Viwanja 300,000 makazi duni kupimwa Dar es Salaam


 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Mozes Kusiluka
SERIKALI kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa mpango maalumu wa upimaji wa ardhi na urasimishaji wa maeneo yote yasiyopimwa katika Jiji la Dar es Salaam ambapo viwanja zaidi ya 300,000 vitapimwa na wamiliki wake kupewa hati.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kuhusu mpango huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Mozes Kusiluka alisema kuwa serikali imeamua kuja na mpango huo kwa sababu ya ukubwa wa jiji hilo na wingi wa watu ulioambatana na ujenzi wa makazi holela.

“Katika mwaka wa fedha 2016/2017 tumepanga kuwa na mpango maalumu wa Jiji la Dar es Salaam ambapo wataalamu wetu watakwenda, kuhakiki mipaka na kupima maeneo yote ambayo hayajapimwa na kutengeneza ramani zitakazoonesha maeneo ya barabara na maeneo ya huduma nyingine kwa kushirikiana na wananchi husika,” alisema Dk Kusiluka.

Alisema kuwa baada ya mpango wa uhakiki, serikali itatoa hati za maeneo hayo na kusisitiza kuwa kazi hiyo itafanyika pia katika maeneo mengine ya miji mikubwa nchini yenye watu wengi likiwemo Jiji la Mwanza.
Dk Kusiluka alisisitiza kuwa urasimishaji utakuwa shirikishi kwa kuwahusisha watu wote wa maeneo yatakayopimwa na serikali ambapo wananchi wenye nyumba watashirikiana na viongozi wa serikali katika mitaa kupanga na kuimarisha mindombinu ya maeneo yao.


Alisema pia pande hizo husika zitakubaliana kuhusu maeneo ambayo barabara za mitaa zitapita, mitaro ya maji machafu, magari ya kupitishia huduma za dharura kama Zimamoto na ya kubeba wagonjwa.

“Mpango wa Urasimishaji ni Shirikishi, wataalamu wa ardhi watakwenda kwenye maeneo yote yatakayopimwa hususan katika Jiji la Dar es Salaam na kukaa na wananchi wote, kupitia mipaka wakishirikiana na wananchi wote kwa uwazi ili zoezi hilo liwe na manufaa na tija kwa wananchi wote,” alisisitiza Dk Kusiluka.

Alisema kuwa licha ya kuwepo kwa sheria zinazoisimamia Sekta ya Ardhi nchini, bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya wakulima na wafugaji, migogoro ya kijinai ya mtu mmoja kuvunja nyumba au kuvamia eneo la mtu mwingine bila idhini, migogoro ya mipaka kati ya majirani na ile inayosababishwa na wananchi kutokujua sheria.

Mbali na sababu hizo alibainisha kuwa idadi ya watu na matumizi ya ardhi kwa shughuli mbalimbali imekuwa ikiongezeka wakati ardhi ikibakia ileile jambo linaloifanya sekta hiyo kuja na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto hizo kupitia wataalamu waliopo.

Alisema kuwa serikali imefanya mambo mbalimbali kuhakikisha kuwa inatatua kero za wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali kwa kuwatumia wataalamu wake kupima na kupanga maeneo ya vijiji mbalimbali, kutoa elimu pia kuajiri wataalamu wa masuala ya ardhi katika halmashauri zote nchini.

Aidha alisisitiza kuwa serikali imejipanga kupima maeneo yote ya ardhi nchini ambayo hayajapimwa kupitia mpango wa miaka 10.

HABARI LEO
Viwanja 300,000 makazi duni kupimwa Dar es Salaam Viwanja 300,000 makazi duni kupimwa Dar es Salaam Reviewed by WANGOFIRA on 20:46:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.