Magazeti 473 Yafutiwa Usajili

SERIKALI imefuta usajili wa magazeti 473 kutokana na kutochapishwa kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema magazeti hayo yamefutwa kupitia tangazo lake lililochapishwa katika Gazeti la Serikali lenye namba 195 la Juni 10, mwaka huu.

Aliyataja baadhi ya magazeti yaliyofutiwa ni Alasiri, Dar Leo, Femina Magazine, Sauti ya Wakulima (KCU 1990) Ltd, Utamu, Raha, Starehe, Muongozo, Motomoto, Daily Times, Financial Times, Sauti ya Siti, Wakati, Hali Halisi na Mkombozi. Pamoja na magazeti hayo, pia yapo magazeti yaliyokuwa yanatolewa katika mikoa maalumu kama vile Mbeya Leo, Kilimanjaro Leo, Arusha Leo, Kigoma Yetu, Karatu Yetu, Tanga Yetu, Sauti ya Jimbo Kuu Mwanza.

Waziri Nape alisema kutokana na kufutwa kwa viapo vya usajili wa magazeti hayo, mtu yeyote atakayechapisha au kusambaza magazeti hayo kwa njia ya nakala ngumu au kielektroniki atakuwa anakiuka sheria ya magazeti hivyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

“Iwapo kuna mmiliki wa gazeti ambaye angependa kuendelea na biashara hii baada ya kufungiwa, milango ipo wazi kwa ajili ya kuwasilisha maombi mapya ya usajili kwa kufuata taratibu zilizopo, ni imani yangu kuwa kwa wale wenye nia njema wameyaelewa maelezo haya,” alisema Nape.

Pia amewataka wamiliki wa magazeti hayo yaliyofutiwa viapo wahakikishe kwamba hawavunji sheria kwa kuanza biashara bila kufuata taratibu za usajili upya na endapo watakiuka maelezo hayo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Magazeti 473 Yafutiwa Usajili Magazeti 473 Yafutiwa Usajili Reviewed by WANGOFIRA on 01:15:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.