WA MILIONI SABA KWA DAKIKA KUPANDISHWA KIZIMBANI TENA
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) leo inatarajiwa
kuwapandisha kizimbani wafanyabiashara wawili akiwemo Mohamed Mustafa
Yusufali ‘Choma’ aliyewahi kutajwa kuwa anajipatia Sh milioni saba kwa
dakika moja kwa njia za udanganyifu katika mapato ya serikali.
Choma na mfanyabiashara wa Arusha, Samweli Lema, walifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana saa 9 mchana kwa
ajili ya kusomewa mashitaka yanayowakabili, lakini ilishindikana kwa
sababu muda ulikuwa umekwisha.
Washtakiwa hao waliondolewa katika viwanja vya mahakama hiyo jioni na
kurudishwa mahabusu kwa kutumia magari ya Takukuru, hivyo leo
wanatarajiwa kupandishwa kizimbani kwa ajili ya kusomewa mashitaka yao.
Choma atakuwa anakabiliwa na kesi mbili kwa wakati mmoja, kwa kuwa
Julai 12 mwaka huu, alifikishwa mahakamani hapo na wenzake wakikabiliwa
na mashitaka 199 likiwemo la kuisababisha serikali hasara ya Sh bilioni
15.6.
Awali kesi ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 15.6
inayomkabili Choma na wenzake Alloyscius Gonzaga Mandago, Isaack
Kasanga, Taherali Sujjauddin Taherali na Mohamed Kabula ilitajwa mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa
upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa
ajili ya kutajwa. Aidha, aliiomba Mahakama iwaruhusu kumchukua Choma kwa
ajili ya kumhoji kutokana na tuhuma mpya zinazomkabili na kuahidi
kumrudisha mahakamani kabla saa za kazi hazijaisha.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Shahidi alimuuliza mshtakiwa huyo kama
ana lolote la kusema, alikaa kimya lakini baadaye alidai kuwa ameelewa
na atakuwa tayari endapo wakili wake atakuwepo kwenye mahojiano hayo.
Hakimu Shahidi aliruhusu upande wa Jamhuri umchukue mshtakiwa huyo na
kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 5, mwaka huu. Choma ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Kampuni ya Superior Financing Solution Limited kwa mara ya
kwanza alifikishwa mahakamani hapo Julai 12, mwaka huu akikabiliwa na
mashitaka 199 ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, uhujumu uchumi
utakatishaji fedha na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 15.6.
Katika mashitaka ya kughushi inadaiwa alighushi hati za usajili
kuendesha kampuni 15 ikiwemo Festive General Business Limited
zimesajiliwa kihalali nchini jambo ambalo si kweli. Aidha, anadaiwa
kuwasilisha nyaraka hizo za kughushi kwa Kamishna wa Kodi Ofisi za TRA
Mkoa wa Kinondoni ili kuonesha kampuni hizo zimesajiliwa na zinastahili
kusajiliwa kama mlipa kodi.
Mbali na mashitaka hayo, washtakiwa wote wanadaiwa kutakatisha fedha,
kwa kuficha uhalali, chanzo na mzunguko wa Sh 1,895,885,000 kwa
kuzikopesha fedha hizo kwa watu mbalimbali na kupokea marejesho ya
mikopo huku wakijua fedha hizo zimetokana na njia zisizo halali za
kughushi na kukwepa kodi.
Yusufali anadaiwa kati ya Januari 2008 na Januari mwaka huu, kwa
vitendo viovu vya kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo kwa Kamishna
wa TRA, ameisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 15.6 ambazo
zilitakiwa kulipwa kama Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
HABARI LEO
WA MILIONI SABA KWA DAKIKA KUPANDISHWA KIZIMBANI TENA
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:39:00
Rating:
No comments: