NDIKILO: WAKATI WA PROPAGANDA UMEISHA TUFANYE KAZI

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

MKUU wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, ametoa rai kwa wananchi mkoani humo kuungana kwa pamoja na serikali ya awamu ya tano kufanya kazi ili kuinua uchumi na maendeleo ya mkoa na Taifa kijumla.

Aidha amesema wakati wa malumbano ya kisiasa na propaganda umekwisha hivyo jamii iwe nyuma ya mh Rais Magufuli na serikali yake kujenga maendeleo ya nchi.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya tume ya uchaguzi kutoka kwa afisa uchaguzi tume ya Taifa ya uchaguzi, Adam Nyando, mkuu huyo wa mkoa alisema wakati wa kukaa na kuzungumzia itikadi za kisiasa umekwisha kilichobaki ni kukubaliana na matokeo yaliyotangazwa na sio vinginevyo.

"Walioshinda wameshinda, aliyekosa kakosa, maji yameshamwagika, lakini kwa watanzania wote tumeshinda kwa kuwa tuna amani "

"Nawasihi wote tuungane kufanya kazi ili kuleta maendeleo ya Taifa, tuchape kazi ili yote yaliyoahidiwa wakati wa uchaguzi yapate nafasi kutekelezwa" alisema mhandisi Ndikilo.

Hata hivyo mhandisi Ndikilo alielezea kuwa kijumla mkoani Pwani zoezi la uchaguzi mkuu lilikwenda vizuri hadi kipindi cha kutangazwa kwa matokeo.

Alisema wapo baadhi ya watu walisema na kufikiri nchi isingetoka salama na ingetumbukia kwenye machafuko ya kisiasa baada ya uchaguzi mkuu badala yake hali ipo shwari.

Alisema mungu alituepushia na kutuondoa huko na sasa tupo shwariiii huku CCM ikiwa imeshinda ambapo Rais wa nchi ni John Magufuli.

Mhandisi Ndikilo alieleza baadhi ya nchi huwa wakitumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, uvunjifu wa amani ama vurugu nyakati za uchaguzi hivyo kwa Tanzania haina budi kumshukuru mungu kwa kutuvusha na kuendelea kuwa na amani.

Awali akimkabidhi mkuu wa mkoa huyo taarifa ya tume ya uchaguzi afisa tume ya Taifa ya uchaguzi, Adam Nyando, alisema kwa sasa tume ya uchaguzi inajielekeza kufanya majukumu mbalimbali ikiwemo elimu ya mpiga kura na zoezi la uandikishaji wapiga kura.

Alisema majukumu hayo yataenda sambamba na maandalizi ya mchakato wa kura ya maoni kwa kuanzia na kurekebisha sheria ya kura ya maoni.

Akieliza anasema uchaguzi mkuu umemalizika kwa amani na utulivu hivyo tume inaendelea na majukumu yake mengine kwa maslahi ya Taifa.

Hata hivyo alielezea kuwa zoezi la uandikishaji wapiga kura utakuwa ni endelevu.

Nyando alisema sheria inasema kati ya uchaguzi mmoja na uchaguzi mwingine lazima kuwe na uandikishaji unaofanyika.

Mratibu wa uchaguzi mkoani Pwani, Shangwe Twamala, alisema changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu 2015 zitashughulikiwa mapema kabla ya chaguzi zijazo.

Katika Uchaguzi mkuu uliopita CCM ilishinda majimbo yote 9 ya mkoani Pwani na Rais na makamu wa Rais Samia Suluhu walishinda kwa kupata kura nyingi dhidi ya vyama vingine vya upinzani.
NDIKILO: WAKATI WA PROPAGANDA UMEISHA TUFANYE KAZI NDIKILO:  WAKATI WA PROPAGANDA UMEISHA TUFANYE KAZI Reviewed by WANGOFIRA on 20:09:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.