NI KWELI DR.RIOBA ATAIBADILI TBC AU ATABADILISHWA NA TBC?






Unapozungumzia  kuhusu tasnia ya habari, kamwe hauwezi kuacha kutaja mchango wa Dr. Ayoub Rioba ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utangazaji la Tanzania yaani TBC.

Uteuzi huu umepongezwa na kupokelewa kwa mikono miwili na wadau mbalimbali wa habari. Na wale wengine ambao wanauzoefu mkubwa wa kiuchambauzi ambao wanaiona TBC imepewa mtu sahihi anayeweza kuifikisha mahali ambapo Shirika la Utangazaji na la Umma linapaswa kuwa.


Binafsi nitoe pongezi zangu za dhati kwa uteuzi huo ambao pasipo shaka yoyote kuwa Dr. Rioba atatekeleza vyema majukumu yake pasipo kuwa na woga wowote. Kwani kauli alizokuwa akizitoa kuhusiana na mienendo ya vyombo vya habari, sekta nzima ya habari na jinsi vinavyoendeshwa. Ambapo wamiliki wa vyombo hivyo utumia nguvu ya sema na propaganda kupindisha ukweli na kuwafanya waandishi wa habari katika vyombo hivyo kuweka kando taaruma na kubaki kufuata matakwa yao.

Kwa namna moja ama nyingine watu wamegawanywa na kuona baadhi ya vyombo vya habari ni bora kuliko vingine. Na kuamini kuwa jambo fulani likitokea kituo X  kitaripoti vizuri habari hiyo kuliko kitakavyo ripoti kituo Y. na hata kama kituo X kikiripoti basi kutakuwa na walakini wa taarifa hiyo.

Nakumbuka maandiko ya Dr. Ayuob Rioba enzi zile anaandikia Raia Mwema, januari 30, 2013 aliandika makala iliyokuwa na kichwa kinachosomeka “Changamoto za vyombo vya habari katika demokrasia ya Tanzania” ambapo ililenga jinsi vyombo vya habari vya Tanzania vinakumbana na changamoto nyingi kuanzia kwa waandishi kufanya kazi kwq kuzingatia matakwa ya wamiliki na kutupilia mbali taaruma.

Nanukuu maneno machache aliyoyaandika katika gazeti la Raia Mwema la siku ya Jumatanno ya januari 6, 2013

 “Katika demokrasia ya vyama vingi ambapo panakuwa na uhuru wa mawazo, lakini pia vyombo mbalimbali vyenye umiliki tofauti, si rahisi Serikali ikafanikiwa kumiliki au kuficha ukweli. Hivyo basi, hata Serikali ikiamua kuendelea kutumia vyombo vyake vibaya kwa propaganda za kudanganya umma, atakayedhalilika ni Serikali yenyewe na vyombo vyake kwa sababu wananchi watajua ukweli kupitia njia nyingine”.

Ukweli huu aliujua tangu zamani ambapo kwa kipindi hicho vyombo vya habari vya umma ambavyo ni gazeti la Habari Leo, TBC1, TBC Taifa ambazo kwa kiasi kikubwa utumiwa na umma mkubwa wa watanzania, vilikuwa vimepoteza mwelekeo.

Pia ukirudi nyuma kidogo, mwaka jana kipindi cha uchaguzi pale Televisheni ya Taifa ya TBC1, ilionyesha upendeleo wa wazi kwa chama tawala, kwa kuonyesha matangazo ya moja kwa moja kutoka sehemu mbalimbali ambapo wagombea wa nafasi mbalimbali wa chama tawala wakiwa majukwaani. Huku vyama vya upinzani vikiachwa pasipo kuwa na mrejesho (coverage) yoyote kutoka televisheni ya taifa.

Ukizingatia hayo ni juzi juzi tu ambapo TBC1 ilirusha moja kwa moja matangazo ya harusi ya tajiri mmoja na kuacha mambo ya muhimu ambayo kama televisheni ilipaswa kuonyesha. Itakumbukwa kuwa hata taarifa ya habari kwa siku hiyo haikuonyeshwa. Kwa kile walichokidai kuwa mwenye harusi alilipia pesa nyingi za muda wa maongezi.

Hiyo ndiyo ilikuwa TBC ambayo kiukweli ilikuwa imepoteza dira na mwelekeo kama televisheni ya taifa. Ambayo kila mwanasiasa hususani kutoka chama tawalaa walitumia kutolea propaganda zao. Na kusahau kuwa wanaongozwa na kauli mbiu ya “Ukweli na uhakika”

“Kwa kweli ilikuwa inachekesha na mara nyingine kuhuzunisha jinsi ambavyo kituo hiki kilikuwa kikiendeshwa kama kituo cha chama, maana TBC ilikuwa inakera na kutia kichefuchefu kuiangalia maana ilikuwa imekoswa mwelekeo. Maana kulikuwa hamna vipindi ambavyo vinavutia watu kuviangalia. Kulikuwa na kipindi maalum kilichojulikana kama “This week in Perspective” kikaondolewa ambapo Dr. Ayoub alikuwa mmoja wa waendesha mjadala. Alisema Amina Ramadhan mkazi wa Dar es salaam.

Kwa upande wake Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ambaye pia ni mwanasiasa na mshauri wa Chama cha ACT- Wazelendo Profesa Kitila Mkumbo aliandika kwenye akaunti yake ya twitter kwa lugha ya kingereza kuwa “Congratulation comrade Dr.Ayoub Rioba on your new appointment as TBC boss. Please bring back This week in perspective programme” akiwa na maana kuwa Hongera Dr. Ayoub Rioba kwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa TBC, nakuomba urudisha kipindi cha This week in Perspective.

Lakini pia bado naikumbuka makala yako ya januari 6, 2013 ambayo nimeielezea hapo juu, uliandika jinsi chombo hiki cha Umma cha TBC kinavyotumiwa na wanasiasa na wanahabari kutumikishwa kisiasa kuliko kutumia taaruma zao katika utekelezwaji wa kazi zao. Uliandika

 “TBC bado inaingiliwa na baadhi ya wanasiasa ambao ama kwa kutokujua au kwa ubinafsi wao, wanaamini kwamba kile ni chombo cha Serikali kama ilivyokuwa kwa Redio Tanzania (RTD). Wanashindwa kubaini kwamba katika demokrasia ya vyama vingi, TBC huru ni bora zaidi na inaweza kuifanya Serikali iaminike zaidi kuliko ile TBC inayokuwa inafugwa na kuingiliwa na Serikali kinyume na matakwa ya taaluma.”
Sasa umeteuliwa Dr. Rioba kuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la utangazaji wa Taifa (TBC), kelele zote ulizozipaza zimesikika na Rais ameamua kukuteua kuongoza taasisi hii muhimu ambayo kwa sasa matumaini wengi yameanza kurejea kuwa huenda TBC ikarudi kama ilivyoanzisha na kufanya kazi kama shirika la umma na kufanana na BBC ambalo ni shirika la Utangazaji la Uingereza.
Nakumbuka pia makala aliyoiandika katika gazeti la Raia mwema la januari 9 ikiwa na kichwa kinachosomeka “Dhima ya vyombo vya habari katika demokrasia ya vyama vingi” ulieleza vyema na kwa umakini wa hali ya juu jinsi wanazuoni mbalimbali wanavyoamini kuhusiana na dhima za vyombo vya habari katika nchi yeyote ile inayofuata misingi ya demokrasia uliandika maneno ambayo ni ya muhimu kwa vyombo vya habari kufanya kazi zao pasipo kuingiliwa.
Kwanza ni haki na uhuru wa kila mtu kuwa na maoni, na kujieleza; pili, haki na uhuru wa kuanzishwa/kuwapo kwa vyombo vya habari; tatu, haki na uhuru wa kufanya kazi ya uandishi /uhariri wa habari bila kuingiliwa au kuzuiwa na mtu au taasisi yoyote mbali na maadili ya kitaaluma ya uandishi; nne, haki ya kupata taarifa kutoka serikalini isipokuwa tu zile ambazo kutolewa kwake hadharani kutaathiri maslahi ya nchi na wananchi kwa ujumla (na maslahi haya ni lazima yafafanuliwe katika katiba na si kuamuliwa na waziri husika); tano, mfumo wa uwajibikaji unakaohakikisha kuwa vyombo vya habari na wanahabari wanatekeleza majukumu yao kwa uhuru na kwa kuzingatia maadili ya taaluma yao; mwisho, sheria ndogo zinazolinda haki na uhuru ulio katika katiba”.
Hizo ndo sifa ambazo vyombo vya habari vinapaswa kuwa nayo katika nchi za demokrasia ikiwemo Tanzania. Ambayo kwa siku za karibuni vyombo vya habari vimekuwa vikilaumiwa kwa wanahabari wake kukosa weredi katika kazi zao.
 Hamis Dambaya ambaye pia ni mmoja wa waandishi nguli katika masuala ya siasa hapa nchini yeye anamuona Dr. Rioba kama mwanahabari shujaa. Ambaye TBC anaimudu vyema kutokana na msimamo wake tangu akiwa mwandishi wa habari chipukizi akiandikia gazeti la serikali la Daily News miaka ile ya 1990.
Dambaya anamfahamu Rioba Vizuri mbali na kufanya nae kazi kwa muda mrefu anamuelezea kitasnia zaidi kuliko Kiuhadhiri. Anaeleza
“Mimi kama mwandishi wa habari namuangalia Dr. Rioba kuwa ni mwandishi mahiri, asiye na uoga, na mwenye uwezo wa kueleza hisia zake kwa jambo lolote lile bila kutafuna maneno”
Pia Dambaya anaeleza jinsi alivyokuwa anavutiwa na Kolamu aliyojulikana kama “By the way” tangu akiwa anasoma na kukumbusha  kuhusu moja ya kichwa cha habari kilichosomeka In rememberance of Bulugu ambapo alivyoeleza kwa kina kuhusu umuhimu wa uandishi wa habari wa kujali maslahi ya umma na kusema wazi kwamba kazi ya uandishi wa habari si kazi ya kufurahisha wakubwa bali kazi ya kusaidia wanyonge ambao mara nyingi haki zao zimekuwa zikipotea.
Huyo ndiyo Dr. Rioba ambaye kwa sasa anachangamoto kubwa ya kuubali mfumo wa TBC kuwa Televisheni ya taifa ili sheria ya vyombo vya habari ikipitishwa vyombo vya habari vijiunge na TBC1, katika habari ya saa mbili usiku na baadhi ya vipindi maalum ambavyo vinahitaji busara za wamiliki wengine wa vyombo vya habari kukubaliana na Shirika la Utangazaji la Taifa.
Ikumbukwe kuwa Dr.Rioba anaingia wakati ambapo bado sakata la urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja kutoka bungeni yakiwa yamesitishwa kwa madai ya hukosefu wa pesa za kurushia matangazo hayo. Jambo ambalo lilizua gumzo kubwa miongoni mwa wananchi na baadhi ya wadau wa habari wakiwemo, Jukwaa la Wahariri Tanzania. Ambapo kwa upande wao waliazimia kutafuta pesa za kuilipa TBC kurusha matangazo hayo moja kwa moja kutoka bungeni Dodoma.
Huu ni mtihani mkubwa sana kwa Dr. Rioba ambao si wa kuingia kichwa kichwa unahitaji maridhiano na kutumia busara nyingi maana watanzania wametulia tu. Wanangoja Bunge lianze ndipo waone kama ni kweli TBC imeamua kusitisha matangazo hayo kwa baadhi ya muda ili wayarekodi na kuyarusha muda wa usiku katika kipindi kiitwacho Leo katika Bunge.
Nimtakie kila la kheri katika ufanisi wa kazi ya Ukurugenzi namalizia kwa maneno machache ya Hamis Dambaya aliyasema Rioba Twakuamini, wewe kijana makini, usilale asilani, Umma wakutegemea, Rioba Tumia vipawa vyako kufanya mabadiliko. Huu mtihani kwako utashinda nakwambia, Rioba- wavivu watakujia , majungu kukuambia , dawa ni kupuuzia hapo utaendelea.
 Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika, Mungu libariki Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) na watanzania wote.

Makala haya yameandikwa na mwanafunzi wa mwaka wa Pili katika fani ya mawasiliano kwa umma, ya Chuo kikuu cha Dar es salaam. Anapatikana kwa namba ya simu ya 0763580901, 0716216249 na barua pepe ya barakangofira@gmail.com.
NI KWELI DR.RIOBA ATAIBADILI TBC AU ATABADILISHWA NA TBC? NI KWELI DR.RIOBA ATAIBADILI TBC AU ATABADILISHWA NA TBC? Reviewed by WANGOFIRA on 21:50:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.