Yanga karata muhimu leo
KIKOSI cha Yanga leo kitakuwa na kibarua kigumu wakati
kitakapokabiliana na wenyeji wao Medeama FC ya Ghana katika mchezo wa
marudiano wa kombe la Shirikisho Afrika.
Mchezo huo utachezwa kwenye uwanja wa Sekondi Takoradi nje kidogo ya Jiji la Accra kuanzia saa 12:00 jioni kwa saa za Tanzania.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam
timu hizo zilitoshana nguvu kwa kutoka sare ya kufunga mabao 1-1,
matokeo ambayo yalizidi kuiweka pabaya Yanga.
Yanga inahitaji ushindi katika mchezo wa leo ili ijinasue mkiani mwa
kundi hilo na kufufua matumaini ya kucheza nusu fainali endapo
watashinda mechi zao mbili zitakazosalia huku wakiwaombea mabaya
wapinzani wao MO Bejai ya Algeria na Madeama zipate matokeo mabaya
kwenye mechi zao zijazo.
Kocha Hans van Pluijm atamkosa beki Vicent Bossou kwenye kikosi chake
kutokana na kuwa na kadi mbili za njano lakini nafasi yake huenda
ikachukuliwa na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye hiyo itakuwa
mechi yake ya kwanza tangu kuanza kwa hatua hiyo ya makundi.
Pamoja na kuzidiwa na wapinzani wao Medeama katika mchezo wa kwanza,
Pluijm ameondoka nchini akiwa na matumaini makubwa ya kupata ushindi
katika mchezo huo wa leo huku akiwatumaini washambuliaji wake wawili
Donald Ngoma na Obrey Chirwa ambao wameonekana tishio kwa wenyeji wao.
Pluijm alisema ameupa uzito mkubwa mchezo wa leo kwa sababu ndiyo
uliobeba matumaini yao ya kufika kule ambapo walipakusudia wakati
wanajiandaa na hatua hiyo ya makundi na hiyo inatokana na maandalizi
ambayo wameyafanya kabla ya kuondoka nchini.
“Tutawakosa Bossou na Deusi Kaseke, lakini waliobaki wote wapo katika
hali nzuri na ninafurahi kuona wachezaji wangu wote katika hali nzuri
kuelekea mchezo huo naamini tutawashangaza wenyeji wetu Medeama kwa
kuwafunga wakiwa nyumbani kwao,”alisema Pluijm.
Kocha huyo alisema kwa kuwa wanahitaji pointi tatu katika mchezo huo
hawatocheza kwa kujihami bali watacheza kwa kushambulia zaidi huku
akijaza viungo wengi katikati ili kusaidia ulinzi kwa sababu wapinzani
wao wanatumia sana mashambulizi ya kustukiza.
Kwa upande wao Medeama ambao wanashika nafasi ya tatu kwenye kundi
hilo wakiwa na pointi mbili, wametamba kuimaliza Yanga katika mchezo huo
kwa sababu wanawajua vizuri wapinzani wao baada ya kuwaona katika
mchezo wa kwanza ulioisha kwa sare ya 1-1.
Kocha Pride Yaw Owusu, alisema Yanga ni timu ngumu na nzuri lakini
amewaanda vyema vijana wake kuhakikisha wanapambana kwa dakika zote 90,
ili kupata ushindi ambao utawahakikishia kucheza hatua inayofuata ya
nusu fainali.
“Najua kama Yanga wamekuja na nguvu kubwa ya kutafuta ushindi wakiwa
ugenini lakini hata sisi tunahitaji pointi tatu ambazo zitatuweka kwenye
nafasi nzuri ya kumaliza wa pili kwenye kundi letu ili tucheze nusu
fainali hivyo hatutakubali kupoteza mchezo huo hata kidogo,” alisema.
Owusu alisema ataingia kwenye mchezo huo akitegemea huduma ya
mshambuliaji wake Bismark Oppong, katika umaliziaji na kwa mbinu na
mikakati waliyoipanga anaamini wanayo nafasi ya kushinda mchezo huo.
Kocha huyo alisema licha ya kikosi chake kuwa na uchovu kutokana na
kukosa muda wa kupumzika, baada ya juzi kucheza mechi ngumu ya ligi ya
Ghana dhidi ya Liberty Professionals na kuibuka na ushindi wa bao 1-0
wakiwa nyumbani Sekondi Tokaradi.
Medeama inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ya Ghana,
kupitia kwa kocha wao wameapa kufanya maajabu kwenye michuano hiyo ikiwa
ni mara yao ya kwanza kufika hatua hiyo ya makundi.
Yanga karata muhimu leo
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:48:00
Rating:
No comments: