MOTO MKUBWA WATEKETEZA MADUKA ZAIDI YA 150, KARAGWE

 

Moto mkubwa umezuka na kuteketeza soko la mji wa Kayanga wilaya ya Karagwe mkoani Kagera usiku wa kuamkia jana. Moto huo ambao unadaiwa kuwa ulianza majira ya saa 2 ya usiku wa jana umeteketeza vibanda 35 na maduka matano. Wafanyabiashara wengi katika soko hilo wamesikitishwa na kutokea kwa janga hilo, kwani wengi wao wamesema walikuwa na mikopo na hawakuwa na bima ya mali zao.
 Jonasi Nyarugenda ni miongoni mwa wafanyabiashara hao anasema “Moto umeteketeza stoo zangu nne zenye bidhaa mbalimbali kama sukari, mchele, ngano na mafuta, kwakeli ukitathimini kwa haraka siyo chini ya milioni 45 zimepotea.” 


Amesema kwamba alikuwa hana bima katika mkopo wake wa milioni 20 kutoka katika benki. Hasara hiyo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na ukosefu wa vifaa vya kuzima moto. Wananchi wa Karagwe imewapasa kusubiri gari la Zimamoto kutoka Bukoba Mjini (magari ya uwanja wa ndege) ambako ni kilomita 120 mpaka kufika karagwe mjini. Hata hivyo magari hayo yalikuta maduka mengi katika soko hilo yamekwishateketea. 

Diwani wa kata ya Kanoni wilayani karagwe, Sabi Rwazo amesema tukio hilo limewashtua na ni tukio la kwanza la moto kuunguza soko wilayani humo. 

Anasema tatizo la ukosefu wa gari la zima moto linachangiwa na uhaba wa fedha. 
“Mara nyingi katika bajeti yetu imekuwa ikishindwa kununua gari.” Amesema Rwazo na kusema maombi yao yako serikali kuu. 

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Deodatus Kinawiro amesema kuwa serikali ya wilaya yake iko katika mchakato wa kupata gari la zima moto hivi karibuni, “Bahati nzuri nilikuwa Dar es Salaam, nimekutana na kamishna mkuu wa zima moto ameniahidi kunipatia gari jipya,” amesema Kinwiro na kuongeza kuwa, “wakati wowote gari hilo litafika wilayani Karagwe.” 

Hata hivyo baadhi ya wananchi wanasema hawakubaliani na kauli hiyo ya mkuu wa wilaya kwa sababu wamekuwa wakitozwa kiasi cha TZS 30,000 kwa mwezi ili kuchangia huduma za zimamoto wilayani hapo lakini wanashangaa kwa nini hawapati elimu ya kujikinga na majanga, na hakuna hata gari la dharura. 

Mpaka sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana lakini taarifa za awali zimeonesha kuwa kuna Mamalishe mwenye kibanda sokoni hapo aliacha jiko lake bila kuzima hivyo likashika nguo zilizokuwa katika kibanda hicho na kusababisha moto kusambaa ghafla.
MOTO MKUBWA WATEKETEZA MADUKA ZAIDI YA 150, KARAGWE MOTO MKUBWA WATEKETEZA MADUKA ZAIDI YA 150, KARAGWE Reviewed by WANGOFIRA on 21:30:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.