71% YA WATANZANIA WANAPENDA BATA.

 

Utafiti uliofanyika hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebaini kwamba asilimia 71 ya watanzania wanatumia muda mwingi kufanya shughuli zisizokuwa za uzalishaji mali wala tija binafsi kwao na Taifa kwa ujumla. 


Akizundua taarifa ya utafiti huo leo jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi,Ajira,Vijana na watu wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa idadi hiyo hufanya kazi zisizoleta tija kwao na taifa na muda mwingi huutumia kujihudumia binafsi kwa kulala na starehe nyingine. 
Ameeleza kuwa takwimu hizo zinaonesha wazi ni kwa namna gani watanzania wanashindwa kujishughulisha katika kufanya kazi zenye kuwaingizia kipato na badala yake wanatumia muda wao mwingi kufanya shughuli zisizo za uzalishaji hasa kufanya starehe mbalimbali. 


“Ndugu zangu watanzania unakuta mtu amekaa baa au anacheza “poll table” kuanzia asubuhi mpaka jioni na hujui anafanya kazi gani ya uzalishaji, ndugu zangu tuone aibu basi tujishughulishe tulijenge taifa letu ili kujiletea maendeleo yetu na nchi yetu.” 


Aidha, matokeo hayo yamebainisha kuwa asilimia 18.5 ya wananchi wanafanya kazi za uzalishaji na asilimia 10.6 ni wale wanaofanya shughuli za nyumbani zisizo na malipo huku uchambuzi wa kijinsia ukionesha kuwa wanaume asilimia 23.8, wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi ikilinganishwa na asilimia 13.5 ya wanawake. 


Amefafanua kuwa wanawake ambao ni asilimia 16.5 katika utafiti huo wanatumia muda mwingi kufanya kazi za nyumbani zisizo na malipo ikilinganishwa na asilimia 4.4 ya wanaume. 


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisa ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amesema kuwa upatikanaji wa Takwimu hizo utaisaidia Serikali kupata mbinu sahihi za kuondokana na tatizo la ajira nchini kwa kuunganisha nguvu kutoka sekta isiyo rasmi ili kuleta changamoto katika soko la ajira nchini. 


Amesema kuwa hii ni mara ya tano Tanzania inafanya utafiti huo na kubainisha kuwa ulianza mwezi Januari hadi Desemba, 2015 ukitumia sampuli ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 iliyotumika kupata taarifa sahihi ya takwimu hizo. 


Aidha, amebainisha kuwa ili kufanikisha utafiti huo NBS imeshirikiana na wadau mbalimbali ikwemo Wizara ya kazi na Ajira,Shirika la Kazi Duniani (ILO),Benki ya Dunia (WB),Benki ya Maendeleo ya Afrika(ADB) na Asasi zisizo za Kiseikali.

 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu),Jenista Mhagama,akizindua ripoti ya matokeo ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2014 katika Viwanja vya Karimjee,Dar es Salaam. Wengine wanaoshuhudia ni kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Takwimu nchini,Dk.Albina Chuwa, Mkurugenzi wa Sensa ya watu na Takwimu za Jamii,Ephraim Kwesigabo na Mwakilishi kutoka Shirika la Kazi Duniani,Marry Kawar. 
 
Na Raymond Mushumbusi – MAELEZO
71% YA WATANZANIA WANAPENDA BATA. 71% YA WATANZANIA WANAPENDA BATA. Reviewed by WANGOFIRA on 22:11:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.