Kikwete: Nipo Tayari Kuutumikia Umoja wa Afrika (AU) Ikiwa Ntapewa Majukumu Hayo

RAIS mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema yuko tayari kuitumikia Afrika kwa nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika katika Umoja wa Afrika (AU), ikiwa atapewa majukumu hayo.

Alisema akiteuliwa kushika nafasi hiyo atakubali, lakini hawezi kuiomba kwa kuandika barua.

Alisema hayo jana Dar es Salaam alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu kutajwa kwa jina lake kwamba ana nafasi kubwa ya kushinda nafasi hiyo katika uteuzi utakaofanywa siku chache zijazo ili kumrithi Mwenyekiti wa sasa, Nkosazana-Dlamini Zuma wa Afrika Kusini.

“Inawezekana mtu alikaa mahali akasema hawa ndio watatu wanaweza kutufaa, lakini mimi siwezi kuandika barua kuomba kazi yoyote,” alisema.

Mwanadiplomasia huyo maarufu alisema amefanya kazi kubwa kuliko zote ambazo binadamu anaweza kufanya ambayo ni kazi ya kuwa Rais wa nchi yake, hivyo hakusudii tena kuandika barua ya kuomba kazi. Alisema kama viongozi wa Afrika wakiamini kuwa anaweza kushika nafasi hiyo na kuongoza, yuko tayari kujitolea kama kiongozi wa Afrika, lakini si kuiomba.

Alisema, “Ili kuwa Mwenyekiti lazima uombe, mimi si mgombea na waliogombea wapo. Watu wananiombea heri, In Shaa Allah, lakini haliwezekani kwa sababu sijaomba.” 

“Naandika barua na nani anaomba na mwingine anaomba, hapana jamani si vizuri. Wakiridhika viongozi wa Afrika wakasema hapa tunakuomba utusaidie ntafanya siwezi kuipa Afrika kisogo,” Kikwete alisema.

Katika tukio jingine, Kikwete alizitaka nchi za Afrika zinazoingia katika mapinduzi ya viwanda kuzingatia athari za tabia nchi zenye madhara makubwa.

Alitoa rai hiyo alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili wa watafiti na wataalamu wa athari za mabadiliko ya tabia nchi duniani, unaojadili namna ya kutekeleza mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema nchi isipopanga maendeleo yake vizuri itafika mahali mazingira yataharibika na kuwa na madhara makubwa, hivyo ni wajibu wa nchi zote duniani kulishughulikia.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja, alimtaja Kikwete kuwa shujaa aliye mtari wa mbele kupambana na tatizo hilo la athari za tabia nchi.
Kikwete: Nipo Tayari Kuutumikia Umoja wa Afrika (AU) Ikiwa Ntapewa Majukumu Hayo Kikwete: Nipo Tayari Kuutumikia Umoja wa Afrika (AU) Ikiwa Ntapewa Majukumu Hayo Reviewed by WANGOFIRA on 20:39:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.