RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi ( A Wizard Student ) - Sehemu ya Pili

Mtunzi: Enea Faidy

Ilipoishia sehemu ya kwanza ( kama hukuisoma bofya hapa)
.....Wakati wanafunzi wengine wakiwalilia wenzao Doreen alikuwa amejitenga peke yake nyuma ya bweni alilokuwa anakaa na kulikuwa na Giza totoro. Alikuwa uchi wa mnyama huku mikono yake ikiwa imeshikilia vitu fulani huku akitamka maneno ambayo aliyaelewa mwenyewe....  


Sehemu ya pili
...DOREEN aliendelea kuongea maneno aliyoyajua mwenyewe akiwa bado yupo uchi wa mnyama nyuma ya bweni alilokuwa anaishi. 
Ghafla kipande kidogo cha karatasi nyeupe kikashuka mikononi mwake bila kuonekana kilikotokea. Doreen alicheka kwa sauti Kali ya kutisha sana kisha akalikazia macho karatasi lile, matone ya damu yaliangukia kwenye karatasi lile kutoka kwenye macho yaliyotisha sana ya Doreen kwani yalikuwa na rangi nyeusi halafu yakawa na umbile kama macho ya paka.
 
"Nenda mpaka ofisi ya mkuu wa shule ukamalize kazi." alisema Doreen akiwa amelinyanyua karatasi like kwa mkono wake wa kushoto. Karatasi likatoweka mkononi mwake na kupepea kwa nguvu kama vile limerushwa na upepo mkali.

Doreen alipomaliza kazi hiyo akasimama vizuri kama mwanajeshi aliyejipanga kwaajili ya gwaride kisha akainamisha kichwa chake chini akapotea eneo lile.

**********
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mabango walikuwa wanahofu kubwa sana kila wakikaa walifikiria kifo tu. Usingizi haukuwajia hata Mara moja hivyo usiku waliketi makundi makundi wakizungumza hili na lile.

Wakati huo Dorice rafiki kipenzi wa Doreen alikuwa amejitenga pembeni akizungumza na mpenzi wake aitwaye Eddy, kijana mtanashati, mzuri, mpole na akili nyingi sana darasani.Wasichana wengi shuleni pale walitamani kuwa nae lakini bahati ilimwangukia Dorice pekee.
 
"Eddy unajua naogopa sana.." ilikuwa sauti ya Dorice akiwa amemkumbatia Eddy kwani kigiza kile cha usiku kiliwaficha wasionekane hivyo wakajiachia.
"unaogopa nini Dorice mpenzi wangu?"
"Naogopa kufa!" binti Huyo wa kinyaturu, mrembo aliyeumbika aliongea kwa sauti ya madeko sana.
"siku zote nakwambia Dorice kama Mungu alipanga huwezi kupangua , mwanadamu asikutishe kwa lolote. Huyu anayeua wenzake naye IPO Siku yake tu!"
"Najua baby Ila hali inatisha"
"Tuzidi kuomba Mungu mpenzi wangu kila unalofanya muombe Mungu."
"Nakupenda "
"Nakupenda pia"

Wakati Eddy na Dorice wakiendelea kuzungumza maneno hayo, Doreen alikuwa nyuma ya mti waliosimama hivyo alisikia kila kitu. 
Roho ilimuuma sana kwani tangu alipohamia shuleni hapo alitokea kumpenda sana Eddy na alitamani awe mpenzi wake kwani ndio chaguo la moyo wake lakini Dorice alikuwa kikwazo. .
Suala hilo lilimuumiza Doreen ndani kwa ndani. Akainuka pale kwenye mti na kupita katikati yao, akamwita Dorice pembeni.
"Dorice.. mimi nawahi kulala Ila kesho unione!"
"nikuone?"
"ndio kwani hujaelewa?" alijibu Doreen kwa ukali jambo lililomwachia maswali mengi Dorice. Lakini Doreen hakujali kitu akaondoka zake Ila moyoni alipanga jambo zito la kumfanyia Dorice siku ya kesho yake.

*********
Ilikuwa asubuhi tulivu sana majira ya saa kumi na mbili na nusu asubuhi ambapo mwalimu Dayana Mbeshi aliwahi ofisini kwake kama ilivyokuwa kawaida yake. 
Majengo ya ofisi yalimkaribisha kwa shangwe naye akaitikia ukaribisho huo kwa kufungua ofisi yake kisha akasogeza mapazia ya dirishani ili kuruhusu mwangaza wa jua changa uweze kupenyeza vizuri. 
Baada ya kukamilisha yote hayo Madam Mbeshi akasogeza kiti chake karibu na meza kisha akaketi halafu akaanza kusogeza vitu vilivyokuwepo mezani pale lakini ghafla akakutana na karatasi chafuchafu mezani kwake lakini ilikuwa na maandishi. 
Akashtuka kidogo halafu akaichukua ili aisome vizuri. Mwalimu Mbeshi hakutaka kuamini kile alichokiona, akataharuki kwa hofu na mshangao...............

Itaendelea....
RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi ( A Wizard Student ) - Sehemu ya Pili RIWAYA: Mwanafunzi Mchawi ( A Wizard Student ) - Sehemu ya Pili Reviewed by WANGOFIRA on 20:26:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.