Rais Magufuli atema cheche Wakati akiwaapisha makamishna wa polisi waliopanda vyeo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Makamishna Wasaidizi Waandimizi na Mananibu Kamishna wa Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa bidii zote bila ya kumuogopa mtu yeyote katika kuhakikisha maslahi ya nchi yanawekwa mbele.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwaapisha wa umma waliopandishwa vyeo hivi karibuni na Rais mwenyewe kutoka  Makamishna Wasaidizi kuwa Makamisha Wasaidizi Waandamizi na waliokuwa Makamishna Wasaidizi Waandimizi kuwa Manaibu Kamishna Wasaidizi.

Amewataka watumishi hao wa umma kufanya kazi kwa moyo mmoja na kutenda haki kwa watu bila kujali cheo wala umaarufu wa watu.

Akitolea mfano wa Askari wa Usalama barabarani Rais Magufuli amesema wamekuwa wakishindwa kukamata baadhi ya magari  yanayomilikiwa na baadhi ya polisi kama Happy Nation na Buffalo pale yanapofanya makosa na pindi wanapochukua hatua dhidi ya magari ya aina hiyo basi wanatishiwa kushushwa cheo au kuhamishwa kutoka pale walipo.

"Nataka mkafanye kazi kwa haki bila kuogopa mtu hata kama ni gari la IGP, Waziri au hata Rais sheria lazima ichukue mkondo wake na mhusika wa gari hilo atakwenda kujieleza polisi mwenyewe." amesema Rais Magufuli

Rais Magufuli amewataka makamishna hao waliopandishwa vyeo kuhakikisha sekta zote zinazotakiwa kulipa kodi kama bandari na utalii zinafanya hivyo kama sheria inavyosema huku akiwashangaa wale wanaosema kuwa meli zimepungua bandarini na watalii kupungua nchini.

“Meli zilizopungua bandarini ni zile ambazo zimekuwa hazilipi kodi kwakuwa sasa mianya yote ya kukwepa kodi imezibwa. Ni afadhali zile meli chache zitakazolipa kodi kuliko nyingi ambazo hazilipi kodi na vivyo hivyo katika sekta ya utalii ni bora watalii wasije kama hawataki kulipa VAT iliyotengwa na Serikali,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, amewataka makamishna hao kwenda kupambana na Tatizo la watumishi hewa katika maeneo yao ya kazi ili kuhakikisha tatizo hilo ambalo limeigharimu serikali mabilioni ya pesa halijirudii tena na kama bado lipo linatokomezwa kabisa.

Akiongelea suala la Polisi Jamii, Rais Magufuli amewataka makamishna hao kufanya kazi bila kujali utaratibu huo wa polisi jamii na kuongeza kuwa amekuwa akiupinga utaratibu huo tangu akiwa Waziri wa Uvuvi na kusisitiza kuwa dunia ya sasa ni tofauti na ile tuliyoizoea.

“Ilikuwa unaweza kumkuta mvuvi katikati ya ziwa akiwa anafanya vitu kinyume na sheria alafu unataka kuleta mambo ya polisi jamii kwa kuanzisha majadiliano na mhalifu, hili halikubaliki na nililipinga kwani ni lazima ifike mahali polisi aheshimiwe na tofauti iwepo kati ya polisi na raia wa kawaida,” amesisitiza Rais Magufuli.

Jumla ya Makamishna Wasaidizi Waandimizi na Mananibu Kamishna 60 wa Jeshi la Polisi wamepandishwa cheo na Rais Magufuli hivi karibuni na leo wamekula kiapo cha uadilifu isipokuwa Manaibu Makamishna wawili ambao wapo nje ya nchi kwa mafunzo maalum.
Rais Magufuli atema cheche Wakati akiwaapisha makamishna wa polisi waliopanda vyeo Rais Magufuli atema cheche Wakati akiwaapisha makamishna wa polisi waliopanda vyeo Reviewed by WANGOFIRA on 20:21:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.