza chuki na kinyongo mioyoni mwa raia, na jamii kwa ujumla na kufanya majanga mbalimbali ikiwemo mauaji ya polisi ambayo yanathibitisha msemo wa Kiswahili usemao Adui muombee njaa, ambayo kwa sasa mauaji hayo ya askari yanapongezwa na raia huku polisi hawa tukiishi nao majumbani kwetu.

Na niimani yangu kuwa vyombo vya usalama kwa kushirikiana na interejensia vinafanya msako wa usiku na mchana ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo hili waweze kueachukulia hatua stahiki. Mungu ibariki Tanzania, ibariki na watu wake pia waishi kwa upendo.

Makala haya yameandaliwa na Baraka Ngofira mwanafunzi wa Shahada ya kwanza ya Mawasiliano ya Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, anapatikana kwa mawasiliano ya 0763580901 au barua pepe ya barakangofira@gmail.com.

JESHI LA POLISI LIJIPIME UPYA KWA MAUAJI YA WENZAO YALIYOTOKEA MBANDE. JESHI LA POLISI LIJIPIME UPYA KWA MAUAJI YA WENZAO YALIYOTOKEA MBANDE. Reviewed by WANGOFIRA on 05:40:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.