WIZARA YA ELIMU KUANZA KUTATUA CHANGAMOTO ZA SOMO LA HISABATI.




Mkurugenzi wa Elimu ya sekondari kutoka wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Bi Paulina Mkonongo (wa nne kushoto) akiwa na viongozi wa Chama cha Hisabati Tanzania wakati wa maadhimisho ya siku ya PI duniani yaliyowafinyika uwanja wa Mnazi mmoja jijini Dar es salaam. (picha na Perus Benson)

Na, Mtapa Wilson
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imeahidi kuanza kutatua changamoto zinazopelekea ufaulu mbovu wa somo la hisabati katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi,Bibi Paulina Mkonongo wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya PI duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.


Bibi Mkonongo amesema kuwa somo la hisabati ni muhimu sana kwani ni kichocheo muhimu katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ambapo sasa serikali ikiwa imejikita katika sera ya viwanda.
“Somo la Hisabati ndio malkia wa Sayansi na Teknolojia.  Tunahitaji sana wanafunzi wasome somo la Hisabati ili kuweza kuendeleza Sayansi na Teknolojia ambayo itasaidia katika utekelezaji wa sera ya viwanda amabyo inaonekana kuwa muelekeo wa serikali yetu katika kukuza uchumi wa nchi”

Aidha Bibi Mkonongo amesema Wizara ya Elimu kupitia chama cha Hisabati nchini inafanya tafiti mbalimbali ili kubaini tatizo la ufaulu mbovu katika somo la Hisabati kwa ngazi ya elimu ya msingi na sekondari ambapo tayari kuna jitihada za makusudi zimeshaanza kuchukuliwa ikiwemo kuongeza walimu wa somo la hesabu, kutoa mafunzo kwa walimu wanaofundisha somo hilo, na kuhimiza wanafunzi kusoma somo la hisabati.

“Tunawajibu wa kutoa semina elekezi kwa walimu wa somo la hisabati. Lakini pia lazima wanafunzi lazima wahimizwe kusoma hisabati kwa kuwekewa misingi bora itakayowasaidia kuepuka dhana potofu ya kusema hisabati ni somo gumu”


Maadhimisho ya siku ya PI duniani yaliadhimishwa kwa maonesho mbalimbali ya vifaa vya kujifunza somo la hisabati kwa vitendo ambapo shule mbalimbali za msingi na sekondari zilishiriki.
WIZARA YA ELIMU KUANZA KUTATUA CHANGAMOTO ZA SOMO LA HISABATI. WIZARA YA ELIMU KUANZA KUTATUA CHANGAMOTO ZA SOMO LA HISABATI. Reviewed by WANGOFIRA on 09:08:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.