Takukuru na TRA wataja mwizi EFDs
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) hatimaye wametaja
mfanyabiashara ambaye alibainishwa na Rais John Magufuli katika hafla ya
kuwaapisha Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Ikulu Dar es Salaam juzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi
Mkuu wa TAKUKURU, Valentino Mlowola alimtaja mfanyabiashara huyo kuwa ni
Mohammed Mustafa Yusuf Ali anayetuhumiwa kuiibia Serikali matrilioni ya
shilingi kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs) ambazo
hazijasajiliwa na TRA na kutoa risiti bandia.
Alisema TRA kwa kushirikiana na TAKUKURU inaendelea na uchunguzi ili
kubaini makampuni yote yanayojihusisha na udanganyifu huu, ambapo hadi
sasa jumla ya makampuni manne yamebainika kujihusisha na ukwepaji kodi
kwa mtindo huu kuanzia mwaka 2010 hadi 2014; na jumla ya Sh
29,216,900,301.7 imebainika kutokulipwa serikalini na makampuni hayo kwa
kipindi hicho.
Alisema kwa sasa wanaendelea na mahojiano naye zaidi ili kuwabaini
wote wanaohusika na mfumo huo na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa TRA, Alfayo Kidata aliyeambatana na
Mlowola katika mkutano huo wa waandishi wa habari, makampuni hayo
yamekuwa yakinunua risiti za manunuzi bandia kutoka kwa watu wanaomiliki
mashine za EFDs ambazo hazijasajiliwa.
“Makampuni hayo wakishanunua risiti za manunuzi bandia, hatimaye
huzitumia risiti hizo kudai marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) bila kuwepo na bidhaa au huduma halisi iliyouzwa au kutolewa na
mhusika, kitendo ambacho kinainyima serikali mapato stahiki kwa mujibu
wa sheria,” alisema.
Aliyataja makampuni hayo kuwa ni pamoja na Skol Building Material Ltd
ambayo tangu mwaka 2012 hadi 2013 haikulipa jumla ya VAT ya Sh
5,464,915,963 na Kodi ya Mapato yenye thamani ya Sh 10,960,787,861
ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh 16,425,703,824 kwa kipindi hicho.
Kampuni nyingine ni Farm Plant (T) Limited ambayo tangu mwaka 2010
hadi 2014 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 5,930,170,573 na kodi ya mapato
yenye thamani ya Sh 4,948,393,516 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa ni Sh
10,878,564,089.
Pia imo kampuni ya A.M.Steel & Iron Mills Limited ambayo kuanzia
mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa jumla ya VAT ya Sh 79,016,112 na kodi ya
mapato yenye thamani ya Sh 131,693,518 ambayo jumla ya kodi inayodaiwa
ni Sh 210,709,630.
Kampuni nyingine ni A.M Trailer Manufacturers Limited ambayo tangu
mwaka 2013 hadi 2014 haikulipa VAT ya Sh 638,221,034.80 na kodi ya
mapato yenye thamani ya Sh 1,063,701,724. 00 ambayo jumla ya kodi
inayodaiwa ni Sh 1,701,922,758.00.
Alisema baada ya kubaini ukwepaji kodi huo kwa kushirikiana na
TAKUKURU inaendelea na uchunguzi wa tuhuma hizo na mara baada ya
uchunguzi kukamilika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya
watakaobainika kukwepa kodi.
Alitoa mwito kwa wafanyabiashara wote kutojihusisha na kununua risiti
za bandia na kudai marejesho ya VAT yasiyostahili kwa kuwa mamlaka
imejizatiti kuendelea kuwabaini wafanyabiashara wanaokwepa kodi na
kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua stahiki.
Aidha alisema uchunguzi wa awali pia umebaini kuwepo makampuni hewa
228 na kusisitiza kwamba wameusimamisha mfumo huo bandia na kutoa siku
tatu kwa kampuni zote zinazodaiwa kulipa fedha hizo.
“Hakuna yeyote anayekwepa kodi atasalimika, wote ni lazima walipe na sasa tumedhibiti mfumo huo bandia,” alisema.
Juzi Magufuli akizungumza na Ma RC na Ma DC wapya, aliwataka
wakasimamie vyema mapato katika maeneo yao kwani kumekuwepo na baadhi ya
watu wajanja wanaotumia vibaya taasisi za Serikali ikiwemo Wakala wa
Usajili wa Kampuni (Brela) TRA kujinufaisha wenyewe na kuliingizia taifa
hasara.
Alisema: “Tulikuwa tunafuatilia mashine za EFDs zinazokusanya mapato,
yupo mtu mmoja alitengeneza kampuni nyingi zilizokuwa zikimlipa
asilimia tano ya VAT na yeye anacheza na TRA halipi asilimia 18 ya kodi
hiyo. Alikuwa anaingiza kati ya shilingi milioni saba mpaka nane kwa
dakika. Serikali ilipoteza matrilioni ya fedha. Huyu mtu yupo kwenye
mikono salama kwa sasa”.
CHANZO; HABARI LEO
Takukuru na TRA wataja mwizi EFDs
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:35:00
Rating:
No comments: