JPM AWAASA WATANZANIA KUTUNZA AMANI
RAIS John Magufuli amewataka Watanzania wasichezee amani kwa kuwa Tanzania ni nchi pekee iliyobakia kuwa kisiwa cha amani.
“Tusichezee amani. Tuidumishe amani yetu kwani kuna watu walijitoa
mhanga kupigania amani hiyo na kuifikisha nchi hapa ilipo,” alisema Rais
Magufuli mjini hapa jana alipohutubia maelfu ya wakazi wa Dodoma na
Watanzania katika sherehe ya Siku ya Mashujaa.
Rais Magufuli aliyeshangiliwa na wananchi waliokuwa wakipunga bendera
ndogo za Taifa baada ya kupanda jukwaani, alisema kuwa wakati
tunaadhimisha Siku ya Mashujaa tukumbuke wapo watu walikubali roho zao
zipotee.
Alitoa mfano wa waliopigania ukombozi wa nchi mbalimbali barani
Afrika kama Msumbiji, Namibia, Angola, Comoro na Afrika Kusini. Wengine
ni waliopigana vita ya nduli Iddi Amin wa Uganda mwaka 1977, wakati
nduli alipovamia Tanzania na wakati wa Mapinduzi kisiwani Zanzibar mwaka
1964.
Aliwataja mashujaa wengine wa Taifa ambao hawawezi kusahaulika kwa
mchango wao mkubwa katika ukombozi wa nchi kuwa ni Baba wa Taifa ,
Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Abeid Amaan Karume wa Zanzibar.
Alisema waasisi hao walijitahidi kuifikisha nchi hapa ilipo.
“Tanzania imekuwa na amani na utulivu kwa sababu wapo watu waliojitoa
mhanga kuipigania. Tudumishe amani yetu. Hawa wenzetu waliotangulia,
hawakujali dini zao na makabila yao. Walijitahidi kuwaunganisha
Watanzania wote,” alisema Rais Magufuli na kuwataka Watanzania
wasichezee amani na asitokee wa kuichafua kwani kila mmoja ana wajibu wa
kuidumisha. Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi
aliwataka Watanzania kulinda umoja na amani ya nchi.
Aliwataka kuendelea kumuombea dua Rais Magufuli ili awe mwepesi
katika kutekeleza yote anayodhamiria kwakuwa amepewa dhamana kubwa ya
kuongoza Watanzania zaidi ya milioni 40.
“Tuache ushetani, tuache ubilisi, tushughulike na yale yanayotuhusu
sisi wenyewe, watoto wetu na vizazi vyetu. Tudumishe utulivu na
kupendana. Heri na amani haiji bila kupatikana usawa,” alisema na
kuongeza kuwa Rais Magufuli amekuwa kiongozi wa watu, anayepigania watu
wanaokosa haki, wanaoonewa na wanaofanyiwa fitna.
Alisema amani ni kitu muhimu sana hivyo Watanzania wafunge masikio
wasisikie mabalaa na machafuko yanayotokea katika nchi jirani. Aliongeza
kuwa, Mungu katujalia amani hivyo tuidumishe ili asitokee mtu
kuiharibu.
“Asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Huko nje maguu yanavunjika na
yataendelea kuvunjika,” alionya Mwinyi. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed
Shein alisema atashirikiana na Rais Magufuli kuimarisha amani ya
Tanzania.
Alisema anafahamu uwezo, nia, ari, jitihada na kasi ya Rais Magufuli
ya kuipeleka Tanzania kuwa nchi yenye matumaini na maendeleo makubwa.
Akitoa dua katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Baraza Kuu la
Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Kaimu Shehe wa mkoa wa Dodoma, Ahmed
Said, alisema Watanzania wanathamini mchango mkubwa walioutoa mashujaa
waliopigania nchi na kwamba mchango wao utaendelea kuthaminiwa.
Alisema umoja na amani havikushuka nchini kama mvua, bali wazee na
askari walitoa jasho na kupoteza maisha kwa ajili ya nchi ndio
waliosababisha viwepo.
Alisema Watanzania hawawezi kusahau waasisi walioongoza mapambano
wakiwemo Mwalimu Julius Nyerere, Shehe Abeid Amaan Karume na Rashidi
Kawawa.
“Tunamuomba Mungu aendelee kuilinda nchi yetu na kudumisha amani,
utulivu na umoja uliopo,” alisema Shehe Said. Pia, Shehe Said aliwataka
Watanzania waendelee kumuombea Rais Magufuli awe na moyo wa ujasiri,
subira na afya njema ili aweze kuongoza nchi kama ilivyokusudiwa.
Aliomba Mungu awaepushie shari viongozi wanaomsaidia Rais Magufuli
kuongoza Serikali. Shehe huyo aliomba Mungu ailinde Tanzania na
Watanzania kwa ujumla na pia aubariki Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ili uendelee kudumu.
Mchungaji Leonard Mtaita akifanya maombi kwa niaba ya Umoja wa
Makanisa ya Kikristo (CCT), alisema waasisi wa Taifa wametoa mchango
mkubwa katika kujenga na kudumisha amani.
Aliwataka Watanzania kudumisha upendo na amani kama njia ya kuwaenzi.
Mtaita aliwahimiza Watanzania waendelee kumuombea Magufuli aendelee
kuwa na afya njema, hekima na busara ili kuwatumikia Watanzania.
Alimsifu Rais kwa kuwatumikia kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
Padri Onesmo Wisi alifanya maombi kwa niaba ya Baraza la Maaskofu
Katoliki Tanzania (TEC), alisema Watanzania wanafurahia amani ambayo
waasisi na askari wetu waliipigania. Aliwahimiza kuwa na umoja ili
kulinda amani iliyopo na kujiepusha na uchochezi wa kisiasa, ambao
mwisho wake ni vurugu.
Katika maadhimisho hayo, shughuli zilizofanyika ni pamoja na kuweka
silaha za asili za mashujaa na maua kwenye mnara, ambapo Rais Magufuli
aliweka mkuki na ngao na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali
Davis Mwamunyange aliweka sime. Kiongozi wa Mabalozi nchini, Balozi
Ambrosio Lukoki aliweka shada la maua.
Lukoki ni Balozi wa Angola nchini. Meya wa Dodoma, Jaffar Mwanyemba
aliweka upinde na mshale na Mwenyekiti wa Tanzania Legion, Rashid Bakar
Ngonji aliweka shoka.
Pia mizinga miwili ilipigwa katika sherehe hizo zilizopambwa na
gwaride maalumu. Maelfu ya wakazi wa Dodoma walihudhuria sherehe hizo.
Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa sherehe za Siku ya Mashujaa kufanyika
nje ya Dar es Salaam.
JPM AWAASA WATANZANIA KUTUNZA AMANI
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:46:00
Rating:
No comments: