Wananchi Watinga Mahakamani Kufungua Kesi ya Kupinga Agizo la Serikali Kuzuia Matangazo ya Moja kwa Moja ya Bunge

HATUA ya serikali kuzuia kurusha moja kwa moja mjadala wa vikao vya Bunge kama ilivyokuwa awali, bado inaumiza wananchi.
 
Safari hii wananchi wametinga mahakamani na kwamba leo wamefika katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kufungua kesi ya kuitaka mahakama hiyo kutengua agizo la serikali la kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Januari mwaka huu, Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Michezo na Sanaa alilieleza Bunge hatua ya kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya chombo hicho kama ilivyokuwa awali.

Miongoni mwa sababu alizotoa ni kwamba, serikali imekuwa ikibeba mzigo mkubwa wa gharama katika kuendesha matangazo hayo pia watumishi wa umma kutumia muda mwingi kuangalia Bunge badala ya kufanya kazi.

Hatua ya serikali kuzuia kurusha matangazo hayo ya moja kwa moja imeibua mjadala mkubwa kitaifa ambapo kada mbalimbali nchini zimekuwa zikipinga hatua hiyo.

Katika kesi iliyofunguliwa leo, ina walalamikaji 10 ambao ni Azizi Himbuka, Perfect Mwasililwa, Rose Moshi, Penina Nkiya, Andrew Mandari, Hilda Sigara, Juma Uloleulole, Kubra Manzi, Ray Kimbito na Ben-Rabiu Saanane.

Kesi hiyo imesikilizwa na Profesa Ferdinand Wambari, Jaji Kiongozi katika mahakama hiyo, na jaji mwengine katika kesi hiyo Sakieti  Kihiyo, hata hivyo hakuwepo mahakamani leo.

Washtakiwa kwenye kesi hiyo ni Nape pamoja na George Masaju, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ambapo Abubakari Mrisho, ndio wakili wa upande wa walalamikiwa.

Kwa upande wa walalamikaji unasimamiwa na Peter Kibatala na Omari Msemo ambao ni mawakili wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kesi ya msingi iliyofunguliwa ni kuitaka mahakama kutengua uamuzi uliotolewa na Nape ambaye aliwasilisha kauli ya serikali bungeni.

Walalamikaji wanaitaka mahakama itangaze kuwa, Raia wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wana haki ya kikatiba ya kujua majadiliano yanayoendelea bungeni kwa mujibu wa ibara ya 18(B), (d) na 29 (1).

Pili walalamikaji wamedai kuwa, serikali imekiuka haki ya kikatiba kwa kuzuia bila kuwa na sababu za msingi haki ya wananchi kusikia majadiliano ya Bunge kwa kuzuia kurusha matangazo ya moja kwa moja.

Tatu, walalamikaji wameitaka mahakama kuilekeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kurejesha haki ya kikatiba ya wananchi kwa kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Nne, walalamikaji wamedai kuwa, matokeo ya kuzuia matangazo hayo ni kunyimwa kwa haki za Watanzania kutokana na kushindwa kuwasimamia pia kuwafuatilia wabunge na mwenendo wao bungeni.

Tano, walalamikaji hao wamedai kuwa, sababu za kuzuia matangazo hayo hazijitoshelezi hivyo Watanzania na walalamikaji wanayo haki ya kupata taarifa ya vikao vya Bunge  kwa maslahi ya taifa.

Hata hivyo upande wa utetezi ulidai kuwa, walichelewa kupata taarifa ya mashtaka hayo hivyo hawakupata muda wa kutosha wa kuaandaa majibu. Kutokana na hivyo, mahakama iliuambia upande wa walalamikiwa kwamba, watajibu mashtaka hayo 15 Julai siku ambayo kesi hiyo itatajwa.

Wananchi Watinga Mahakamani Kufungua Kesi ya Kupinga Agizo la Serikali Kuzuia Matangazo ya Moja kwa Moja ya Bunge Wananchi Watinga Mahakamani Kufungua Kesi ya Kupinga Agizo la Serikali Kuzuia Matangazo ya Moja kwa Moja ya Bunge Reviewed by WANGOFIRA on 11:45:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.