MAAMUZI YA KESI YA DAUDI MWANGOSI KUTOLEWA LEO MAHAKAMANI

Mahakama kuu kanda ya Iringa imeendelea kusikiliza kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel ten Daud Mwangosi ambapo mahakama imeendelea kusikiza hoja za mawakili kutoka upande wa Jamhuri na upande wa utetezi katika kesi hiyo ya mauaji inayomkabili aliyekuwa askari wa jeshi la polisi kikosi cha kutuliza ghasia FFU mjini Iringa Pasificus Cleophace Simon. 

Hatua hiyo ni baada ya mahakama kusikiliza ushahidi wa tukio hilo ambapo jumla ya mashahidi wanne wametoa ushahidi wao akiwemo aliyekuwa kamanda wa kikosi cha FFU mjini Iringa Said Mnunka, mkuu wa kituo cha polisi mjini Mafinga Ancelin Mwampamba Lewis Teikya wote kutoka jeshi la polisi na Flora Mhelela anayetambulishwa kama mlinzi wa amani. 


Wakili wa upande wa utetezi Rwezaula Kaijage ameiambia mahakama kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi walioletwa na Jamhuri hauoneshi moja kwa moja kuwa mshitakiwa ndiye aliyetenda kosa hilo na badala yake mashahidi hao wanadhania kuwa mshitakiwa huyo ndiye aliyetenda kosa.

Wakili huyo wa utetezi ameendelea kufafanua kuwa hata ushahidi ulitolewa na mashahidi watatu kati ya wanne umeegemea kwenye picha iliyochapishwa na gazeti la Mwananchi toleo la septemba tatu 2012 ambayo hata mpiga picha wa picha hiyo hakuhojiwa mahakamani hapo.

Ameongeza kuwa ushahidi uliotolewa na mlinzi wa amani ukimnukuu mshitakiwa kukiri kutenda kosa hilo huko kijijini Nyololo siku ya Septemba 2 ,2012 hauthibitishi mahakama kuwa mshitakiwa ndiye aliyetenda kosa hilo kwakuwa kabla ya kuhojiwa na mlinzi huyo wa amani mshitakiwa aliitwa na kamanda wa polisi mkoa wa Iringa wa wakati huo na kwamba inawezekena alipewa maelekezo kukiri kosa hilo hivyo upande wa utetezi unaona ushahidi huo haumtii hatiani mshitakiwa na unaiomba mahakama kumwachia huru kwakuwa hana kesi ya kujibu. 


Hoja hiyo ilipingwa na mawakili wa upande wa Jamhuri Sunday Hyera na Ladislaus Komanya wakisema kuwa ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri ikiwemo picha iliyochapishwa na gazeti la mwananchi toleo la septemba tatu 2012 unamuonesha mtuhumiwa akiwa amemuelekezea bunduki aina ya long range inayotumika kulipua mabomu ya machozi pamoja na mabomu ya kishindo huku akijua bunduki hiyo hutumika kupiga kwenye digrii 40 hadi 45 jambo linaloonesha mshitakiwa huyo alikusudia kumuua marehemu Mwangosi. 


Jaji anayesikiliza kesi hiyo Mheshimiwa Dokta Paul Kihwelo ameahirisha kesi hiyo hadi kesho ambapo mahakama itatolea maamuzi kama mshitakiwa anayo kesi ya kujibu au kumwachia huru baada ya kuridhika kuwa hana kesi ya kujibu.
Chanzo-ITV
MAAMUZI YA KESI YA DAUDI MWANGOSI KUTOLEWA LEO MAHAKAMANI MAAMUZI YA KESI YA DAUDI MWANGOSI KUTOLEWA LEO MAHAKAMANI Reviewed by WANGOFIRA on 20:09:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.