WANAFUNZI UDSM NA UDOM WAMMWAGIA SIFA KEDEKEDE PROF. NDALICHAKO KWA KUTUMBUA MAJIPU HESLB
NA,
BARAKA NGOFIRA
0763580901,
0716216249
Waziri wa Elimu,Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) |
Ni
furaha isiyo na kifani mioyoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, pale
waliposikia taarifa kuhusu kusimamishwa kazi kwa wakurugenzi wanne wa bodi ya
mikopo (HESLB). Kutokana na kile ambacho wao wanaeleza wazi kuwa walikuwa
wamechoshwa na utendaji wa bodi hiyo iliyokuwa inafanya kazi kwa mazoea na
ubadhilifu wa fedha za vijana wa kitanzania kwa muda mrefu.
Lakini
pia kwa wale ambao awanufaiki na bodi huku sifa za kupata mkopo wakiwa nazo,
nao walisikika sauti zao zikipazwa kwa sauti kuu, zikisema afadhali maana
tumeteswa kwa muda mrefu, wazazi wenu wanakatwa kodi kila kuchapo. Watoto wa
wakulima wanakosa mkopo huku watoto wa vigogo wakipewa hela hata pasipo kuomba
na kuwaringishia pesa ambazo kwa namna moja ama nyingine hazikuwa za kwao.
Siku
ya jumanne majira ya saa asubuhi zilienea taarifa juu ya waziri wa Elimu,
Sayansi, Teknolojia na mafunzo ya ufundi Profesa Joyce Ndalichako kuwa
amewasimamisha kazi watendaji 4 wa bodi ya mikopo ya Elimu ya juu (HESLB)
akiwemo mkurugenzi mtendaji wa bodi hiyo Bwana George Nyatenga na wenzake watatu
kwa utendaji wao usioridhisha pamoja na kuwa wazembe. Jambo linaloibua matatizo
makubwa na kuathiri maisha ya wanafunzi wa vyuo vikuu kogoma na baadhi yao
kuandamana kudai pesa zao.
Pamoja
na kusimakishwa kwa kwa wakurugenzi wengine watatu ambao ni Yusufu Kisare
(Fedha na utawala), Juma Chagonja (urejeshaji mkopo) pamoja na Onesmo Laizer
(upangaji na utoaji mikopo). Ambapo wote hawa wanahusika kufanya ubadhirifu wa
zaidi ya Bilioni 3.2, ambazo zililipwa kwa watu waliokufa, waliositisha masomi,
waliomaliza masomo na wengine kulipwa zaidi ya mara mbili. Lakini jambo la
kushangaza ni kuwa ni zaidi ya wanafunzi 19,348 kupewa mkopo pasipo kupitishwa
na kamati ya mikopo, huku wanafunzi 54,299 kupewa mikopo pasipo kuomba na
kusababisha watoto wengi wenye vigezo na waliolipa zaidi ya Tsh 50,000 katika
harakati za kuomba na kutuma maombi kunyimwa mikopo. Huku wengine wakigawana
pesa kwa kujuana na kubagua vijana wa walala hoi ambaao hawajui kesho yao
itakuwaje.
Lakini
pia kwa upande wangu kama mwanahabari na mwanafunzi pia namshukru sana waziri
Profesa Ndalichako kwa uamuzi wake, kwani kila mara suala la utendaji mbovu wa
Bodi ya Mikopo umekuwa ukilalamikiwa sana na watu wengi. Hasa wanafunzi na
wazazi kwani wanatumia pesa nyingi kuomba huku wengine wakithubutu kuomba zaidi
ya mara 4 pasipo kupata mkopo huku sifa zote wakiwa nazo.
Lakini
pia wanafunzi wa vyuo vikuu wengi wamekuwa wakieleza wazi jinsi taasisi hii inafanya kazi kwa mazoea na
kusahau kuwa sasa ni muda wa kazi tu, pia wamekuwa wakieleza wazi jinsi mikopo
hii inavyotolewa pasipo kuzingatia vigezo na kufanya baadhi ya vijana wa
kitanzania tena hali ya chini kutoendelea na masomo ya elimu ya juu, kwa
saababu ya kukosa mkopo huku sifa na vigezo wakiwa navyo. Na kushangaa wengine
waliosoma shule wanazoziita wao eti ni za “SAINT” wamepata mkopo tena kwa
asilimia mia moja lakini wao waliosoma shule za kayumba wananyimwa.
Pamoja
na jitihada zote ulizozionyesha lakini bado kuna haja ya kufumuliwa yote na
kuundwa upya, ili kuweza kuleta ufanisi wa kazi ambao utasababisha vijana wengi wa kitanzania kufaidi matunda ya
nchi yao japo kwa kuwezeshwa kusoma elimu ya juu.
Elihazina
Kangalu ni mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya ualimu katika chuo kikuu cha
Dodoma (UDOM) anasema “kwangu mimi ni sahihi kwa sababu kwa sasa utendaji wao
umekuwa ukidorora sana na wanafunzi wengi wamekuwa wakilalamikia utendaji wa
bodi hii”
Lakini
pia Celvin Nkya mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya ualimu chuo kikuu cha Dodoma
yeye anasema “ni jambo zuri kwa sababu kati ya bodi hii imekuwa miongoni mwa
taasisi ambayo watu wake wamekuwa wakifanya kwa mazoea na kujisahau kuwa
wanawatumikia watanzania ambao ni wasomi na viongozi wa kesho.
Nae
Rebeka Kishegena ambaye mhitimu wa shahada ya kwanza ya masuala ya kijamii
(Sociology) katika chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM) yeye anasema waondolewe
tu kwa sababu wamekuwa wakiwahujumu wanafunzi pesa zao na kuwacheleweshea pesa
zao huku wakijua kuwa kuna bajeti ambapo wamesababisha wanaafunzi wengi kupata
pesa za mkopo na kuishia kulipa madeni”.
Kwa
upande wake Marium Thabiti mwanafunzi wa Shahada ya kwanza ya mawasiliano kwa Umma kutoka chuo kikuu cha
Dar es salaam yeye anasema “ ni sawa kama uchunguzi umefanyika na wamebainika
wana makosa ni lazima wawajibishwe. Kwa sababu kila kazi ina kanini na taratibu
zake na ni lazima wala si ombi kuzifuata” na kuongezea kuwa “kwa kuwa wamekiuka
ni lazima wawajibishwe ili iwe funzo kwa wengine walio katika ofisi za umma”.
“Kwa
kweli hilo suala lina pande mbili kwa maoni yangu, inapaswa nijiulize uhalali
wa kusimamishwa na pili matunda ya kuteuliwa kwa viongozi wapya. Nikianza na
uhalali wa kusimamishwa nafikiri kila mwanafunzi anafahamu kuwa ni halali
kutokana na taarifa walizosema kuwa kila mwanafunzi amepewa mkopo jambo ambalo
halina ukweli wowote. Na ucheleweshwaji wa fedha za mikopo kwa wastahiki jambo
ambalo limekuwa sugu katika miaka yangu miwili niliyopo hapa chuoni” alisema
Pious Sylvester mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya Sheria kutoka Chuo kikuu
chaa Dar es salaam.
Lakini
pia Neema Mbundamila mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya Mawasiliano kwa Umma
kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam UDSM yeye anasema “Ni jambo la kusikitisha
sana kuona pamoja na juhudi za Rais Dokta Magufuli kuhakikisha anatafuta fedha
ili ziwanufaishe wanafunzi wa Elimu ya Juu na wengine wanahitaji mkopo lakini
bado kuna baadhi ya wakurugenzi wanakwamisha juhudi hizo”.
Na
kuongeza kuwa ikiwa wakurugenzi wa Bodi ya mikopo waliosimamishwa kazi
watakutwa na hatia basi sheria kali zichukuliwe juu yao ikiwa ni pamoja na
kufilisiwa mali na fedha zao na kupelekwa kwa walengwa. Pia anamuomba Profesa Ndalichako kuangalia upya
waombaji wa mkopo ambao wanaendelea na masomo yao kwa mwaka wa pili, tatu na
nne lakini hawakupata mkopo, japo waliahidiwa na Rais Magufuli kipindi cha
Kampeni zake.
Na
kusisitiza kuwa “waathirika ni wengi na athari zinazidi kuongezeka hivyo ni
muhimu kwa serikali kuwapitia mkopo kwani hakuna ajuaye kesho ya yule
anayemfadhili kuwa itakuwaje endapo uchumi ukiyumba au kufariki lakini pia
anaongeza kwa kusema wakati watoto na wanafunzi wa watanzania maskini na wa
wakulima wanakosa mkopo kwa kunyimwa kimakusudi kabisa kwa kisingizio cha fani
wanazosomea, jambo linalopelekea wengi kupoteza haki yao ya msingi ya kitaba ya
kupata elimu na mahitaji mengine kwa sababu tu ya upuuzi na uzembe wa
wakurugenzi wa wasiowaadilifu” na kumuomba waziri profesa Ndalichako
kuwawajibisha vilivyo.
Kwa
upande wa shirikisho la wanafunzi wa Elimu ya juu ( TAHALISO) kupitia
Mwenyekiti wa mawaziri wa mikopo ya elimu Juu Ndugu Shitindi Venance, ambaye
pia ni msemaji wa shirikisho hilo anasema kuwa wamepokea kwa furaha kubwa kusimamishwa
kwa wakurugenzi hao wa bodi ya mikopo.
“Sisi
kama shirikisho la wanafunzi wa Elimu ya Juu (TAHILISO) tumepokea kwa furaha
kubwa tena sana na tupende kumpongeza waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi kwa hatua aalizozichukua. Kwa upande wetu TAHILISO tumekuwa
tukinyanyaswa na wakurugenzi hawa hasa Mkugenzi mkuu wa bodi ya mikopo
aliyesimamishwa ndugu George Nyatenga amekuwa akitutishia sana hasa mimi
mwenyewe, kwani tayari keshaniandikia barua mbili kupitia uongozi wa chuo ili
nifukuzwe chuo lakini nashukru sijafukuzwa kwani hata uongozi wa chuo unaelewa
napigania maslahi ya vijana wa kitanzania na watoto wa maskini na wakulima
ambao hawana uwezo wa kujisomesha au kusomeshwa na wazazi au wadhamini wao”
Amefafanua
kuwa mpaka sasa zaidi ya wanafunzi 8000 nchi nzima awajalipwa pesa zao za mkopo
tangu wameanza masomo yao Novemba mwaka jana. Hivyo kuomba viongozi na makaimu
walioteuliwa kulifanyia kazi kwa haraka iwezekanavyo ili kunusuru maisha ya wanafunzi
hawa, wanaoishi kwa kukopeshwa na wenzao tena kwa riba kubwa lakini kushindwa
kulipa kwa wakati jambo linalojenga uadui na wivu miongoni mwao.
Lakini
pia kama msemaji wa Mawaziri wa Mikopo TAHALISO Bwana Shitindi alisema “inabidi
bodi hii itambue kuwa inafanya kazi na vijana wasomi tena watu wazima na wala
si watoto wa chekechea , hivyo na Mkurugenzi atakayechaguliwa kurithi nafasi ya
Nyatenga ajiandae kabisa kujua anakuja kufanya kazi na wasomi wanaojua hali
halisi ilivyo, wakiwa na akili timamu kabisa ya kufanya tathimini ya na
kuchambua ukweli ni upi na ubaya ni upi kwa hiyo aje kazini akitambua hilo
kabisa na kama naye atatambua hilo hakika hatadumu bodi ya mikopo hataondolewa
tu”
Na
kumalizia kwa kutoa Ushauri kuwa Mkurugenzi ajaye ni vyema na ni lazima akasome
utafiti uliofanya na Profesa Maboko na kuchapishwa mwaka 2011, unaotoa miongozo
mizuri kuhusu mageuzi ya Bodi ya mikopo. Na kuamini kuwa Mkurugenzi
atakayeteuliwa atayamaliza matatizo yote ya mikopo na kufanya wanafunzi wafurahie
nchi yao na masomo yao vyuoni waishi salama pasipo kucheleweshewa pesa kutoka
bodi ya mikopo ambazo muda mwingi zimegeuka kulipa madeni.
Makala
hii imeandaliwa na Baraka Ngofira, mwanafunzi UDSM-SJMC. Anapatikana kwa
mawasiliano ya 0763580901, 0716216249 au barua pepe ya barakangofira@gmail.com kwa maoni na
ushauri zaidi.
WANAFUNZI UDSM NA UDOM WAMMWAGIA SIFA KEDEKEDE PROF. NDALICHAKO KWA KUTUMBUA MAJIPU HESLB
Reviewed by WANGOFIRA
on
22:09:00
Rating:
No comments: