RC MKOANI PWANI HANA GARI ALAZIMIKA KUTUMIA LA DC KISARAWE
Mkuu wa
mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, akizungumza na baadhi ya
watumishi wa umma na wakurugenzi mkoani hapo juu ya changamoto
zinazowakabili watumishi na sekretariet ya mkoa pamoja na hatua
wanazozichukua kukabiliana nazo.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa
Pwani pamoja na katibu tawala wa mkoa huo hawana usafiri wa uhakika
katika kutekeleza majukumu yao ya kazi hali ambayo inasababisha mkuu wa
mkoa huo kutumia gari la mkuu wa wilaya ya Kisarawe ambae bado
hajaripoti kazini.
Aidha baadhi ya
wakuu wa wilaya magari yao ni mabovu ikiwemo gari la mkuu wa wilaya ya
Kibaha huku maafisa tarafa 26 kati ya 27 waliopo mkoani hapo
wanakabiliwa na tatizo la kukosa pikipiki wanazotumia kwenye kazi zao.
Akizungumzia
changamoto zinazoikabili sekretarieti ya mkoa huo,mkuu wa mkoa wa
Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo alisema analazimika kutumia gari la mkuu
wa wilaya ya Kisarawe kwasasa.
Alielezea kuwa
anatumia gari hiyo kutokana na mkuu huyo wa wilaya bado hajamwapisha
kutokana na kutoa udhuru maalum na endapo mkuu huyo wa wilaya ataanza
kazi yeye atakuwa hana gari la kutumia.
Mbali na hayo
,mhandisi Ndikilo alisema wanakabiliwa na changamoto nyingine ya uhaba
wa fedha za matumizi ya kawaida (OC)ambapo uhaba huo unatokana na
kushuka kwa ukomo wa bajeti mwaka hadi mwaka hususan katika mwaka wa
fedha 2015/2016 ulishuka kwa asilimia 40 ikilinganisha na ukomo wa fedha
katika kipindi cha nyuma.
Alisema fedha
pia za matumizi ya kawaida zinazopokelewa kila mwezi ni pungufu tofauti
na kiasi cha fedha iliyopangwa hivyo kuathiri sekretarieti ya mkoa
katika kutekeleza majukumu yake.
“Changamoto hii
ni kubwa ambayo inasababisha kuzalisha changamoto nyingine ikiwemo
madeni ya watumishi ambayo hadi sasa yamefikia mil.152”
“Watumishi
hawapati stahiki zao kwa wakati na mazingira ya kazi yakikabiliwa na
changamoto mbalimbali hivyo watumishi wengine wanaamua kuhama na kwenda
kufanya kazi kwingine ambapo wanafikiri wataweza kutumiwa vizuri na
kupata maslahi mazuri”alisema mhandisi Ndikilo.
Akizungumzia
juu ya upungufu wa vitendea kazi alisema pikipiki kwa maafisa tarafa ni
tatizo jingine ambalo linahitaji kushughulikiwa.
Mhandisi Ndikilo alieleza ni tarafa moja ya Kaskazini Mafia iliyo nzima kati ya maafisa tarafa 27 waliopo mkoani Pwani.
Alisema kuwa
maafisa tarafa hao ni mkono wa kulia wa wakurugenzi na wakuu wa wilaya
ndio wanaochapa kazi katika pande hizo lakini hawana usafiri wa uhakika.
Alisema
sekretarieti ya mkoa ,wataalamu na maafisa tarafa hushindwa kutembelea
mamlaka za serikali za mtaa na maeneo mbalimbali kwa lengo la kufuatilia
miradi na shughuli zinazopaswa kufuatilia na hata wakitembelea inakuwa
sio kwa kiwango kinachotakiwa .
Mhandisi
Ndikilo alisema zipo hatua wanazozichukua ikiwa ni sanjali na kufikisha
changamoto hizo katika wizara na idara husika ili ziweze kutafutiwa
ufumbuzi.
Hatua nyingine
ni madeni ya watumishi kufikishwa hazina ili yaweze kulipwa licha pamoja
na kuwasilisha taarifa hizo lakini hazina bado haijalipa kwa wakati.
Hata hivyo
Mhandisi Ndikilo alielezea kwamba baadhi ya maafisa tarafa hawana ofisi
za kudumu wanalazimika kutumia ofisi ambazo hazina hadhi huku kukiwa
hakuna huduma muhimu za maji na umeme.
Mkuu huyo wa mkoa alisema ofisi ya mkoa imeshajenga ofisi 6 kati ya 27 zinazohitaji kwa maafisa tarafa hao.
Mhandisi
Ndikilo aliiomba ofisi ya rais ,utumishi wa umma kuangalia kwa ukaribu
matatizo hayo ili kuyatafutia ufumbuzi kwani ni moja ya sababu
zinazokwamisha utekelezaji wa ufuatiliaji na jitihada za kuinua
maendeleo ya mkoa kwa haraka.
Mwisho
RC MKOANI PWANI HANA GARI ALAZIMIKA KUTUMIA LA DC KISARAWE
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:26:00
Rating:
No comments: