Waziri Mkuu alia na mauaji dhidi ya raia
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amekemea matukio ya mauji yanayoendelea nchini na kusema kuwa hakuna dini inayofundisha vitendo hivyo viovu.
Alisema serikali inawaomba viongozi wa dini nchini kuendelea
kushirikiana nayo kutoa elimu kwa waumini wao kama njia ya kukomesha
mauaji dhidi ya watu wasiokuwa na hatia nchini.
Akizungumza Dar es Salaam jana katika fainali ya mashindano ya
kimataifa ya kuhifadhi Koran nchini, alisema ni wajibu kwa
Watanzania kushikana kulinda amani ya nchi.
“Napenda nigusie mambo machache ambayo nimeyaona; ni hivi karibuni
nchi yetu ilingia katika mtihani ambao wengi wenu kupitia vyombo vya
habari mliarifiwa juu ya kuuawa kwa waumini wema waliokuwa wakifanya
ibada ndani ya msikiti kule mkoani Mwanza.
“Katika siku za hivi karibu kumekuwa na matukio mabaya mbele ya macho
yetu na nchi yetu imefika mahala hadi watu wanafuatwa majumbani na
kuchinjwa jambo ambalo kwetu sisi kama Serikali tuna kazi ya kulinda
uhai wa kila Mtanzania.
“Linapotokea suala kama hili hatuwezi kula wala kulala mpaka tuone
juhudi za dhati katika kukomesha unyama wa aina hii,” alisema Majaliwa.
Alisema Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama inaendelea
kushughulikia tatizo hilo kwa umakini na akawataka Watanzania kuendelea
kutoa ushirikiano.
Akizungumzia utendaji wa Serikali ya awamu ya tano, alisema watendaji
wengi ni wapya huku akiomba kukoselewa inapokosea jambo ambalo
litasaidia kujenga Serikali imara na yenye mshikamano.
Mashindano hayo ya kuhifadhi Koran yalihusisha washiriki 21 kutoka
mataifa mbalimbali duniani huku kijana, Rashid Ally (8) kutoka
Tajikistan akiibuka mshindi wa kwanza.
Waziri Mkuu alia na mauaji dhidi ya raia
Reviewed by WANGOFIRA
on
11:57:00
Rating:
No comments: