PROF. NDALICHAKO, HESLB BADO KUNA MAJIPU YA MENGI.



NA, 
BARAKA NGOFIRA

Unaweza kushangaa na kuhuzunishwa na vijana wa kitanzania hasa wale watoto wa maskini waliokosa mikopo huku wakiwa na sifa za kupewa mikopo hiyo. Pia waweza kuona kuwa wanaonewa pale watoto wa wenye navyo kupewa vipaumbele nap engine kupewa aslimia mia moja za mkopo.

Sishangai maana hii ni hali ya kawaida hasa kwa mataifa mengi ya kiafrika ambapo Rushwa na kujuana kumetawala miongoni mwa viongozi na ulafi wa madaraka, na undugu kutalawa na kuweka nyuma ubinadamu wa watu wengine.

Pia hata sishangai kuona watoto wa yule mkulima,  mfugaji na mwalimu wa shule ya msingi aliyedharauliwa, kutojaliwa katika haki zake za msingi ikiwemo elimu na Afya.

Pia sioni shida yoyote watoto wa wenye navyo waliozoea kula mkate wa blue band na chai ya  maziwa kila kuchapo,  huku mlangoni gari la shule likipiga honi kuwaita kwenda shule kupewa mkopo tena kwa asilimia mia moja. Lakini mtoto wa maskini anayeshindia viazi na mihogo ya kuchoma kila siku kukosa mkopo kwa sababu ya fani anayosoma eti haina kipaumbele.

Haya ni maisha ya kawaida, kwetu watoto wa masikini ambao hatujui kesho yetu itakuwaje. Lakini nikiwa mdogo nakumbuka wazazi wangu walinifunza kuridhika na maisha ya kwetu, bila shaka naamini wenzangu na mimi hawa nao walifundishwa vivyo hivyo. 

Ndio maana hata hawashangai kunyanyaswa na wakubwa wachache waliokalia ofisi zilizojawa na viyoyozi na viti vya magurudumu wakizunguka bila shida. Ni kawaida lakini maana hata kwenye vitabu vitakatifu wameandika mwenye nacho uongezewa na asiyenacho unyang’anywa hata kile alichonacho.

Naandika makala hii kwa niaba ya wanafunzi wenzangu tuliodahiliwa mwaka wa masomo 2014/2015 katika vyuo mbalimbali hapa nchini, lakini hatukupewa mikopo na bodi ya mikopo kwa kile tulichoambiwa kuwa “Badget exhausted” yaani bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15 haitoshi kuwapa wanafunzi wote wenye vigezo vya kupata mkopo.

Na kuahidiwa kuwa serikali itakapopata fedha tutazingatiwa kwanza, lakini makubaliano hayakuwa kama tulivyokubaliana maana fedha zilivyokuja tuliwaona watoto wa matajiri wakiongezewa mikopo na baadhi yao waliokuwa hawajapewa nao ikawa nafasi yao ya kunufaika.

Hatukukata tamaa kwenda ofisi ya bodi ya mikopo kuuliza tatizo liko wapi maana fedha zimekuja na tulioambiwa tutanufaika kuwekwa pembeni. Majibu tuliyopewa yalitufedhehesha na kulaumu kuzaliwa kwenye familia maskini. Lakini kwa sababu hatukupenda kuzaliwa huko tulijikaza tu maana hakuna namna nyingine zaidi ya kuvumilia kuendelea kuishi kwa mkate na maji kila siku.

Lakini baada ya kuona tumefedheheshwa na majibu yao walituambia tujaribu kuomba tena kwa mwaka wa fedha 2015/16, huenda tukapewa, lakini mambo yakawa ni yaleyale. 

Tulijipa moyo na kuendelea maisha ya chuo kwa wazazi wetu kukopa fedha nyingi kwenye vikoba, na kwenye mabenki halikuisha. Ambapo mpaka sasa wanadaiwa fedha nyingi na naamini muda si mrefu dhamana zao walizoweka zikiwemo hati za nyumba mashamba, viwanja na dhamana nyingine karibu zipigwe mnada kwa ajili ya kushindwa kulipa madeni makubwa wanayodaiwa mpaka sasa kwa ajili ya kutupigania watoto wao tusome.

 Lakini kwa sasa maji yametufika shingoni tena maji ya barafu damu zishatuganda, na wengine wameshaacha masomo kwa kukosa ada na fedha za kujikimu, kwa upande wa dada zetu baadhi yao kwa sababu ya upeo mdogo wa kufikiri wameshageuza bidhaa za kuuza miili yao vichochoroni ili tu waweze kuyamudu maisha ya chuo.

Ukiachilia mbali hayo, mwanzoni mwa mwezi wa pili mwaka huu watendaji wanne wa bodi ya mikopo walisimamishwa kazi kwa matumizi mabaya ya madaraka.  ambapo jambo liliotuhumiza zaidi ni pale tuliposikia zaidi ya wanafunzi 54,000 walipewa mikopo bila kuomba. Na wengine zaidi ya 5000 kupewa mikopo huku majina yao yakiwa kwenye zaidi ya chuo kimoja.

Japo hatua hiyo ilipongezwa na wanafunzi wengi ambao walikuwa hawajapata mikopo kwa matumaini ya kwamba huenda tulioahidiwa kunufaika na mikopo kwa kudanganywa kuandika majina lakini bado mambo ni yaleyale.

Rai yangu kwako Mama yetu mpendwa nahisi na wewe ulizaliwa familia kama za kwetu za wazazi oye aye japo kwa kipindi hicho ninyi mlifaidi maana mlipata fursa ya kusomeshwa bure na serkali yetu tukufu, na kupewa kila kitu . 

Najua unafahamu fika maisha ya chuo jinsi yalivyo urahisi wake na ugumu wake unaufahamu fika, maana wewe huu msomi na ni imani yangu kuwa Rais wetu mtukufu hakukosea kukuweka kwenye wizara hiyo ambayo viatu vyake umevivaa vilivyo na havijakupwaya na wala havitakupwaya kamwe.

Tusaidie  tupate nasi mikopo, maana wengi wetu wamesitisha masomo kwa kukosa mikopo  ya elimu ya juu.

Makala hii imeandaliwa na Baraka Ngofira, mwanafunzi wa mwaka wa pili chuo nkikuu cha Dar es salaam anasomea shahada ya kwanza ya mawasiliano nkwa Umma anapatokana kwa mawasiliano ya 0763580901, au barua pepe ya barakangofira@gmail.com.
PROF. NDALICHAKO, HESLB BADO KUNA MAJIPU YA MENGI. PROF. NDALICHAKO, HESLB BADO KUNA MAJIPU YA MENGI. Reviewed by WANGOFIRA on 06:23:00 Rating: 5
Powered by Blogger.