Kiswahili kinazidi kupasua anga
TANZANIA inatarajiwa kuanza kutumia Kiswahili katika mikutano yote ya
kimataifa itakayowakilishwa na viongozi wake baada ya serikali
kukamilisha kutuma wataalamu watakaotafsiri lugha hiyo kwa watumiaji wa
lugha nyingine duniani.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma
katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu. Kauli ya
Majaliwa ni jibu kwa swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Zainabu Vulu (CCM)
aliyehoji namna serikali inavyoenzi lugha ya Kiswahili aliyoitumia Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuunganisha taifa. Majaliwa anasema,
vyuo vikuu duniani kote vimeanza kufundisha Kiswahili hivyo kuongeza
mahitaji ya walimu wa kufundisha lugha hiyo kutoka Tanzania.
Anasema, vyuo vikuu nchini vinafundisha walimu wa lugha hiyo kukidhi
mahitaji kwenye soko la kimataifa, lakini pia serikali inajiandaa
kupeleka nje wataalamu wa kutafsiri Kiswahili. Chama cha Wafanyakazi wa
Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kimempongeza Waziri Mkuu kwa tamko hilo la Juni 16 mwaka huu.
Kinaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi za kukuza na
kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa kuwa ni tunu ya taifa.
Kinasema, tamko la kutumia Kiswahili kuwa lugha kuu ya mawasiliano
katika ofisi za serikali na vikao vya ndani n a v y a kimataifa ni jambo
jema. T H T U inaipongeza serikali kwa kuboresha utumishi wa umma,
kudhibiti watumishi hewa serikalini na kusitisha ajira kwa muda ili
kuboresha mchakato wa ajira nchini. Kinasema, juhudi za serikali
zitawezesha kufahamu idadi ya watumishi hivyo kuwa rahisi kuboresha
maslahi na wakati huohuo ikiongeza ajira kwa kukuza Kiswahili kuongeza
pato la taifa.
Mwenyekiti THTU Mlimani, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Salifius Mligo
anasema wameona lugha ya Kiswahili inavyozidi kukua kwa kasi barani
Afrika, Afrika Mashariki na nje ya Bara la Afrika. Anatoa mfano wa Bunge
la Afrika kuwa linatumia lugha ya Kiswahili. Anasema lugha hiyo
inafundishwa katika vyuo na shule za serikali na watu binafsi katika
nchi kadhaa ikiwemo Ghana, Libya, Zimbabwe, Namibia, Misri, Aljeria,
Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda. Bara la Asia ni China,
Japan, Korea Kusini na India.
Ulaya ni Ujerumani, Italia, Uholanzi, Uingereza, Sweden, Ufaransa na
Austria. Kwa Amerika ya Kaskazini ni Marekani na Canada. Amerika ya
Kusini ni Mexico na Jamaika, na Australia ni katika miji ya Melbourne,
Sydney na Adelaide. Mligo anasema, lugha ya Kiswahili inatumika kama
lugha ya mawasiliano na biashara katika nchi za DRC, Namibia, Afrika
Kusini, Zimbabwe, Malawi, Msumbiji, Comoro, Zambia, Madagaska, Oman na
nchi zote za Afrika Mashariki.
Anasema juhudi za serikali haziishi katika kukuza lugha tu bali pia
kuitangaza Tanzania kimataifa na kukuza biashara. “Ni juhudi
zinazoijengea lugha ya Kiswahili heshima inayostahili. Aidha kwa hapa
Tanzania Kiswahili kimekuwa lugha ya taifa,” anasema Mligo. Anasema,
kiongozi wa k i t a i f a anapokuwa ndani au nje ya nchi hana budi
kulitangaza taifa lake na kujivunia. Kwa mujibu wa Mligo, viongozi
wakizungumza Kiswahili inadhihirisha uhuru walionao na kutangaza wazi
sera ya kujitegemea kwa nchi yetu.
Kiswahili ni lugha ya kibantu na ni lugha ya Kiafrika. Kwa kuijenga
na kuiendeleza serikali pia inajenga umoja na mshikamano wa Waafrika kwa
kutumia lugha ya Kiafrika. “Jambo hili linaungwa mkono na azma
waliyokuwa nayo waasisi wa mataifa ya Kiafrika, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, Kwame Nkrumah, Kenneth Kaunda na wale walioko sasa hivi kama
vile Robert Mugabe katika kuijenga Afrika Moja,” anasema.
Anaiomba serikali iendelee na utekelezaji wa suala hilo kwa kusimamia
na kutoa maagizo na kuhakikisha yanatekelezwa. Anasema serikali
inatakiwa kutoa waraka maalumu wa kurasimisha matumizi rasmi ya
Kiswahili katika taasisi zote za umma kutumia Kiswahili katika
mawasiliano yote na kuacha matumizi ya Kiingereza. Mligo anasema, katika
maazimio hayo, watumishi wote wanaokwenda kuwakilisha serikali ya
Tanzania nchi za nje wakipewa ruhusa lazima wapewe pia waraka rasmi wa
kutumia na kukitangaza Kiswahili huko waendako.
Wachezaji mpira, wasanii na wanamichezo wanaporuhusiwa kwenda nje ya
nchi kuiwakilisha Tanzania, wapewe bendera na waraka wa kutumia
Kiswahili kuitangaza nchi yetu. “Mheshimiwa Waziri Mkuu tamko lako
bungeni limekuja katika wakati muafaka ambao tunazungumzia umoja wa nchi
za Afrika na dunia. “Ni imani yetu kwamba lugha ya Kiswahili
ikizungumzwa ipasavyo itakuwa ni kiungo kikubwa sana cha watu duniani.
Na hii itasaidia sana kuinua uchumi wa Watanzania na Afrika kwa ujumla,”
anasema Mligo.
Anasema, wana imani na utendaji wa serikali hivyo katika maboresho
yanayofanywa kwenye utumishi wa umma, matumizi ya Kiswahili yawe ni
sehemu ya mikakati itakayotekelezwa. Profesa kutoka Taasisi ya Taaluma
za Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Aldin Mutembei
anasema chuo hicho kilianza kufundisha Kiswahili mwaka 1930. Anasema
mwaka 2009/10 kilianza kufundisha shahada ya kwanza ya Kiswahili na
kuendelea na shahada ya pili.
“Sisi tulianza mapema kabla ya wenzetu lakini tulichelewa kuanza
kutoa shahada,” anasema Mutembei. Anasema, walimu wengi kutoka UDSM
wamepelekwa nje ya nchi kufundisha lugha ya Kiswahili. Kuna taarifa
kwamba, kuanzia Julai mwaka huu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitaanza
kutumia lugha ya Kiswahili kuwasiliana katika vikao vyote isipokuwa
kufundishia darasani.
Machi mwaka huu, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Anastazia Wambura amewataka watendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa
(Bakita), kujitangaza na kushiriki katika matukio ya kitaifa na
kimataifa kuhamasisha matumizi ya lugha ya Kiswahili ili kiweze
kufahamika na kutumika na mataifa mengine. Katibu Mtendaji wa Bakita, Dk
Selemani Sewange anasema baraza hilo limekuwa likishiriki katika Bunge
la Afrika na Umoja wa Afrika hivyo kutangaza lugha ya Kiswahili.
Serikali imekusudia kupeleka wataalamu wa Kiswahili katika nchi
mbalimbali ili kuwezesha viongozi kutoka Tanzania wanapokwenda katika
mikutano ya kimataifa, watumie Kiswahili na wataalamu hao watoe tafsiri
kwenda kwenye lugha nyingine za kimataifa. Tanzania imepeleka walimu wa
Kiswahili nchini Burundi, Rwanda, Uingereza na Ufaransa ambako
wanafundisha lugha hiyo. Kati ya lugha kubwa za kimataifa, Kiswahili
kama si lugha ya sita ni ya nane.
Imeandaliwa na Lucy Ngowi.
Kiswahili kinazidi kupasua anga
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:47:00
Rating:
No comments: