Alichokisema Rais Magufuli Baada ya Kuchaguliwa Kuwa Mwenyekiti wa CCM
MWENYEKITI
wa tano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli, amewaomba
wanachama wa chama hicho kumuombea kwa Mungu ili apate uvumilivu wa
mtangulizi wake, Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete.
“Mzee Kikwete wewe una moyo wa uvumilivu. Sina hakika kama mimi ninao uvumilivu kama wako...umetupa fundisho kubwa sana,”
alisema Magufuli wakati akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya
kuchaguliwa kwa kura asilimia 100 kuwa Mwenyekiti wa chama hicho.
Katika
kuonesha tofauti yake na Kikwete katika uvumilivu, Magufuli alikumbusha
changamoto aliyokutana nayo Kikwete, wakati alipoingia katika kikao cha
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM mwaka jana, kupeleka mapendekezo
ya majina ya wagombea watano wa urais waliokuwa wamepitishwa na kikao
cha Kamati Kuu, ili wapigiwe kura.
Ndani
ya kikao hicho wakati Kikwete, wajumbe wa Kamati Kuu na wa Baraza la
Wazee la Ushauri wakiingia, baadhi ya wajumbe wa kikao hicho walikiuka
utaratibu wa siku zote wa chama hicho, kwa kuimba kuwa na imani na mmoja
wa wagombea wa urais, Edward Lowassa, ambaye jina lake lilikatwa katika
kikao cha Kamati Kuu.
Kupotezwa
“Siku
ile umeingia ukumbini, watu wakawa wanaimba kuwa wana imani na mtu
mwingine, siku hiyo hiyo robo au nusu yao wangepotea...sifahamu, umetoa
fundisho kwa sisi vijana kwamba saa nyingine uvumilivu ni kitu muhimu,” alisema akimaanisha kama hali hiyo ingemkuta yeye ndiye Mwenyekiti, hayo ndiyo yangetokea.
Kutokana
na uvumilivu aliouonesha Kikwete katika mkutano huo, Magufuli aliwataka
wanachama hao wa CCM kumuombea kwa Mungu, ili apate angalau nusu ya
uvumilivu wa Kikwete, ili katika uongozi wake mambo yaende salama.
Kuzushiwa JK
Alimsifu
Kikwete kwa kutumia hekima ya uvumilivu, kwa kuwa kiongozi huyo
mstaafu, amesemwa mambo mengi, akazushiwa na hata kutukanwa kutokana na
hatua, uamuzi na vitendo vyake Magufuli.
“Umesemwa
mengi, umetukanwa mengi na umezushiwa mengi kwa ajili yangu, lakini kwa
upendo wako na kwa kumtegemea Mungu, ukakaa kimya...sina cha kukulipa,
bali nitafanyia kazi Watanzania na hasa wana CCM kwa nguvu zote,” alisema Dk Magufuli.
Alitoa
mfano wa Kikwete kuzushiwa alikuwa akikataa kumkabidhi Dk Magufuli
uenyekiti wa CCM kwa kufuata desturi ya chama hicho, akasema Mwenyekiti
huyo mstaafu amemshawishi mara nne, lakini yeye ndiye aliyekuwa
akikataa.
“Nakumbuka
umeniambia mara nne, ya kwanza ulikuja kuniambia nikakukatalia bosi
wangu, ulinipigia simu na mimi nikawa naanzisha mjadala mwingine. Nakupa
pole na unisamehe sana kwa kuwa kukukatalia kulisababisha utukanwe,” alisema Rais Magufuli.
Serikali Dodoma
Kabla
ya kumaliza hotuba yake, Magufuli alitangaza ahadi kwa wanachama hao,
kuwa amebakiza miezi minne na miaka minne kabla ya kumaliza kipindi
chake cha miaka mitano na kusema kabla ya kumaliza kipindi hicho,
atakuwa amehamishia serikali yote Dodoma.
Magufuli
alisema kwa sasa miundombinu ya Dodoma inawezesha serikali kuhamia
huko, kwa kuwa barabara za kutoka Makao Makuu hayo ya serikali kwenda
sehemu mbalimbali nchini, zinapitika kwa lami.
Mbali
na barabara, alisema pia huduma kwa ajili ya maisha ya watu nazo
zinapatikana kwa kuwa mkoa huo una uzoefu wa kuhudumia wabunge, wajumbe
wa Mkutano Mkuu wa CCM na mikutano mingine, huku mkoa huo ukiwa na Chuo
Kikuu cha Dodoma, ambacho ndio kikubwa kuliko vyote nchini.
Alisema,
akihamia yeye katika Ikulu ya Chamwino ambayo alisema ina kila huduma
anayohitaji, anatarajia Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri na
serikali nzima itamfuata.
Babu wa demokrasia
Magufuli
alisema CCM ndio chama kilicholea demokrasia hapa nchini na kinaendelea
kutoa ulezi huo na kufafanua kuwa chama hicho ndio babu na bibi wa
demokrasia; baba na mama wa demokrasia na kaka na dada wa demokrasia kwa
vyama vyote nchini.
Alisema
kwa kuwa Serikali anayoiongoza inatekeleza Ilani ya chama hicho, hivyo
chama hicho ndio mabosi wa mabosi wote serikalini na kuonya kuwa ambaye
hataki hilo, ataondolewa.
Kupendekezwa kwake
Awali
wajumbe wa Mkutano huo Mkuu Maalumu wa CCM wapatao 2,398 walimpigia
kura ya kumchagua Magufuli kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho.
Mwenyekiti
aliyemaliza muda wake, Kikwete ndiye aliyesoma pendekezo la NEC kwa
wajumbe wa mkutano huo kuhusu mgombea wa nafasi hiyo.
“Madhumuni
ya mkutano huu ni kuchagua mwenyekiti mpya. Sisi katika Halmashauri Kuu
tunampendekeza kwenu Mheshimiwa Dakta John Pombe Joseph Magufuli ashike
nafasi hiyo,” alisema Kikwete saa 7:10 na kauli yake hiyo kupokelewa kwa shangwe, vifijo na vigelegele.
Akimwelezea
Magufuli, Kikwete alisema ana imani isiyo na hata chembe ya shaka kuwa
atafanya kazi hiyo vizuri, kwa sababu ya imani na mapenzi yake makubwa
kwa chama hicho na Watanzania.
Alisema
Magufuli ametumikia Taifa na wananchi kwa miaka mingi kwa uaminifu na
uadilifu mkubwa, katika wadhifa mbalimbali aliokuwa nao. Alisema
Magufuli amekuwa mbunge na waziri kwa miaka 20, ambapo miaka 10 wakati
wa serikali ya Rais Benjamin Mkapa na mingine 10 wakati wa serikali
yake.
Alisema
pia Magufuli amekuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya na mkoa,
mjumbe wa mkutano mkuu wa wilaya na mkoa na mjumbe wa mkutano mkuu wa
taifa kwa miaka 20, hivyo anakijua mno chama.
Kikwete
alisema Magufuli ameongoza nchi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa katika
kipindi kifupi cha miezi 8 tangu alipochaguliwa, hivyo sasa anafaa kuvaa
kofia zote mbili.
“Kichwa chake sasa kinatosha avae kofia zote mbili - ya urais na uenyekiti wa chama. Nawaomba wajumbe wote tumuunge mkono.
“Tumpe kura zote za ‘Ndiyo’ na isipotee hata moja,” alisema Kikwete ambaye ameng’atuka baada ya kuongoza Chama tangu Juni 2006.
“Mimi
naondoka na bila shaka yoyote namwachia Chama Cha Mapinduzi Rais Dakta
John Pombe Joseph Magufuli. Nakiacha Chama Cha Mapinduzi katika mikono
salama na nina hakika kitapata maendeleo makubwa ya haraka,” alisema.
Kura zatangazwa
Kazi
ya kupiga kura na kuzihesabu ilipokuwa ikiendelea, viongozi wakuu wa
CCM na wastaafu baada ya baadhi yao kupiga kura, waliondoka kwa ajili ya
mapumziko.
Baada
ya mapumziko, walirejea ambapo baada ya salamu za wageni na baadhi ya
wanasiasa waliorejea CCM baada ya kukimbilia upinzani kumalizika,
Kikwete alisoma matokeo.
Akitangaza
matokeo hayo, Kikwete alisema kura zilizopigwa zilikuwa 2,398,
zilizoharibika sifuri na hivyo kura halali zikawa 2,398.
Kikwete
aliendelea kuwa matokeo yameonesha kuwa, kura za Hapana ni sifuri na
kura za ndio ni 2,398, na hivyo Magufuli amepitishwa na wajumbe wa CCM
kwa nidhamu ya juu ya kumpa asilimia 100 ya kura.
Makamu wenyeviti
Awali,
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema mkutano mkuu huo usio wa
kawaida, unafanyika kwa mujibu wa Kifungu cha 7 (103) (4) cha Katiba ya
CCM na ajenda yake ni kumchagua mwenyekiti mpya, kufuatia uamuzi wa
Kikwete kung’atuka, akitekeleza utamaduni wa chama kuachiana madaraka,
ili kumpisha Rais John Magufuli.
Aidha,
alisema kwa mujibu wa Kifungu 7 (105) (5) (a) cha Katiba hiyo,
unapofika wakati wa uchaguzi kazi mojawapo ya mkutano mkuu ni kuchagua
makamu wenyeviti.
Lakini, alisisitiza makamu wote wawili wa sasa, muda wao haujamalizika kikatiba na utamalizika mwezi Novemba 2017 “Makamu
wote wawili hawajamaliza muda wao. Muda wao utamalizika Novemba 2017,
hivyo hakuna sababu ya kuwachagua tena. Hapa leo tunachagua mwenyekiti
peke yake,” alitangaza Kinana.
Makamu Mwenyekiti wa CCM kwa upande wa Bara ni Phillip Mangula na upande wa Zanzibar ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Viongozi
wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na marais wastaafu, Ali
Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais wa Zanzibar Dk Shein , mawaziri wakuu
wastaafu Mizengo Pinda, Cleopa Msuya, Dk Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph
Warioba, John Malecela, Makamu wa Rais mstaafu Mohamed Gharib Bilal na
makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Wilson Mukama.
Alichokisema Rais Magufuli Baada ya Kuchaguliwa Kuwa Mwenyekiti wa CCM
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:32:00
Rating:
No comments: