‘Mkutano Mkuu wa CCM siyo wa kupokezana vijiti’

 Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka
Msemaji wa Chama Ole Sendeka

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kwamba Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho, utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii si wa kupokezana vijiti, kwa sababu nafasi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti unapofika wakati wa uchaguzi haziombwi, bali yanapendekezwa majina ya watu wanaofaa kushika nyadhifa huo.

Aidha, kimesema maandalizi ya mkutano huo utakaofanyika Jumamosi wiki hii, yamekamilika na unatarajiwa kushirikisha wajumbe 2,456 na mpaka sasa wamekodi hoteli 306 ambazo zitawalaza zaidi ya watu 3,331 mjini Dodoma.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema Mkutano Mkuu Maalumu wa Taifa utamchagua Mwenyekiti wa CCM Taifa baada ya Mwenyekiti wa sasa, Jakaya Kikwete kung’atuka na kutoa nafasi hiyo kwa Rais John Magufuli kugombea.

Alisema Rais Magufuli atakuwa Mwenyekiti wa CCM wa tano baada ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete.

“Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, nafasi ya Mwenyekiti wa CCM na Makamu Mwenyekiti wawili unapofikia wakati wa uchaguzi nafasi hizi haziombwi isipokuwa Kamati Kuu inafikiria na kupendekeza majina na kuyawasilisha kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ambayo humteua,” alisema Sendeka.

Alisema kisha Mkutano Mkuu wa Taifa unamchagua kwa kumpigia kura. Alisema wanaopendekezwa hawajazi fomu za kugombea nafasi hizo na katika mchakato huo kinachofanyika si kupokezana kijiti, kama wengi wanavyopenda kuita, bali ni uchaguzi wa kumpata mwenyekiti wa CCM.

Alisema katika uchaguzi huo itapigwa kura ya ‘ndio’ au ‘hapana’ ili kupata mwenyekiti na lazima apate nusu ya kura na akipata chini ya nusu mapendekezo yataanza upya.

“Tuna imani wajumbe wote watampa mwenyekiti mpya kura zote za ‘ndio’ ili achukue nafasi ya kuongoza kitaifa,” alisema na kuongeza kuwa akipatikana mwenyekiti ataunda ‘jeshi’ lake, kwani hiyo ni desturi ya chama na walio katika Sektetarieti, watapisha ili mwenyekiti mpya aunde jeshi lake.

Rais Magufuli anatarajiwa kufanya mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya CCM baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa Taifa, kwa kupanga upya safu yake ya viongozi, ambao anaamini anaweza kufanya kazi nao kwa ajili ya kuleta mabadiliko ndani ya Chama.

Viongozi watakaojiuzulu ili kupisha Dk Magufuli kupanga safu hiyo ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, manaibu katibu mkuu wawili na watendaji wengine.

Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ni pamoja na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Katibu wa Oganaizesheni, Katibu wa Siasa na Uhusiano ya Kimataifa, Katibu wa Uchumi na Fedha na wa Itikadi na Uenezi.

“Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana atakabidhi barua yake kwa mwenyekiti wa chama kupisha Rais Magufuli aweze kuunda safu yake ya watu atakaofanya nao kazi,” alieleza Sendeka na kuongeza kuwa anaamini Magufuli ataunda safu nzuri itakayoleta mabadiliko.

“Chama madhubuti huzaa serikali madhubuti na chama legelege huzaa serikali legelege,” aliongeza na kubainisha kuwa maandalizi kwa ajili ya mkutano huo, yamekamilika na tayari fedha zimetumwa mikoani ili kuwezesha wajumbe wote kufika; na magari yatakodishwa kuwaleta mjini hapa.


Alisema jumla ya wajumbe 2,456 watahudhuria mkutano huo, lakini pia wanajitahidi kuweka hesabu vizuri kwa kuondoa wajumbe wenye kofia mbili. Alisema wamekodi hoteli 306. Akizungumzia hali ya usalama alisema wamejipanga kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa amani.

“Dodoma ni shwari na salama watu wasiwe na hofu na tuna imani mkutano utamalizika vizuri,” alifafanua na kuongeza kuwa wajumbe wa NEC watawasili Alhamisi tayari kwa kikao cha Ijumaa na wajumbe wengine watawasili Ijumaa.

HABARI LEO
‘Mkutano Mkuu wa CCM siyo wa kupokezana vijiti’ ‘Mkutano Mkuu wa CCM siyo wa kupokezana vijiti’ Reviewed by WANGOFIRA on 20:41:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.