RELI YA KATI KUANZA KUFANYA KAZI MEI MOSI

Treni ya kwanza ya abiria ya Deluxe  kutoka Dar es Salaam kwenda bara itaondoka saa 2 asubuhi siku Jumapili Mei Mosi, 2016 kuelekea Kigoma.

Kuanza kwa safari hiyo kunatokana na kutengemaa kwa eneo korofi baina ya  stesheni za  Kilosa mkoani  Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma. 

Kwa mujibu wa taarifa ya Wakuu wa Idara za uendeshaji wa kampuni ya Reli Tanzania (TRL) iliyotolewa  Aprili  26, 2016 baada ya ukaguzi wa kina wa  eneo la Gulwe, imesema  sasa eneo hilo  linapitika  na kwamba tuta limeiamarika na kuwezesha treni zote za abiria na mizigo kupita kwa usalama kabisa.

Mara ya mwisho huduma za treni za abiria ya kawaida zilihamishiwa Dodoma mnamo Aprili 07, 2016.

Ratiba za safari treni ya kawaida kutoka Dar es salaam kuelekea Mwanza na Kigoma  ni kila siku ya Jumanne na Ijumaa saa 11 jioni ambayo imepangwa kuanza Jumanne Mei 3, 2016.Wakati treni ya  Deluxe inaondoka Dar es salaam kila Jumapili saa 2.00 asubuhi.

Na kutoka Mwanza na Kigoma treni ya kawaida inatoka huko kila siku ya Alhamisi na Jumapili saa 11.00 jioni kwa Kigoma na saa 12 jioni kwa Mwanza. Treni ya DELUXE  nayo inatoka  Kigoma au Mwanza kila siku ya Jumanne saa 2.00 asubuhi.

Wasafiri wote wanaombwa kufanya mipango  ya safari (booking) katika stesheni zetu husika na sio vinginevyo.

Aidha taarifa za uhakika kuhusiana na taratibu  za safari zetu za treni za abiria  na  mizigo  zinapatikana  katika vituo vyetu vyote vya TRL.

Uongozi wa kampuni  ya TRL  unawaomba radhi  wateja wake na wananchi kwa ujumla kwa usumbufu wowote uliojitokeza katika kipindi chote  hicho ambacho huduma zetu zilipokuwa zinaanzia na kuishia Dodoma badala ya Dar es salaam kama ilivyo kawaida.

Aidha Kampuni inashukuru jitihada za  Serikali pamoja na taasisi zake kadhaa   kufanikisha kurejesha hali ya miundombinu  ya reli  katika hali yake ya kawaida.

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano:
Kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL
Ndugu Masanja Kungu Kadogosa
Aprili 28, 2016
DAR ES SALAAM
RELI YA KATI KUANZA KUFANYA KAZI MEI MOSI RELI YA KATI KUANZA KUFANYA KAZI MEI MOSI Reviewed by WANGOFIRA on 20:55:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.