Serikali Yarejesha Misamaha Ya Kodi Kwa Taasisi Za Dini, Yatoa Masharti Mazito


Serikali imelegeza msimamo wake kuhusu kuondoa misamaha ya kodi kwenye Taasisi za dini badala yake itaongeza udhibiti ili kuzuia mianya ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ametoa ufafanuzi huo mjini Dodoma wakati akiongea na vyombo vya habari ili kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge wakati wa kujadili bajeti Kuu ya Serikali iliyopitishwa Juzi na Bunge.

Amesema kuwa uamuzi huo wa serikali umefuatia maombi na mapendekezo mbalimbali ya wadau yaliyoitaka serikali iendelee kutoa misamaha ya kodi kwa Taasisi hizo kutokana na umuhimu wake wa kuisaidia jamii kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hizo.

“Kwa kutambua mchango mkubwa wa taasisi mbalimbali za kidini katika utoaji wa huduma za elimu, afya, maji; nimeamua kufuta utaratibu nilioutangaza katika hotuba ya bajeti, badala yake serikali itaimarisha zaidi udhibiti wa misamaha hiyo”Alisema Dkt. Mpango

Alizitaja baadhi ya hatua zitakazochukuliwa kuzuia mianya ya matumizi mabaya ya misamaha hiyo kuwa ni kuzitaka Taasisi za dini kuwasilisha orodha ya vifaa vinavyotarajiwa kununuliwa kutoka nje ya nchi kila mwanzo wa mwaka wa kalenda, pamoja na kuthibitisha kama vifaa vilivyosamehewa kodi mwaka uliotangulia vilitumika kwa mujibu wa sheria

Aidha, utaratibu mpya utazitaka Taasisi hizo za dini kuwasilisha majina ya watu waliowaidhinisha kuandika barua za maombi ya msamaha wa kodi zikiainisha cheo, saini, picha, anuani na namba za simu za wahusika.

“Taarifa hizo ni muhimu katika kuiwezesha TRA kufuatilia bidhaa zilizoombewa na kupewa misamaha kama zimepata kibali cha Taasisi husika zimetumika na zimetekeleza miradi iliyokusudiwa” Aliongeza Dkt. Mpango

Dkt. Mpango alisema katika utaratibu huo mpya, wameweka masharti ya kuzilazimisha Taasisi hizo za dini kuiandikia serikali barua ya kumuidhinisha wakala wa forodha waliyemteua kutoa bandarini mizigo itakayokuwa ikiagizwa kutoka nje

Alizitaja hatua nyingine kuwa ni wakati wa kuomba msamaha wa kodi katika bidhaa zinazoingizwa nchini, Taasisi za dini zitalazimika kupata barua ya uthibitisho kutoka kwa Afisa Mtendaji wa serikali ya Mtaa ama kijiji na mkuu wa wilaya mahali Taasisi au Mradi ulipo ili kuthibitisha uwepo wa Taasisi au mradi na mahitaji ya vifaa vinavyoombewa msamaha

Dkt. Mpango alifafanua kuwa magari yatakayoingizwa kwa msamaha wa kodi yatalazimika kuwa na rangi pamoja na namba maalumu za utambuzi mfano TEV 222 AXZ kama njia ya kudhibiti matumizi yake.

Alionya kuwa Taasisi ya dini itakayothibitika kutumia vibaya msamaha wa kodi itafutiwa usajili wake.
Serikali Yarejesha Misamaha Ya Kodi Kwa Taasisi Za Dini, Yatoa Masharti Mazito Serikali Yarejesha Misamaha Ya Kodi Kwa Taasisi Za Dini, Yatoa Masharti Mazito Reviewed by WANGOFIRA on 20:45:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.