Bunge lapitisha muswada wa Sheria ya Fedha kwa mwaka 2016
Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo limepitisha muswada wa sheria ya
Fedha ya mwaka 2016 ili kuwezesha utekelezaji wa bajeti ya Serikali
kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Muswada huo umepitishwa na Bunge pamoja na marekebisho yake ambayo yametolewa na kamati ya kudumu ya bunge ya bajeti na wabunge.
Marekebisho
yaliyofanyika katika muswada huo ni pamoja na kutoongeza ushuru wa
kuingiza sukari ya viwandani kutoka asilimia 10 kwenda 15 ambapo kamati
ya kudumu ya bunge ya bajeti ilishauri Serikali isiendelee na pendekezo
hilo kutokana na hatua hiyo kuwa na athari kwa viwanda vinavyotumia
sukari viwandani kama malighafi ya kuzalisha bidhaa nyingine kama juisi
na soda.
“Serikali
imekubali pendekezo lililotolewa na kamati ya kudumu ya Bunge ya bajeti
ya kutoongeza ushuru wa kuingiza sukari ya viwandani kutoka asilimia 10
kwenda asimilia 15, hivyo kuendelea kutoza asilimia 10 iliyokuwepo kwa
mwaka huu wa fedha,” alifafanua Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Philip Mpango.
Marekebisho
mengine yaliyofanyika ni pamoja na kuondoa adhabu ya kifungo cha miezi
Sita kwa wale ambao hawatodai risiti baada ya kununua bidhaa au huduma
na kubaki na adhabu ya kulipa faini kulingana na thamani ya bidhaa.
Aidha
Mhe. Mpango amesema kuwa muswada huo umezingatia kwa kiwango kikubwa
mapendekezo ya wadau mbalimbali wakiwemo wabunge, wamiliki wa viwanda,
wafanyabiashara na taasisi za Serikali.
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Ndani ya Bunge..
Bunge lapitisha muswada wa Sheria ya Fedha kwa mwaka 2016
Reviewed by WANGOFIRA
on
20:18:00
Rating:
No comments: