Mahakama Yatoa Ufafanuzi Wa Taarifa Iliyochapishwa na Gazeti la Mwananchi la julai 12


Mahakama ya Tanzania inapenda kutoa ufafanuzi kwa umma juu ya habari iliyoandikwa na gazeti la kila siku la Mwananchi toleo la Jumanne, Julai 12, 2016. 

Gazeti hilo lilichapisha habari ambayo Mwandishi wa habari hiyo alimnukuu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mheshimiwa Katarina Revokati akiwataka watendaji wa mahakama nchini kujenga utamaduni wa kuwajibika na kutoruhusu uhuru wa mahakama kuingiliwa na watu kutoka nje ya Mahakama.

Kutokana na habari hiyo, Mahakama ya Tanzania inakanusha taarifa hiyo kwa kuwa ililenga katika kuipotosha jamii na kuleta msuguano kati ya Mahakama na Taasisi nyingine.

Ufafanuzi wa Taarifa Hiyo
 
Mahakama ya Tanzania inapenda kutoa ufafanuzi wa alichokisema Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania wakati wa ufunguzi wa Mkutano kuhusu Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania Jumatatu Julai 11, 2016 mjini Dodoma.

Aidha, Msajili aliwataka watumishi wa mahakama nchini kutekeleza mpango mkakati kwa nia thabiti na siyo kuutumia uhuru wa mahakama vibaya kufunika maovu, badala yake aliwataka wale wenye kasoro katika utendaji wa kazi kujirekebisha wao wenyewe ndani ya mahakama la sivyo watarekebishwa hata kutokea nje kwani jamii yetu kwa sasa imedhamiria kubadilika na haitavumilia utendaji mbovu kwa kigezo cha uhuru wa mahakama.

Mahakama ya Tanzania inapenda kuujulisha umma kuwa inafanya kazi na watu wote na wadau wote nchini ili kuhakikisha nchi inaenda inavyotakiwa na haitaogopa kukosolewa kinyume na picha iliyopelekwa kwa jamii na habari iliyopotoshwa kwenye gazeti la Mwananchi.

Mahakama inashauri waandishi wa habari kuwasiliana na Mahakama endapo kuna jambo lolote linalohitaji ufafanuzi. Makosa mengine katika taarifa ni kama vile kukosea cheo kwa kusema Jaji badala ya Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na kuandika taarifa kuhusu hatua zinazochuliwa kwa Wahe. Majaji waliohusika na sakata la ESCEOW ambapo kiukweli katika mkutano huu halikuongelewa kabisa.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI, ELIMU NA MAWASILIANO
Mahakama Yatoa Ufafanuzi Wa Taarifa Iliyochapishwa na Gazeti la Mwananchi la julai 12 Mahakama Yatoa Ufafanuzi Wa Taarifa Iliyochapishwa na Gazeti la Mwananchi la julai 12 Reviewed by WANGOFIRA on 01:00:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.