Serikali kutekeleza miradi mikubwa 4 ya kielelezo
MPANGO wa Maendeleo wa Mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano
chini ya Rais John Magufuli, umekuja na miradi mikubwa minne ya
kielelezo, itakayotekelezwa kwa kutumia sehemu kubwa ya Sh trilioni 11.8
zilizotengwa kwa maendeleo, ambazo ni sawa na asilimia 40 ya Bajeti
yote ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Reli ya kisasa ya kiwango cha geji.
Kwa kuonesha dhamira ya serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo,
asilimia 74 ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya maendeleo itakuwa
makusanyo ya ndani ya serikali na asilimia 26 tu ndio mapato ya nje.
Akisoma Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2015 na Mpango wa Maendeleo
wa Taifa kwa mwaka 2016/2017 bungeni jana, Waziri wa Fedha na Mipango,
Dk Philip Mpango (pichani) alitaja miradi hiyo ambayo baadhi Rais
Magufuli alishaizungumzia katika baadhi ya hotuba zake.
“Kwa maana ya kipekee, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2016/17,
umeainisha miradi mikubwa ya kielelezo, ambayo itapewa msisitizo katika
utekelezaji wake,” alisema Dk Mpango. Mradi wa kwanza wa maendeleo
katika kundi hilo la miradi minne mikubwa ya kielelezo ni ujenzi wa reli
ya kisasa (standard gauge) ambao Rais Magufuli aliahidi kutenga Sh
trilioni moja ya kuanza ujenzi wakati wakitafuta fedha za kuendeleza
ujenzi wake.
Reli hiyo itaanzia Dar es Salaam kwenda Kigoma na Tabora mpaka Mwanza na
itakuwa na matawi ya kutoka Isaka hadi Kigali/Keza na Msongati hadi
Kaliua- Mpanda. Aprili mwaka huu, wakati Balozi wa China nchini, Dk Lu
Youqing alipokwenda Ikulu, Rais Magufuli alimweleza kuwa Tanzania
imedhamiria kuanza ujenzi wa reli hiyo haraka iwezekanavyo na tayari
imetenga fedha hizo katika bajeti yake hii ya kwanza kwa ajili ya kuanza
awamu ya kwanza ya ujenzi huo.
“Tuna imani kuwa mradi huu utasaidia kuleta mapinduzi makubwa ya uchumi
katika nchi yetu na katika nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kati
zikiwemo Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ndio maana
hatutaki kupoteza muda kwa mazungumzo marefu, tunataka kazi ianze na
watu waanze kunufaika,” alikaririwa Rais Magufuli katika mazungumzo
hayo. Naye Dk Youqing alielezea utayari wa China kushirikiana na
Tanzania katika mradi huo ambao zabuni za ujenzi zinatarajiwa kutangazwa
hivi karibuni.
Rais Magufuli pia alipozindua ujenzi wa barabara ya juu ya Tazara,
alirejea kauli hiyo, lakini akasisitiza kuwa reli hiyo ikifika Ruvu,
mizigo yote ya Bandari ya Dar es Salaam itasafirishwa kwa reli mpaka
eneo hilo na malori yataanzia Ruvu badala ya kuongeza foleni na kuharibu
barabara za Dar es Salaam.
Manufaa mengine reli hiyo itakapokamilika, itapunguza gharama za
usafirishaji wa mizigo kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam kwa
asilimia 30, na kuifanya bandari hiyo kuwa na unafuu mwingine kwa wateja
kimataifa, mbali na unafuu unaotokana na eneo la kimkakati.
Mradi wa pili wa kielelezo katika bajeti ya maendeleo ya kwanza ya
Serikali ya Awamu ya Tano kwa mujibu wa Dk Mpango ni ununuzi wa ndege
tatu mpya za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Dk Mpango alitaja aina ya ndege hizo kuwa ni Bombardier Q400 mbili,
zenye uwezo wa kubeba abiria 67 mpaka 88 kila moja na nyingine aina ya
Bombardier CS 300 yenye uwezo wa kubeba abiria 100 mpaka 150.
Dk Mpango alitaja mradi wa tatu wa kipaumbele kuwa ni ununuzi wa meli
moja mpya ya usafirishaji wa mizigo na abiria katika Ziwa Victoria,
ununuzi utakaofanyika sambamba na ukarabati wa meli tatu za Mv Victoria,
Mv Butiama na Mv Liemba ili kuimarisha usafirishaji.
Nia hiyo ya serikali ambayo sasa imewekwa katika utekelezaji wa miradi
ya kielelezo iliyotengewa fedha iliwahi kuzungumziwa na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, Machi mwaka huu aliposema serikali imeanza kukusanya
fedha kwa ajili ya kununua meli mpya.
Alisema ahadi ya ununuzi wa meli hiyo iliyotolewa na Rais Magufuli
katika kampeni za 2015 iko palepale kwa ajili ya usafirishaji wa abiria
na mizigo kwenye Ziwa Victoria. Mradi wa nne wa msisitizo katika mpango
wa maendeleo wa mwaka huu ambao utekelezaji wake utaanza ni mradi wa
makaa ya mawe Mchuchuma na mradi wa chuma Liganga katika wilaya ya
Ludewa mkoani Njombe.
Eneo la Mchuchuma linakadiriwa kuwa na hazina ya tani milioni 540 za
makaa ya mawe ambayo ni malighafi muhimu ya uzalishaji umeme nafuu
kuliko wa mafuta unaohitajika kwa wingi kwa ajili ya kujenga uchumi wa
viwanda.
Aidha, eneo la Liganga linakadiriwa kuwa na hazina ya chuma cha pua tani
milioni 45 ambayo ndiyo malighafi mama ya viwanda vikubwa na vya kati
duniani. Mbali na hazina hiyo, maeneo hayo pia yapo kimkakati zaidi kwa
kuwa yako karibu na hivyo kufanya uyeyushaji wa chuma hicho cha pua kuwa
nafuu kuliko mahali pengine duniani, kutokana na ukaribu wa hazina ya
makaa ya mawe na chuma hicho.
Serikali kutekeleza miradi mikubwa 4 ya kielelezo
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:37:00
Rating:
No comments: