Naibu Waziri apiga marufuku ushuru michezoni


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura amepiga marufuku halmashauri zote nchini kutoza fedha za ushuru katika shughuli zote za kijamii zinazofanyika kwa maslahi ya wananchi hususani katika masuala ya michezo.

Wambura aliyasema hayo juzi katika kilele cha mbio za Baiskeli za Acacia tufanikiwe zilizofanyika mjini Kahama na kuhusisha washiriki kutoka mikoa sita ya Kanda ya Ziwa zilizofadhiliwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia chini ya migodi yake mitatu ya Buzwagi, North Mara pamoja na Bulyanhulu.

Wambura alisema kitendo cha halmashauri ya mji wa Kahama kuwatoza ushuru wawekezaji hao kwa ajili ya uwanja wa Halmashauri na mambo mengine ni kinyume na utaratibu kwa mashindano hayo yalikuwa yakihusu jamii na si taasisi.

Alisema Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Mgufuli ilishakataa kuona vitu kama hivyo vinafanyika ambavyo vina maslahi kwa jamii husika na kuongeza kuwa viongozi wa halmashauri ndio pingamizi kubwa katika masuala mbalimbali ya michezo nchini.

Aidha Naibu Waziri huyo alisema michezo ni jambo muhimu katika jamii na kuongeza mashindano hayo ya mbio za baiskeli ya Kanda ya Ziwa yatafungua milango kwa mikoa mingine nchini kuanzisha mashindano kama hayo kwa lengo la kupata vipaji mbalimbali vitakavyowakilisha nchi katika mashindano makubwa baadaye.

HABARI LEO
Naibu Waziri apiga marufuku ushuru michezoni Naibu Waziri apiga marufuku ushuru michezoni Reviewed by WANGOFIRA on 20:51:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.