Mambo 4 rahisi kuhamia Dodoma


WAKATI watumishi wa umma wakikuna vichwa, kuhusu maagizo yaliyokwishatolewa na yanayoendelea kutolewa ya kutakiwa kuhamia Dodoma mara moja, taarifa zinaonesha kuwa gharama za kuhamia na kuishi, si kubwa kama inavyodhaniwa.

Tathmini ya awali ya gazeti hili imeonesha kuwa hofu kubwa ya watumishi hao ni gharama za kuanza makazi mapya hasa nyumba na huduma za starehe na mapumziko baada ya kazi na wakati wa mwisho wa juma.

Pia imebainika gharama nyingine ni mazoea tu, kwa kuwa huduma nyingi zikiwemo za chakula na usafiri, vimeonesha kuwa ni nafuu kwa mkoa huo, ikilinganishwa na mkoani Dar es Salaam.

Takwimu za Gharama za Maisha (CPI) za Juni mwaka huu, zinaonesha kuwa sehemu kubwa ya kipato cha Watanzania sawa na asilimia 38, hutumika katika chakula huku hoteli na migahawa ambayo hutoa huduma hizo pia, pamoja na nyinginezo ikichukua asilimia 4.2 ya kipato cha Watanzania na kwa Dodoma huduma hizo ni rahisi kuliko Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa takwimu hizo zilizopo katika tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), usafiri na usafirishaji ndio huduma ya pili kwa kuchukua sehemu kubwa ya kipato cha Watanzania sawa na asilimia 12, lakini haihofiwi katika kuhamia Dodoma.

Usafiri umefuatiwa na huduma za nyumba na makazi pamoja na huduma ambatanishi za maji, umeme, gesi na nishati nyingine, ambazo huchukua asilimia 11.6 ya kipato hicho, ingawa ndio vinavyohofiwa zaidi na wanaosubiri maagizo ya kuhamia Dodoma.

Kutokana na uhalisia huo wa asilimia 60 ya kipato cha Watanzania kutumika katika chakula, usafiri na usafirishaji na nyumba, tathmini ya gazeti hili imefanikiwa kupata taarifa kuhusu namna mtumishi anavyoweza kupata huduma hizo kwa urahisi akiwa Dodoma.

Nyumba
Ingawa jambo la kwanza ambalo watumishi wengi wanaotarajiwa kwenda Dodoma, hasa wanaomiliki nyumba zao jijini Dar es Salaam, wana hofu kubwa ni gharama za nyumba, tathmini ya gazeti hili imebaini zipo nyumba za bei rahisi kuliko za Dar es Salaam.

Tathmini hiyo imeonesha kuwa eneo lenye nyumba za gharama ya chini kabisa ni Mlimwa C, ambako huduma ni za vyumba badala ya nyumba nzima. Katika eneo hilo la Mlimwa C, kuna nyumba za bei ya chini kabisa lakini za tope, ambazo hata hivyo zimeezekwa kwa bati na zina umeme. Kodi ya chumba kimoja ni Sh 15,000.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Prosper Ganyala, alisema mbali na urahisi huo wa kodi, kutoka eneo hilo kwenda mjini ni kilometa tano tu.

Kwa mujibu wa Ganyala, pia kuna nyumba za matofali ya saruji, ambayo kodi ya chumba kimoja ni Sh 25,000 na anayetaka chumba na sebule, kodi ni Sh 35,000 lakini choo na maliwato viko nje ni vya kushirikiana wapangaji wote.

Eneo lingine lenye makazi ya bei nafuu, ni Area A ambako kodi ya chumba kimoja kwa nyumba ya kawaida, imetajwa kuwa ni Sh 30,000 kwa mwezi hadi 50,000 kulingana na hadhi ya nyumba.

Mkazi wa Area A, Nazael Mkuse amesema kodi hizo hutegemea aina ya nyumba na idadi ya vyumba vilivyo katika nyumba hiyo na kama mteja atataka nyumba nzima, atahesabiwa idadi ya vyumba vilivyopo.

“Maeneo haya chumba na sebule ni Sh 100,000 lakini vyoo huwa vya kuchangia na mitaa ya huku bado haina lami na inamlazimu mpangaji kutembea umbali wa kama robo saa hivi, ili kufika stendi ya mabasi ya kwenda mjini,” alisema.

Eneo lingine la nyumba za gharama nafuu, ni Maili Mbili, ambako imeelezwa kuwa nyumba nyingi zinapangisha vyumba badala ya nyumba nzima, ambapo chumba kisicho na dari (ceiling board), chenye sakafu ya kawaida, umeme na maji, kodi ni Sh 30,000 hadi 35,000, huduma za umeme na maji za kuchangia.

Nyumba bei juu

Akizungumza na gazeti hili wiki hii dalali wa nyumba na viwanja, Merere Yusuph, alisema nyumba za gharama za kati na juu zipo ingawa zinatofautiana kwa hadhi na bei.

“Nyumba nyingi Dodoma zina hadhi ila inategemea iko eneo gani, kukaa Kisasa, Uzunguni, Area D na Area C inategemea na hali ya mfuko wako ilivyo. “Kodi katika maeneo hayo huanzia Sh 300,000 kwa mwezi kulingana na ukubwa wa nyumba na kuendelea. Zina vyoo na maliwato ndani na nyingine zina chumba cha kulala chenye choo na maliwato ndani,” alisema.

Alitoa mfano wa nyumba za Chang’ombe Extension, kuwa zimejengwa kwa ramani na mpangilio mzuri, ambako zipo zenye uzio na zisizo na uzio na kodi huwa maelewano kati ya mwenye nyumba na mpangaji.

“Isiyo na uzio wanaanzia Sh 100,000 hadi 200,000 kwa mwezi na yenye uzio huanzia 200,000 hadi 350,000,” alisema.

Katika eneo la Kisasa, alisema kuna nyumba zenye maduka ya biashara na nyingine za ghorofa zenye huduma za starehe, ikiwemo eneo kubwa la kuegesha magari, bustani mpaka mabwawa ya kuogelea.

“Nyumba katika maeneo hayo, kodi huanzia Sh 400, 000 kwa mwezi na kuendelea na zenye mabwawa ya kuogelea bei huwa ni mapatano,” alisema.

Alipoulizwa hali ya wateja ikoje katika shughuli hiyo ya udalali wa vyumba na nyumba za kuishi, alisema tangu suala la kuhamia Dodoma lionekane halina mbadala, amekuwa akipata ofa nyingi za wakazi wa Dar es Salaam wanaotaka nyumba za kuishi na wengi wao wanataka nyumba nzima.
Usafirishaji
Huduma nyingine inayochukua sehemu kubwa ya gharama za maisha kwa Watanzania ni usafiri na usafirishaji, ambao hata hivyo watumishi wengi wa serikali hawaihofii katika suala la kuhamia Dodoma, kama wanavyoumiza kichwa kuhusu makazi.
Hata hivyo kutokana na umuhimu wake katika maisha ya watu na hasa watumishi, gazeti hili lilizungumza na madereva wa teksi na bodaboda.
Dereva teksi, Mussa Amiri alisema maeneo ambayo wamekuwa wakipata wateja kutoka mjini kwenda huko na kutoka huko kurudi mjini ni Nzuguni, Nkuhungu na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambako wanaoishi ni watu wa kipato cha kati na juu.
Kwa mujibu wa Amiri, kutoka mjini Dodoma kwenda Kisasa bei huwa ni Sh 10,000 hadi 12,000 kulingana na umbali na kwenda Nzuguni bei huwa Sh 15,000 hadi 20,000.
Alisema unapopeleka abiria katika maeneo ya Nkuhungu, bei huwa si chini ya Sh 7,000 na mtu akitaka kufika Udom, atalazimika kulipa kuanzia Sh 15,000 na kuendelea kulingana na umbali anaokwenda. “Kwenye maeneo yenye barabara za vumbi bei huongezeka,” alisema.
Taarifa zinaonesha katika maeneo ambayo gharama za makazi ziko chini kama Mlimwa C na Area A, ni nadra kupata wateja wa teksi na mara nyingi, wanaotoa huduma za usafiri ni bodaboda.
Hata hivyo, huduma hiyo ya usafiri wa pikipiki, taarifa zinaonesha kuwa zimesambaa katika maeneo mengi ya mji na bei hutegemeana na umbali wa eneo husika. Kwa maeneo yaliyo karibu bei huwa Sh 1,000 hadi Sh 2,000 na kwa maeneo ya mbali bei huwa kati ya Sh 5,000 na kuendelea.
Mmoja wa waendesha pikipiki, Yusuph Kimani alisema kupeleka abiria maeneo ya Nzuguni ni Sh 6,000 hadi 10,000; kulingana na umbali na wale wanaoenda Mkuhungu, Area C, Area D, Uzunguni bei huwa Sh 3,000 hadi Sh 4,000.
Vyakula, migahawa
Ingawa chakula na vinywaji visivyo na vilevi ndio huduma na bidhaa zinazochukua sehemu kubwa ya kipato cha Watanzania, lakini cha ajabu si miongoni mwa hofu za watumishi wa umma, katika gharama za kuhamia mkoani humo.
Akizungumza na gazeti hili mkazi wa Dodoma, Edina Mkopi alisema migahawa mingi imekuwa na bei tofauti tofauti za vyakula. Katika baadhi vyakula huanzia Sh 7,000 na mingine Sh 14,000 kwa mtu mmoja, lakini iko mingine wakiwemo mama lishe ambao vyakula huanzia Sh 1,500 hadi kati ya Sh 3,000 na 4,000.
Kuhusu upatikanaji wa vyakula kwa ajili ya kupika majumbani, taarifa zinaonesha ni mzuri na bidhaa za vyakula ni za bei nafuu kuliko Dar es Salaam kutokana na kuzungukwa na mikoa ya wakulima.
Starehe
Jambo la nne miongoni mwa mambo matatu yanayohofiwa na watumishi wa umma katika kuhamia Dodoma, mbali na nyumba, chakula na usafiri ni maeneo ya kupumzika na starehe.
Ingawa takwimu za NBS zinaonesha kuwa starehe na masuala ya utamaduni huchukua asilimia 1.6 tu ya kipato cha Watanzania na unywaji wa vilevi na utumiaji wa bidhaa za tumbaku huchukua asilimia 3.7 tu, lakini mambo hayo yanatajwa kuwa moja ya hofu kubwa za watumishi katika kuhamia Dodoma hasa vijana.
Gazeti hili lilipita maeneo ya klabu za usiku, ambako kuna matumizi makubwa ya vinywaji na starehe, ambapo ilibainika kuwa zimekuwa zikipata wateja wengi wakati wa vikao vikubwa kama Bunge na mikutano ya CCM tu.
Mkazi wa Dodoma, Emmanuel Mbaule, anayejishughulisha na biashara ya vinywaji vyenye vilevi, alisema klabu hizo huwa na watu wengi hasa kipindi cha Bunge ambapo Dodoma huwa na msongamano mkubwa wa watu, lakini baada ya Bunge wateja ni wachache.
“Sasa ukienda klabu wateja hawafiki hata 50 tena siku za mwisho wa juma kwa siku za kawaida unaweza kukuta watu hata watano,” alisema.
Hata hivyo Mbaule alisema klabu nyingi za usiku, zinahitaji marekebisho maana nyingi hazikidhi vigezo vya kisheria. Alitoa mfano wa vilabu hivyo kukosa vyumba vya kuvutia sigara na milango ya dharura, huku maeneo ya klabu yakiwa finyu.
Kuhusu baa ambazo pia zimekuwa zikitoa huduma za starehe, mapumziko na kuuza vilevi na bidhaa za tumbaku, Mbaule ambaye ni mwakilishi wa mauzo ya vinywaji hivyo Kanda ya Kati, alisema Dodoma kuna baa zaidi ya 156 lakini nyingi ziko kwenye makazi ya watu.
Maeneo ya kupumzika
Maeneo mengine ya kupumzika mbali na baa na klabu za usiku, ambayo kwa Dar es Salaam ni pamoja na katika fukwe za bahari, imeonekana kuwa mkoa huo wa Dodoma yatakuwa na changamoto kubwa.


“Dodoma haina maeneo mengi ya kupumzikia zaidi ya pale Mashujaa na Viwanja vya Nyerere, serikali ilione na hili ni kitu muhimu,” alisema mkazi wa Dodoma, Beatrice Chinyuka. Alisema maeneo hayo pia yanahitaji kuboreshwa kwa usafi maana hata viti vilivyopo ni vile vilivyojengwa kwa kutumia saruji.
Mambo 4 rahisi kuhamia Dodoma Mambo 4 rahisi kuhamia Dodoma Reviewed by WANGOFIRA on 20:56:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.