THAMANI YA MWANAHABARI KWA JAMII
NA, BARAKA NGOFIRA

0763580901, 0716216249

Hakuna shaka yoyote kuwa kuna mtu hajui umuhimu wa vyombo vya habari katika kuhabarisha umma, na kufanya taifa lolote lile liweze kuwa na maendeleo makubwa. Si tu maendeleo bali pia vyombo vya habari vimekuwa vikifanya kazi kubwa ya kufichua maovu mbalimbali yanayotokea kwenye jamii zetu.

Rudi nyuma kidogo wakati wa uchaguzi mkuu uliopita mwaka jana jinsi vyombo vya habari vilivyofanya kazi kubwa ya kuhabarisha umma, kuhusu matukio yote na wengine wakawa hawapitwi na lisaa hata limoja kabla hawajasikiliza redio, kusoma gazeti au kutazama televisheni.

Hii ni kuonyesha tu kuwa jamii ya sasa yetu haiwezi kuishi pasipo vyombo vya habari, na kama kuna mtu anabisha ajaribu kujifungia kwa siku mbili chumbani kwake asishike simu, asisikilize redio wala kusoma gazeti na wala kutazama televisheni hapo ndipo atakapoelewa kile ninachokimaanisha.
Mbali na kuwepo kwa mitandao ya kijamii ambayo imesaidia kusambaa za taarifa ambazo mara nyingi huwa ni za uongo lakini bado umuhimu wa vyombo vya habari bado huko palepale, tazama asubuhi watu wengi husema wanaamka na BBC, DW pia hawaachi kusikiliza uchambuzi wa magazeti ya nyumbani katika redio na televisheni za nyumbani.

Hapa ndipo unaona jinsi vyombo vya habari vinavyofanya kazi kwa kusaidiana na jamii kuibua na kufichua maovu yanayotokea ndani ya jamii zetu, vyombo vya habari kwa sasa vimekuwa sehemu ya maisha ya wanajamii katika nchi yoyote ile duniani. 

Piga picha miaka ya 1980 taarifa mbalimbali za kiserikali zilikuwa zinawafikiaje wananchi? Au watu walitambuaje kuwa hayati Baba wa Taifa Mwl.Nyerere anafanya ziara kwenye maeneo yao? Lakini leo mambo ni tofauti kabisa kwani leo matukio mengi yakitokea hasa ya kitaifa hurushwa moja kwa moja kwenye vyombo vya habari hususani redio na televisheni.

Hapo ndipo utajua kuwa vyombo vya habari vina umuhimu mkubwa kwa jamii yetu, lakini cha ajabu na cha kushangaza taarifa au mambo mengi yanayofanywa na vyombo hivi vya habari vinapendwa sana na vingi vinasifiwa lakini wanahabari hawapendwi.

Nasema hawapendi kwa sababu maisha wanayoyaishi wanahabari ni tofauti kabisa na kazi zao, wengi hudharauliwa, wanachekwa na kupuuzwa na baadhi ya watu na pengine viongozi wa sekta binafsi na wale wa kiserikali.

Pia, wanafunzi ambao wanasoma fani hizi nao hawapewi kipaumbele kwa kuambiwa kuwa fani wanazosoma si kipaumbele kwa wao kupewa mkopo ili wasome na kubobea katika fani hizi za habari. Hivyo ndivyo hali ilivyo.

Inashangaza sana kuona mwanahabari mwanafunzi hananyimwa mkopo na pale anapoenda kuuliza kwa nini amenyimwa mkopo na sifa na vigezo vyote anavyo. Jibu analopewa ni kuwa fani anayosoma si kipaumbele cha yeye kupata mkopo wa kumuwezesha yeye kusoma elimu ya juu.
Wakiwa na maana kuwa kama mtu hana uwezo wa kujilipia ili asome fani zinazohusiana na masuala ya habari basi inambidi abadili maamuzi aende fani nyingine ambazo ni kipaumbele. Ikiwemo ualimu na nyingine ambazo kwa sasa watu wanaenda kusoma ili mradi tu na wao wajulikane kuwa walisoma elimu ya juu na kuongeza idadi ya wasomi tena wengine wakiwa na shahada za juu. Lakini walichokisoma hawakijui kwani haikuwa dhumuni lao kusomea fani hizo.

Kwa hili inabidi serikali iliangalie kwa makini kwani inachangia kwa kiasi kikubwa kukosekana kwa watu mahili na wanahabari machachali ambao wangesaidiana na serikali pamoja na wananchi ili kujenga nchi yetu ili iweze kuwa na uchumi imara na wenye kuleta tija kubwa kwa wananchi wa nchi yetu.

Kwa hili pia nimuombe waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo Bwana Nape Nauye, kwani ni jukumu lake kututetea kama waziri wa Habari, na kama ukishindwa mtetezi mwingine hatuna. Tupiganie na ututetee maana ukishindwa wewe kama waziri mwenye dhamana basi hatujui ni nani hatatutetea.

Najua waziri huyu anafahamu fika kuwa wanafunzi wanaosoma fani hizi za habari hawapewi kipaumbele cha kupata mkopo kwa ajili ya wao kusoma fani hizi za habari. Kwa kuambiwa kuwa fani wanazozisoma si kipaumbele na hapa ndipo nabaki na maswali mengi ya kujiuliza iweje wanahabari si vipaumbele na habari iwe kipaumbele?

Inashangaza sana mtu kutothaminiwa lakini kazi yake kuthaminiwa na kupewa kipaumbele, tazama kazi wanazozifanya waanahabari, wanawafanya wanasiasa kuwa maarufu na kuwajengea majina makubwa. Lakini wanahabari wakiwa bado hawathaminiwi, wala kusikilizwa na wanasiasa hawa ambao washajengewa majina na vyombo vya habari.

Ni ombi langu kwa waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bwana Nape Nauye utusaidie, utupiganie na umshawishi waziri wa Elimu na mama yetu Prof. Ndalichako ili nasi tupewe kipaumbele katika mwaka ujao wa masomo la sivyo, Taifa letu litakuja kujuta miaka ya mbeleni kwa kukosa wanahabari mahiri na waliobobeaa kwenye fani hii.

Kwani ni jambo la aibu tena kubwa kwa nchi yetu kuona baadhi ya vyombo vya habari kuendelea kufanya madudu ambayo kiukweli unabaki kujiuliza ni kweli watu hawa wana taaruma ya habari au la?  Kwani ni aibu kabisa hata kusema hadharani kuwa mimi ni mwanahabari.

Na kufanya taaruma yetu ya habari watu wengi kuiona kama ni ya watu wambea ambao ni wenye kufuatilia maisha ya watu. Na baadhi yetu kudharauliwa na kuitwa wadaku. Jambo ambalo ni aibu kubwa lakini ni kwa sababu tu baadhi ya wenzetu ambao naamini hawanaa taaruma hii wanafanya kazi hizo za udaku.

Mwisho ni ombi langu kwa wadau na wanahabari wote tuunganishe nguvu zetu pamoja tuiombe 
 serikali yetu tukufu ituangalie kwa jicho la pili na watufanye nasi tuwe kipaumbele kama zilivyo fani nyingine kama Ualimu, masomo ya Afya na fani nyingine kwani umuhimu wetu ni sawa kabisa na tunategemeana na fani hizo na pia tunatumika kama daraja la kupitishia taarifa mbalimbali. 

Kwa hiyo ni jukumu letu kama wanahabari kuunganisha nguvu na kuisisitiza serikali ambayo naamini ni sikivu kwani nakumbuka hata Rais wetu Magufuli alituahidi kuwa tuunde chombo ambacho atakutana nacho ili kujadili kero na ambazo tunakabiliana nazo ambazo hata kutopewa kipaumbele katika elimu ya juu likiwa moja wapo.

Makala haya yameandikwa na mwanafunzi wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo kikuu cha Dar es salaam. Anapatikana kwa mawasilano ya 0763580901, 0716216249 na barakangofira@gmail.com.
THAMANI YA MWANAHABARI KWA JAMII THAMANI YA MWANAHABARI KWA JAMII Reviewed by Unknown on 04:13:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.