KINANA ACHAGULIWA KUENDELEA KUWA KATIBU MKUU WA CCM

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ameandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo kwa Mwenyekiti mpya wa CCM, Rais John Magufuli, lakini Rais amekataa barua yake hiyo.

Badala yake, Rais Magufuli amemtaka Kinana na manaibu katibu wakuu wawili na sekretarieti nzima ya chama hicho, kuendelea na kazi. 

Hayo yalisemwa na Rais Magufuli wakati akitoa hotuba ya kushukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu Malumu wa CCM, mjini hapa.

“Nimepata barua ya Kinana ya kujiuzulu nafasi yake pamoja na wakuu wa idara za sekretarieti. Nimeamua Kinana na sekretarieti yote waendelee kuwepo. 

“Kama kutakuwa na haja baadaye nitaitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na siyo leo,” alisema Magufuli, akiwatangazia wajumbe hao wa kikao cha Mkutano Mkuu, ambacho ni kikao cha juu cha chama.

Alisema kwa kuwa mkutano huo ndiyo wenye uamuzi wa mwisho kuhusu masuala ya chama, hivyo anawauliza wajumbe kama wamekubaliana na pendekezo lake hilo la Sekretarieti ya chama iendelee.

“Nawauliza wajumbe mnaafiki?” Ambapo wote kwa kauli moja walisema; “Ndiyo.” Magufuli alisema kulikuwa na watu waliokuwa wamejipanga kuchukua nafasi hizo za sekretarieti, lakini “sasa imekula kwao”. Hakutaja watu hao.

Akiongeza kuwa; “Nitaendelea kuwa na Kinana na nina imani yeye na sekretarieti nzima watasimamia vizuri mambo kadhaa niliyoagiza yasimamiwe haraka.”

Magufuli alisema CCM ni chama cha aina yake duniani, kwa kuwa kila upande kuna fursa ya ushauri kutoka kwa wazee wastaafu (huku akiwataja kwa majina), jambo linalofanya kazi iliyo mbele yake kuwa nyepesi.

Rushwa
Akizungumzia kuhusu utendaji wa chama na upitiaji wa muundo wa chama, Magufuli alionya kuwa katika uongozi wake mwanachama atakayetumia fedha kuomba uongozi, hatapita.

Alikumbusha wakati wa kuomba udhamini ili ateuliwe kugombea urais kupitia CCM, kwamba alifika Iringa akakuta Wilaya moja wanachama wote wamenunuliwa, akalazimika kwenda vijiji vya mbali kupata wadhamini.

Magufuli alisema rushwa aliyosema iko ndani ya chama hicho, imekuwa ikiwanyima haki wanachama wengine kugombea na matokeo yake, vyeo vimekuwa vikishikwa na watu wenye fedha na kuacha watu muhimu kwa sababu hawana fedha.

Vyeo kufutwa
Aidha, aliahidi kuongeza maslahi ya wafanyakazi wa chama hicho lakini akaonya kuwa kuna baadhi ya vyeo ambavyo haoni kama vina tija katika siasa za sasa, ambavyo anafikiria kuviondoa.

Alitoa mfano wa makamanda wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), walezi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), washauri wa Jumuiya ya Wazazi na chipukizi, ambao alisema wengi ni wa umri wa kuanzia miaka nane mpaka 15, ambao wanapaswa kuwa shuleni.

Mwenyekiti huyo pia alisisitiza umuhimu wa mwanachama mmoja cheo kimoja na kuonya kuwa hapendi kuona mawaziri, ndio wajumbe wa NEC, ndio makamanda wa vijana na kusema hali hiyo inawanyima cheo wanachama wengine.

Mali za chama 
Kuhusu mali za chama hicho, aliagiza sekretari hiyo nayo kuzifuatilia, kuziorodhesha na kuhakiki mali ipi inaingiza mapato yapi na yanakwenda wapi. 

Kuhusu ada za wanachama wanaozidi milioni 8.7, ambao Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete alisema kama kila mmoja angelipa ada ya Sh 1,200 kwa mwaka, chama hicho kingepata zaidi ya Sh bilioni nane na kuondokana na ukata wa kutegemea ruzuku, Magufuli aliagiza uhamasishaji wa kulipia ada ufanywe na malipo yawe kwa njia ya kielektroniki.

Kinana 
Akizungumza baada ya kurejeshwa madarakani, Kinana alisema baada ya kuandika barua hiyo ya kujiuzulu na hata kuzungumza na Magufuli, amejikuta akigonga mwamba na hivyo anajipanga kuomba tena kupumzika.

Alisema alipokuwa akifanya kazi, kuna wakati alidhani yuko mwenyewe lakini Mwenyekiti Kikwete, alimpigia simu na kumwambia kuwa anamuunga mkono, jambo lililomtia moyo.
KINANA ACHAGULIWA KUENDELEA KUWA KATIBU MKUU WA CCM KINANA ACHAGULIWA KUENDELEA KUWA KATIBU MKUU WA CCM Reviewed by WANGOFIRA on 20:34:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.