KIWANDA CHA BIA YA SERENGETI CHAPIGWA FAINI KWA UCHAFUZI WA MAZINGIRA.

                                       

Kiwanda cha bia aina ya serengeti kilichopo chang'ombe wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam kimepigwa faini ya shillingi za kitanzania millioni kumi na sita(16) na Baraza la usimamizi wa mazingira Nchini (NEMC) baada ya kutokutimiza masharti ya sheria ya mazingira ya mwaka (2004) na kanuni zake. 
         
Uamuzi huo umefikiwa baada ya  Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa raisi Muungano na mazingira Mh.Luhaga Mpina kupata malalamiko kutoka kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya kiwanda hicho. Na kuainisha uchafuzi wa mazingira yanayowazunguka wananchi hao yanayohatarisha  usalama wa afya zao.

Na kumlazimu naibu waziri huyo kufanya ziara ya kushtukiza  kiwandani hapo, akiwa ameambatana na Wakurugenzi kutoka Baraza la usimamizi wa mazingira nchini (NEMC) na kujionea uharibifu huo.                   
Mh.Mpina  ameagiza kiwanda hicho kulipa faini hiyo na kurekebisha miundo mbinu hiyo ndani ya siku arobaini na tano kusiwepo tena na utiririshaji maji machafu na yenye kemikali kali za sumu ambayo yanatoa harufu mbaya inayohatarisha afya  za wakazi wa chang'ombe wilaya ya temeke. 
              
Pia mkurugenzi wa mazingira Bw. Boniventure Baya ametoa siku saba kwa kiwanda hicho kiwe kimelipa faini hiyo vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwani wamekua wakikaidi maagizo yanayotolewa na Baraza hilo la mazingira nchini (NEMC). Na kuwataka kufanya hivyo haraka iwezekanavyo baada ya kukiuka sheria ya utunzaji mazingira ya mwaka(2004) na kutokutimiza masharti waliyopewa takribani miaka miwili iliyopita.
           
Naye mbunge wa Temeke (CUF) Mh.Abdallah Mtolea alisema kiwanda hicho kimekua na mahusiano mabaya na wananchi wanaozunguka  maeneo jirani na kiwanda hicho hivyo kupelekea kuwa na mgogoro wa muda mrefu na uongozi  kiwanda hicho.  Na  kumuomba Naibu waziri kutatua tatizo hilo ambalo limekua likifanywa kwa makusudi na uongozi wa kiwanda hicho ilihali wanajua madhara ya wanayoyapata wananchi. 
                                                         
Aidha kwa upande wake Afisa mazingira wa kiwanda hicho Bw.Simon Peter alipinga vikali tuhuma hizo ambazo zimeelekezwa katika kiwanda hicho na kusema uongozi wa kiwanda hicho unafanya kila jitihada ili kuweza kutatua kero hiyo na si kweli kwamba hawashughulikii tatizo hilo la mazingira jirani na wakazi hao.
               
Kwa upande wa wananchi kupitia kwa Bi.Emanuela Peter, walisema hiyo ni kero kubwa sana kwao.  Ambapo imekuwa ikiwalazimu kuyahama makazi yao hasa wakati wa kipindi cha masika, ambapo maji ya mvua na yale ya kiwanda huchanganyikana na kujaza uchafu wote majumbani mwao hali inayowalazimu kuhamia kwenye nyumba za kulala wageni kwa muda, hivyo wameiomba serikali kuangalia kwa makini na kuweza kulipatia ufumbuzi. 
                   

Vilevile,  Mh.Luhaga alifanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda cha Cement Wazo kilichopo Tegeta wilaya ya kinondoni jijini Dar es salaam, ambapo hakufanikiwa kuonana na uongozi wa kiwanda hicho kwa madai ya kuwa nje ya jiji la Dar es salaam. Ambapo alitoa tamko la serikali kuwa, serikali ya awamu ya tano haina uadui na wafanyabiashara pamoja na wawekezaji kama inavyozaniwa na watu wengine, bali inachowataka ni kufuatwa kwa Sheria, taratibu na kanuni kama inavyostahili.
KIWANDA CHA BIA YA SERENGETI CHAPIGWA FAINI KWA UCHAFUZI WA MAZINGIRA.  KIWANDA CHA BIA YA SERENGETI CHAPIGWA FAINI KWA UCHAFUZI WA MAZINGIRA. Reviewed by WANGOFIRA on 08:57:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.