Ndoa kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971

KUFUATANA na na sheria ya ndoa ya mwaka 1971, ndoa ni muungano wa hiari kati ya mwanamme na mwanamke unaokusudiwa kudumu kwa muda wa 

maisha yao.

Aina za ndoa

Kuna aina mbili za ndoa;
i) ndoa ya mke mmoja, hii ni ndoa ambapo mwanamme ana mke mmoja tu.
ii] ndoa ya wake wengi, hii ni ndoa ambayo
mwanamme ana wake zaidi ya mmoja.
Ndoa itokanayo na dhana ya ndoa; hii ni ndoa ambayo mwanamke na mwanamme wamekaa pamoja ndani ya nyumba kama mke na mme kwa muda wa miaka miwili na kuendelea na wote wakapata hadhi ya kuwa wanandoa.

Vipengele gani vya kuzingatia ili wanaotaka kufunga ndoa wakubaliwe kisheria kufunga ndoa

(a) Ni lazima muungano uwe wa hiari

Mume na mke wawe wameamua kuishi pamoja kwa ridhaa yao wenyewe. Hii inamaanisha kusiwe na kulazimishwa, kuhadaiwa kwa aina yoyote kwani
muungano kama huo utakuwa batili kisheria.
Ni kosa la jinai kushiriki katika shughuli ya ndoa ambayo mmoja wapo au wote wamelazimishwa kufunga ndoa.

(b) Muungano uwe ni kati ya mwanamke na mwanamme

Muungano wa watu wa jinsia moja hata kama ni wa hiari muungano huo hautambuliki kisheria.
Pia mtu huhesabika mwanamke au mwanamme kutokana na
sehemu za siri alizozaliwa nazo na siyo alizozipata baadaye.

Jamii inachukulia kuwa ndoa ni njia pekee
ya kujipanua, upanukaji huku ni kwa kuzaa watoto.

Kwa hali hiyo ili kupata watoto ni lazima ndoa iwe kati ya mwanamme na mwanamke.

(c) Muungano huo uwe unakusudiwa kuwa wa kudumu

Pamoja na kuwa mwanamke na mwanamme wameamua kuishi pamoja kwa hiari yao lakini siyo kwa kutodumu muungano huo hautambuliki kisheria
kama ndoa.

Muungano ni lazima uwe wa kudumu
maisha yote au kama mmoja wao amefariki au kama ndoa imekumbwa na matatizo na mahakama ikaona ni bora kutoa talaka kwa yeyote aliyefika kulalamika.

(d) Wanandoa wasiwe maharimu
Maharimu ni watu walio na mahusiano ya karibu ya damu au kindugu.

Wawili wanaoamua kufunga ndoa wasiwe na uhusiano wa karibu kindugu.

Inakatazwa katika kifungu cha 14 cha Sheria ya ndoa ya mwaka
1971 mtu kuoa au kuolewa na mzazi wake, mtoto au mjukuu wake, kama ni dada yake, mama au shangazi au baba wa mjomba wake, baba au mama wa kambo na mwanaye aliyemfanya kuwa mtoto
wake (adopted child).

(e) Wanandoa wawe wametimiza umri unaokubalika kisheria

Mwanamke na mwanamme wawe wametimiza miaka 18 ili kufunga ndoa.

Hata hivyo mwanamke anaweza kuolewa akiwa na umri wa chini ya miaka18 lakini sio chini ya miaka 15 kama atapata idhini
ambayo hutolewa na baba na kama hayupo ni mama au kama wote wamefariki idhini itatolewa na mlezi wa binti huyo.

Kama wote wamefariki basi hatahitaji idhini.

Kuna wakati katika mazingira fulani
mahakama inaweza kutoa idhini kwa binti kuolewa akiwa na miaka 14 lakini si chini ya hapo ikiwa ataonekana kwa mfano ana mimba.

Pia mwanaume anaweza kuruhusiwa na mahakama kuoa akiwa na umri wa miaka chini ya 18 lakini lakini si chini ya 16
kama ataonyesha kuelewa jukumu lake kama mtu mzima.

Lakini hii ni pale ambapo kuna tatizo kama la kumpa msichana mimba ndipo mahakama inaweza
ikatoa idhini.

Hii inathibitishwa katika ombi la kuoa la Shabiri A. M Virji (1971) HCD no.407 la Mahakama Kuu ya Tanzania, mwombaji alikuwa na miaka 16 lakini
alimpa mimba binti wa miaka 18.

Mahakama katika kuchunguza ombi la mvulana la kuoa ilitoa kibali kwa
sababu wote wawili walipendana sana na wazazi wao hawakuwa na kipingamizi cha wao kuoana.

(f) Kusiwe na ndoa inayoendelea

Kama mwanamke ana ndoa inayoendelea na
inatambulika kisheria haruhusiwi kufunga ndoa nyingine (polyandry).

Kadhalika kama mwanamme
ana ndoa ya mke mmoja au kama ni mwislamu ana wake wanne tayari hataruhusiwa kufunga tena
ndoa.

(g) Kusiwe na kipingamizi

Kama ndoa imezuiwa na Mahakama au halmashauri ya usuluhishi kutokana na uwezo zilizopewa na ndoa ikaendelea kufungwa kabla ya wenye
kupeleka kipingamizi hawajasikilizwa au Mahakama imeshaamua ndoa hiyo isifungwe basi ndoa hiyo
itakuwa ni batili.

(h) Mfungishaji ndoa kutokuwa na mamlaka
Kama wanaofunga ndoa wanajua wazi kuwa
anayewafungisha ndoa hana mamlaka hayo na kwa makusudu wakakubali awafungishe ndoa basi ndoa hiyo itakuwa ni batili.

Mfungishaji ndoa ili kuwa na
mamlaka anapaswa kusajiliwa na Msajili Mkuu wa Ndoa na kupewa leseni ya kufungisha ndoa.

(i) Kutokuwepo kwa wafunga ndoa

Kama ndoa imefungwa bila ya wafunga ndoa wote kuwepo basi ndoa hiyo haitambukuliwa kisheria.

Hata hivyo sheria inaruhusu ndoa kufungwa ikiwa mmoja
wa wafunga ndoa hayupo, kama mfunga ndoa ambaye hayupo amewakilishwa na mtu ambaye alikuwepo wakati mfunga ndoa hayupo, alipotoa ridhaa yake ya kuoa au kuolewa.

(j) Mashahidi wa ndoa

Ili ndoa itambulike kisheria ni lazima ishuhudiwe na mashahidi wasiopungua wawili ambao wanaruhusiwa
kisheria yaani umri wao usipungue miaka 18 na wafahamu kinachosemwa na kutendeka wakati wa kufunga ndoa.

(k) Kuwa katika eda

Eda ni kipindi cha kukaa ndani kinachotolewa kwa mwanamke wa kiislamu aliyeachika katika ndoa au aliyefiwa na mumewe, ili taratibu fulani za kidini
zifanyike.

Kama mwanamke ambaye ndoa ilifungwa kiislamu anaolewa wakati wa kipindi cha eda hakijaisha basi ndoa hiyo itakuwa batili.

Lakini mfaruku hiyo ni pale iwapo mtalikiwa awe anafuata dini ya Kiislamu.

Kama atabadili dini baada ya kufiwa au kupewa talaka masharti ya eda
hayatambana na atakuwa huru kuolewa.

Aina za ufungaji ndoa na taratibu za kufuata

Taarifa ya nia ya kuoa

Kwanza kama mwanamke na mwanamme wanataka kufunga ndoa ni wajibu taarifa ya nia ya kufunga ndoa itolewe kwa mfungishaji ndoa siku 21 kabla ya
siku ya kufunga ndoa.

Taarifa hiyo ionyeshe mambo yafuatayo:-

(i) Majina kamili na umri wa wanaotaka
kuoana.

(ii) Uthibitisho kwamba hakuna kipingamizi
dhidi ya hiyo ndoa wanayotarajia kufunga.

(iii) Majina kamili ya wazazi wao na sehemu
wanakoishi.

(iv) Hadhi ya wafunga ndoa, yaani kama ni
mwanamke ifahamike kama hajaolewa,
ametalakiwa au ni mjane na mwanamme
pia anapaswa kama hajaoa, au ana mke au/wake wengine (hii ni kwa ndoa za
kiserikali na kiislamuu) au kama ametaliki.

(v)Kama muolewaji ana umri chini ya miaka 18, jina la mtu aliyetoa idhini ya yeye
kuolewa kama yupo ionyeshwe.

(vi) Kama ni ndoa ya kiserikali au kiislamuu
hapana budi kueleza kama ndoa ni ya wake
wengi au inatazamiwa kuwa ya wake wengi,
majina ya wake waliopo yatajwe.

Pia katika fungu hili kama mtu anataka ndoa iwe ya mke mmoja anapaswa kueleza.

Baada ya taarifa yenye maelezo haya kufikishwa kwa mfungishaji ndoa yeye anawajibika kutangaza hii nia ya kufunga ndoa.

Sababu ya kufanya hivyo ni ili kama kuna mwenye kipinganizi na ndoa hiyo atoe taarifa.

Matangazo haya hutolewa kama ndoa inatarajiwa kufungwa kidini, sehemu za ibada.

Kama ni ndoa ya kiserikali tangazo litabandikwa nje ya ofisi ya msajili wa Ndoa ambaye ni Mkuu wa Wilaya.

Vipingamizi vya ndoa viko vya aina
mbili, cha kwanza ni kile cha kisheria yaani
kama ndoa itakayofungwa itakuwa batili.

Kipingamizi cha pili ni kama muoaji ana mke au wake wengine tayari, hivyo mke au wake wanaweza kutoa kipingamizi kama uwezo wa muoaji kifedha ni mdogo kiasi kwamba kuongeza mke mwingine kutazidisha shida.

Mfungishaji ndoa anapopokea taarifa ya kupinga ndoa isifungwe, ataipeleka taarifa hiyo kwenye Baraza la Usuluhishi la Ndoa.

Huko aliyewekewa kipingamizi na aliyeweka wataitwa na kila mmoja
atajieleza.

Baada ya kusikiliza pande zote Baraza
lina uwezo wa kuamua ndoa hiyo ifungwe au isifungwe na mfungishaji ndoa atafuata uamuzi wa Baraza.

Kama mtu atatoa kipingamizi cha uongo na
ikithibitika hivyo, adhabu yake anaweza kufungwa kifungo kisichozidi miaka mitatu.

Baada ya kipengele hiki kutimizwa ndoa inaweza kufungwa.

Aina za ndoa

Kama tulivyosema awali kuna aina mbili za ndoa.

(a) Ndoa ya mke mmoja

Huu ni muungano unaoruhusu mwanamme kuoa si zaidi ya mke mmoja, mfano wa aina hii ya ndoa ni ndoa ya Kikiristo.

(b) Ndoa ya zaidi ya mke mmoja

Huu ni muungano unaoruhusu mwanamme kuoa mke zaidi ya mmoja, mfano wa aina hii ya ndoa ni ndoa za Kiislamu na ndoa za kimila.

Sheria ya ndoa inatambua aina tatu za ufungaji wa ndoa yaani kiserikali, kidini na kimila.

Ndoa hizo zaweza kufungwa kwa kufuata taratibu za kidini au za kiserikali.

Utaratibu huo utafuata au kuzingatia kama wanandoa ni waumini wa dhehebu
fulani au la.

(a) Ndoa ya kidini

Ndoa hii hufungwa kwa mujibu wa taratibu ya dini husika hivyo ni lazima masharti yote yatimizwe kisheria na taarifa ya nia ya kufunga ndoa itolewe na ndoa
ifungiwe mahali pa wazi panapokubalika kisheria na mfungishaji awe na mamlaka hayo kisheria.

(b) Ndoa ya kiserikali

Ndoa hii hufungwa mbele ya Mkuu wa Wilaya ambaye ndiye Msajili wa Ndoa.

Ndoa itafungwa katika ofisi ya Msajili au mahali pengine popote palipotajwa
katika leseni yake ya kufungisha ndoa.

(c ) Ndoa ya kimila

Ndoa inaweza kufungwa kimila iwapo mmoja wa wafunga ndoa au wote wawili wanafuata sheria za
mila za kabila fulani ambapo mwandishi wa ndoa za kimila ni Katibu Tarafa.

Ndoa ya kimila hufungishwa na
mtu anayetambulika kimila kuwa ana uwezo huo.

Ni muhimu sana Katibu Tarafa kuhudhuria kwenye ufungishaji huo wa ndoa kwani ndiye atakayehusika na kuleta vyeti vya ndoa kutoka kwa msajili.

Ufungaji ndoa nje ya nchi

Kifungu cha 8 cha sheria kinampa mamlaka Waziri wa Sheria kuteua baadhi ya maofisa ubalozi kuwa wasajili wa ndoa.

Ni lazima msajili aridhike kuwa masharti yote yametimizwa ndipo afungishe ndoa.

Kuna masharti ya nyongeza kama angalau mmoja wa wafunga ndoa awe ni Mtanzania. Pia kama mmoja wa wafunga ndoa si Mtanzania ni lazima Msajili aridhike kuwa ndoa inayokusudiwa kufungwa
itatambulika kisheria katika nchi ambayo huyo mmoja wa wafunga ndoa ni mkazi.

Utaratibu unaotumika kufungisha ndoa hizi ni sawa na ule unaotumika
katika kufungisha ndoa za kiserikali.

Dhana ya kuchukulia ndoa

Kuna dhana inayokanushika (rebuttable
presumption) kuwa mwanamme na mwanamke wakiishi pamoja kwa miaka miwili au zaidi huchukuliwa kuwa ni mke na mume mbele ya sheria
japokuwa hawakuwahi kufunga ndoa. Dhana hii imeelezwa katika kifungu cha 160 cha Sheria ya Ndoa.

li dhana hii iwepo ni lazima yafuatayo yathibitishwe.

(i) Lazima ithibitike kwamba mwanamke na mwanamme wameishi pamoja kwa muda wa miaka miwili au zaidi kwa mfululizo.

(ii) Lazima pia ithibitike kuwa umma
unaowazunguka unawachukulia na
kuwapa heshima kama mke na mume.

(iii) Lazima ithibitishwe kuwa watu hao
walikuwa na uwezo wa kuwa mke na mume
wakati walipoanza kuishi pamoja kama
umri ulikubalika kisheria.

(iv) Ni lazima pia ithibitishwe kuwa kati ya hao wawili au wote hakuna aliye na ndoa
inayoendelea.

Ndoa batili na sababu zinazoweza kuifanya ndoa kuwa batili

Ndoa batili ni ndoa ambayo itachukuliwa kisheria kuwa ni ndoa halali hadi hapo amri ya kuivunja itakapotolewa.

Ndoa batili ni halali kama ndoa
nyingine isipokuwa ina kasoro fulani.

Wanandoa katika ndoa hiyo wana haki na wajibu sawa kama ilivyo katika ndoa nyingine zisizo na kasoro.

Kadhalika watoto waliozaliwa katika ndoa ya namna hii ni halali
na wana haki zote kisheria.

Ni vitu gani vinavyofanya ndoa kuwa batili?

1. Maradhi ya zinaa

Kama wakati wa kufunga ndoa mmoja wa wafunga ndoa alikuwa na maradhi ya zinaa na yule asiye na ugonjwa kama wakati wa kufunga ndoa alikuwa hajui lolote anaweza kulalamika mahakamani na
ndoa ikavunjwa.

2. Kukataa makusudi kutimiza ndoa

Kama baada ya kufunga ndoa mmoja wa wafunga ndoa atakataa kuitimiliza ndoa anayekataliwa ana haki ya kuiomba mahakama kuvunja ndoa
hiyo.

Maingiliano yanayotambulika kisheria ni yale yanayofanyika siku ya ndoa na kuendelea na siyo kabla ya ndoa.

Kukataa kuitimia ndoa kunakuwa
sababu ya kubatilisha ndoa ikiwa mwenye kukataa hana sababu yoyote ya msingi na mwenye kukataliwa ametumia kila mbinu kumshawishi aliyekataa lakini
ikashindikana kufanya tendo la ndoa.

3. Mimba ya mwanamme mwengine

Kama wakati wa kufunga ndoa mke atathibitika ana mimba aliyopata kwa mwanamme mwingine, mume
anaweza kuiomba mahakama ivunje ndoa hiyo.

Kama itathibitika kuwa mume alijua hivyo hali wakati wa kufunga ndoa, lalamiko lake halitasikilizwa.

4. Wazimu au kifafa cha kipindi

Mmoja wa wafunga ndoa kama ana wazimu au kifafa cha kurudia rudia na mwenzake alikuwa hajui hilo hali wakati wa kufunga ndoa, atakuwa na haki ya kuiomba mahakama kuivunja ndoa hiyo.

Ieleweke kuwa ugonjwa ni lazima uwe unarudia rudia na siyo mtu awe aliugua na akapona.

5. Kushindwa kutimiza ndoa

Kama mmoja wa wafunga ndoa atashindwa kuitimiliza ndoa basi ndoa hiyo inaweza kubatilishwa.

Kwa mwanamme kama anashindwa kuitimiliza ndoa kwa sababu ya kukosa nguvu za kiume basi ana haki ya
kuiomba mahakama kuibatilisha ndoa.

Ili kukosa nguvu za kiume kuwe sababu ya kubatilisha ndoa ni lazima ithibitike kuwa hali hiyo ilitokea kabla au wakati
wa kufunga ndoa na siyo baada ya kufunga ndoa wakati kitendo cha kuitimiliza ndoa kilishafanyika.

Ili ndoa iweze kubatilika ni lazima kukosa nguvu huko kuthibitishwe na daktari kuwa hakuponi au kunapona lakini mwanamme hataki matibabu.

Mwanamke anaweza kuwa na maumbile ambayo yanaweza kufanya ndoa ishindwe kutimilizika.

Ikithibitika hali hiyo lakini mwanamke hataki tiba mwanamme
anaweza kuomba mahakamani ndoa kubatilishwa.

Ili mahakama iweze kusikiliza shauri la kuomba kubatilisha ndoa ni lazima shauri hilo lipelekwe haraka.

Kama shauri litakwenda mahakamani baada ya mwaka mmoja tangu tarehe ya ndoa Mahakama haitalipokea.

Pia ni lazima ithibitike kuwa mlalamikaji
alikuwa hajui kasoro hiyo wakati wa kufunga ndoa na baada ya kuigundua kasoro hiyo hajawahi kuingiliana
na mwenzie mwenye kasoro hiyo.

Ndoa batili huvunjwa na mahakama pekee baada ya kupokea malalamiko toka kwa mmoja wa wanandoa.

Kama hakutakuwa na malalamiko yatakayopelekwa mahakamani na anayedhurika na kasoro hizo, ndoa
hiyo itadumu ama labda mmoja afariki au kama kuna talaka itatolewa na mahakama.

Watu waliooana wana uhuru wa kugeuza ndoa yao kuwa ya mke mmoja au ya wake wengi pale wanapofuata taratibu zinazokubalika kisheria.

Kabla ya kufanya uamuzi wa kugeuza ndoa ni hapanabudi wanandoa wakubaliane kuhusu uamuzi huo.

Kitendo cha kugeuza ndoa hufanywa mbele ya Hakimu wa Wilaya au Jaji ambapo wanandoa watatoa tamko la maandishi lenye saini zao na Hakimu au Jaji
aliyeshuhudia naye hutia sahihi yake.

Katika kugeuza ndoa, ndoa ya kiserikali ya kienyeji au ya Kiislamu inaweza kugeuzwa kuwa ya mke mmoja kama kabla ya kugeuza hizi zinaweza kugeuzwa
kuwa ya wake wengi.

Ikumbukwe kuwa kubadilisha dini pekee hakubadilishi hadhi ya ndoa.

Vilevile ndoa ya kikristo haiweza
kugeuzwa kuwa ya wake wengi wala ndoa ya wake wengi inayodumu kuwa ya mke mmoja.
Talaka na taratibu zake

Talaka ni ruhusa au amri ya mahakama ya kisheria ambayo mume au mke hupewa wakati anapomwacha mwenzake.

Chombo chenye mamlaka ya kutoa talaka ni
mahakama tu.

Mahakama hiyo itatoa talaka kwa
ndoa ambayo imedumu kwa muda wa miaka miwili au zaidi.

Mahakama inaweza kutoa talaka kwa ndoa
ambayo haijafikisha muda huo endapo mlalalmikaji atatoa sababu za msingi mahakamani.

Kutengana

Kutengana si talaka,kutengana maana yake ni hali ambayo mke na mume hukaa mbalimbali.

Kukaa mbalimbali au kutengana kwaweza kuwa kwa mapatano kati ya wanandoa hao au kutengana kwaweza kuwa kwa amri ya mahakama.

Mahakama itatoa amri hiyo endapo mmoja wao atapeleka maombi mahakamani.

Faida ya kutengana wote au mmoja wao waweza au aweza kutambua makosa na baadaye kukata shauri kurudiana au kuishi tena.

Kutengana kwa mapatano, ni kutengana kwa hiari yao wenyewe bila shuruti, mapatano hayo yaweza kuwa ya maandishi au ya mdomo.

Mambo kadha yaweza kuzingatiwa wakati wa makubaliano kama; heshima kwa kila mmoja, matumizi au matunzo,watoto kama wapo watakaa na nani, mali ya pamoja je itatunzwa namna gani na kutobughudhiana.

Kutengana kwa amri ya mahakama, hii ni hali ya mume na mke kutengana kwa amri ya mahakama na mahakama imeridhika kuwa ndoa imevunjika.

Ushahidi wa kuwa ndoa imevunjika ni ushahidi ambao unaweza kutolewa mbele ya mahakama kunapokuwepo na maombi au shauri la talaka.

Sababu za kutoa talaka mahakamani

Kabla ya kupeleka shauri au maombi mahakamani ya talaka, mwanandoa husika hana budi kufuata au kuzingatia hatua zifuatazo;

a) kufungua au kupeleka malalamiko
kwenye Baraza la Usuluhishi la Ndoa kwa mfano Bakwata, kanisani,Ustawi wa Jamii au Baraza la Kata.

b) Baraza litasikiliza, na endapo litashindwa mapatano au muafaka kati ya wanandoa hao, basi baraza litatoa cheti ambacho kitaeleza kuwa limeshindwa kusuluhisha mgogoro wa ndoa na kuomba
mahakama kuendelea kutoa talaka.

c) Baada ya mwanadoa mmoja kupata cheti
hicho basi atatakiwa atayarishe madai ya
talaka akionyesha kuwa kulikuwa na ;-
ndoa halali, kuna mgogoro kati yao,
watoto, mali walizochuma wakati wa ndoa yao,.

Muombaji huyo ataiomba mahakama hiyo itoe amri ya talaka, mgawanyo wa mali zilizochumwa kwa nguvu za amoja,mamlaka ya kukaa na watoto na matunzo yao, gharama za madai au shauri.

Ili mahakama itoe talaka sababu kadha huangaliwa na mahakama.

Sababu hizo ni mambo ambayo
yatakayofanya ndoa ionekane kuwa imevunjika kiasi kwamba haiwezi kurekebishika tena, mambo hayo ni
kama ifuatavyo;

a) Ugoni; hii ni zinaa ambayo hufanywa na
mwanamme na mwanamke ambao hawajaoana.

Hii hutokea ambapo mwanamme ana mke wake au mwanamke ana mume wake, hivyo mmoja wapo anamwacha mke/mume na kufanya zinaa na mtu mwingine.

b) Ukatili; ukatili ni kuumiza nafsi nyingine, kuharibu mwili au kuwa na hofu ya kuumizwa.
c) Kulawiti; kulawiti ni kumwingilia mtu kinyume na maumbile,

d) Kichaa; ni kutokuwa na akili timamu, na hali hii lazima iwe imethibitishwa na madaktari bingwa wa akili.

e) Kuzembea wajibu kwa makusudi; haya ni majukumu ya mume, majukumu hayo ni kama haya; kumtunza mke kwa kumpa chakula, malazi na mavazi.

f) Uasi; ni hali ya mke au mume kuhama nyumba ya ndoa na kwenda kuishi mahala pengine bila sababu yoyote ya msingi,

g) Kutengana; kukaa mbalimbali kwa mume na mke kwa muda wa miaka isiyo pungua mitatu, kutengana kwao ni sababu tosha ya talaka.

h) Dhana ya kifo; hii ni hali ambayo mmoja wa wana ndoa amekufa, na hii hutokea iwapo mojawapo hataonekana / ametoroka kwa muda mrefu, kama miaka 5, hapo mahakama hutoa tangazo kuwa
fulani amekufa.

i) Kifungo; hii ni hali ambayo mume au mke ametenda kosa la jinai na ametiwa hatiani na mahakama imemfunga miaka 5 au maisha basi mahakama
inaweza kutoa talaka kwa mwombaji.

j) Tofauti za imani za kidini, endapo mwanandoa mmoja atabadili dini basi ni sababu tosha ya kuomba
mahakama ivunje ndoa na kutoa talaka.

Haki na wajibu katika ndoa

Baada ya kufunga ndoa na ikaonekana haina kasoro yoyote, mke ana haki mbalimbali kisheria anazostahili
kuzipata.

Haki hizi ni kama; Matunzo; mke au wake wana haki ya kutunzwa na mume wao kwa kuwapatia mahitaji muhimu kama
chakula, malazi, mavazi, matibabu, n.k kulingana na uwezo alionao mume.

-Kumiliki mali; mke ana haki ya kumiliki mali aliyoipata kabla na baada ya ndoa kama aliipata kwa fedha yake mwenyewe.

-Mke ana haki ya kuingia mikataba, kushitaki na kushitakiwa.
- Makubaliano yaweza kufanywa na wanandoa hiyo jinsi ya kumiliki
mali iliyopatikana kabla ya ndoa yao jinsi gani waimiliki. Kwa mali iliyopatikana wakati wa ndoa, mali hiyo ni mali ya wanandoa wote, kwa sababu
imepatikana kwa mchango wa nguvu za pamoja.

Hii haijalishi kuwa mmoja wa wanandoa (mke) hachangii pesa tasilimu au anakaa nyumbani na kufanya shughuli za nyumbani tu.

Kufanya shughuli za nyumbani ni mchango mkubwa na ameokoa fedha
nyingi.

Umiliki wa mali kwa wanandoa haujalishi
kuwa mmoja wapo amemiliki mali hiyo kwa jina lake au la.

Haki ya kukopa kwa dhamana ya mume; jukumu la kutunza mke na watoto ni jukumu la mume au
baba.

Kwa msingi huo, endapo baba amesafiri,
au ametoroka na baadaye matatizo yakajitokeza yanayohitaji fedha, basi mke ana haki ya kukopa fedha kwa jina la mume au kuweka rehani mali yamumewe.

- Haki ya kuishi katika nyumba ya ndoa;
Nyumba ya ndoa ni nyumba ambayo mke na mume wanaishi wakati wa ndoa. Hata kama wanandoa wana nyumba nyingi, basi wanayoishi au kutumia
kama makazi ndiyo nyumba ya wanandoa.

Nyumba hii haiwezi kuuzwa, kuweka rehani au kuchukuliwa na mtu mwingine kama zawadi bila ya makubaliano ya wanandoa wote.(bila ridhaa ya wanandoa).

Mwanandoa ana haki ya kuishi kwenye nyumba hiyo mpaka amri ya mahakama ya kuvunja ndoa, au kutengana itakapotolewa.

Talaka kisheria
Neno talaka linaweza kuwa mojawapo ya maneno yaliyozoeleka midomoni au masikioni mwa watu wengi katika ulimwengu wa sasa.
Kwa lugha nyepesi, talaka ni kitendo cha wanandoa kuachana na mahusiano ya kindoa yaliyokuwa baina yao.
Lakini kisheria, ingawa maana ya talaka inaakisiwa na maana hii ya Kiswahili, lakini katika maana ya sheria kuna mambo mengine zaidi ya kuzingatia.
Tafsiri ya sheria ya ndoa ya Tanzania, sura ya 29 ya marekebisho ya sheria ya mwaka 2002, talaka ni kitendo cha mahakama yenye mamlaka katika shauri linalohusika, kutoa tamko la kuivunja ndoa iliyokuwapo,kwa sababu mbalimbali.
Hivyo, tukiangalia kwa mtazamo wa kihistoria, ndoa kwa mujibu wa sheria ya Kiingereza (common law) ambayo imeakisiwa sana na sheria ya ndoa ya Tanzania, ilikuwa haitambui sababu ya aina yeyote katika kuivunja ndoa kwa msingi wa talaka.
Lakini baada ya miaka mingi kupita, sheria ya talaka ilianza kutumika nchini Uingereza baada ya sababu kadhaa za kisheria za kuvunja ndoa kwa talaka kuanzishwa.
Sheria ya Talaka (The Divorce Act) ya mwaka 1969 ilianzishwa nchini Uingereza kufuatia ripoti ya askofu Kent wa nchini humo.
Mwaka mmoja baadaye yaani mwaka 1969 serikali ya Tanzania kupitia tamko la serikali (Government Notice) namba 1 ya mwaka huo, iliyojulikana kama White Paper ilichukua msimamo na mtazamo huu wa sheria ya Kiingereza juu ya talaka.
Hadi mwaka 1971 tulipochukua msimamo huu wa sheria ya Uingereza juu ya talaka, mabadiliko makubwa ya kimsingi ya sheria juu ya talaka yalitokea katika sheria yetu hapa nchini nayo ni pamoja na kuwa na sababu moja tu inayoweza kuifanya ndoa kuvunjwa na mahakama kwa tamko la talaka, sababu hiyo ni kuwa mahakama itakapothibitisha kwamba ndoa hiyo imevunjika kabisa na haiwezi kurekebishika kutokana na kasoro zisizo weza kurekebishika.
Hivyo, sheria ya Tanzania katika hili nayo ikachukua sababu moja inayoweza kuifanya ndoa kuvunjwa na talaka.
Hata hivyo, wakati tunaangalia sheria hii, tunatakiwa kujua kwamba sababu moja ya kuivunja ndoa kwa talaka ipo Tanzania bara pekee.
Baadhi ya watu wanadhani sababu za kuvunja ndoa ni zile zinazoelezewa na sheria hii kama hali au mazingira ya kuthibitisha kwamba ndoa hiyo ina tofauti zisizorekebishika.
Sababu hizo ni pamoja na uzinifu nje ya ndoa, ukatili pamoja na kumkimbia/kumtelekeza mwanandoa mwezako.
Uzinifu ni mojawapo ya sababu zinazoipa mahakama mamlaka kisheria kuivunja ndoa yoyote.
Hata hivyo, unatakiwa kujua uzinifu una maana nyingi kutegemea na eneo husika.
Kimsingi uzinifu ni kitendo cha mwanandoa mmoja kufanya ngono nje ya mahusiano yake ya ndoa iliyo halalishwa.
Hapa katika kuondokana na wasiawasi wa kuweza kushindwa kuthibitisha uzinifu, sheria imetoa dhana kwamba pale tu itakapokutwa mume na mke wamelala pamoja na wako watupu, basi dhana hapa ni kwamba wametoka au wanataka kufanya ngono.
Dhana hii kama ilivyoanzishwa na mahakama katika shauri la Denise dhidi ya Denise, Jaji Single anasisitiza kwamba dhana hii ni ngumu kuipinga isipokuwa kama itathibitika kwamba mwanaume aliyekutwa ni hanithi au mwanamke huyo ni bikira.
Na uthibitisho wa uzinifu nje ya ndoa ni kama uthibitisho wa katika kesi ya jinai ambapo anayelalamika anatakiwa kuithibitishia mahakama pasi na shaka kwamba uzinifu umetokea.
Kwa upande wa Uingereza, kama itathibitika kwamba kulikuwa na uzinifu na kwamba mtoto alizaliwa nje ya ndoa, pia atahesabika ni mtoto haramu na hivyo kukosa haki zake zote kwa mzazi wake wa pili.
Hata hivyo, mara nyingi uzinifu unaweza kuthibitishwa na ushahidi wa mazingira kama vile mmoja wa wanandoa kuwa na ugonjwa wa zinaa na kadhalika.
Kifungu cha 170(2) cha sheria ya ndoa ya Tanzania, kinatoa maelekezo juu ya ushahidi wa aina hii.
Hata hivyo, uzinifu si lazima uwe sababu ya mahakama kutoa talaka. Mahakama kwa kuzingatia mazingira ya kesi husika inaweza kuamuru mtu aliyefanya uzinifu na mmoja wa wanandoa kumlipa fidia muathirika wa uzinifu huo.
Ukatili pia ni sababu mojawapo ya sababu zinazoweza kuithibitishia mahakama kwamba ndoa hii ina kasoro zisizoweza kurekebishika.

Kuharamisha, kubatilisha ndoa katika Sheria ya Ndoa

NENO kuharamisha ni la kawaida katika lugha ya Kiswahili ambalo linalotokana na neno ‘haramu’ likimaanisha kitu kisichofaa, kwa maana iliyo nyepesi.
Aidha kuharamisha ndoa kisheria ni kitendo cha mahakama kutoa tamko kwamba ndoa ambayo iliyodhaniwa kuwa imefungwa haikufungwa wala haikuwapo.
Hapa tunatakiwa tujue mantiki ya kitendo hiki ni kuharamisha (nullify) ndoa ambayo ilidhaniwa ni halali wakati wa kufungwa, lakini kumbe katika jicho la sheria ndoa hiyo “haipo na wala haikuwahi kuwapo”.
Hii siyo talaka kama ambavyo watu wengine wanaweza kufikiri. Somo la talaka tutalizungumzia baadae katika makala nyingine.
Kama ambavyo nadharia nyingi za sheria zetu zimetoka katika sheria za mahakama za nchini Uingereza, yaani Common law, nadharia hii imetoka huko huko, wakati wa mageuzi baada ya kuanguka kwa dola ya utawala wa kifalme wa Kirumi huko Ulaya.
Wakati wa utawala wa kirumi huko Ulaya, sheria za Kanisa Katoliki zilikuwa zinatumika kwa kiwango kikubwa, imani na mafundisho ya Kanisa Katoliki ndoa ni Sakramenti iliyoanzishwa na Mwenyezi Mungu.
Hii ilikuwa na maana kuwa ndoa ni takatifu hivyo talaka ni kitu ambacho hakitambuliki katika sheria za Kanisa, kusisitiza maneno ya bwana Yesu katika Injili ya Marko 10:7-8 kwamba mwanaume na mwanamke wakiungana wanakuwa mwili mmoja na kwamba alichokiunganisha Mungu mwanadamu yeyote asikitenganishe.
Kwa mantiki hiyo, njia pekee ya watu kutoka ndani ya ndoa wakati huo ilikuwa ni kuiharamisha na si talaka, kwani ilikuwa haitambuliki kama tulivyoona hapo awali. Baada ya kuanguka kwa dola ya Rumi huko Ulaya, tawala za kifalme zikawa maarufu sehemu nyingi huko Ulaya na kusababisha sheria za kanisa (Canon law) kupotea na kwa upande wa Uingereza, sheria za mahakama za Uingereza yaani Common law zikashika kasi.
Hivyo basi athari ya sheria hizi za mahakama za Uingereza ilikuwa ni pamoja na kuleta mafundisho mengine ikiwemo kuanzisha upya talaka.
Kwa Tanzania, vifungu vya 39 na 49 vya Sheria ya Ndoa, 1971; vinaelezea njia mbili kuu za kuharamisha ndoa. Njia hizi ni zile ambazo ikithibitika mahakamani, basi mahakama itatoa tamko la kuharamisha ndoa.
Njia hizi ni pamoja na ndoa haramu (void marriage) na ndoa isiyo haramu lakini pia si halali kwa kuwa imekosa mahitaji kadhaa ya kisheria yaani ndoa batili ( voidable marriage).
Kwa ndoa haramu, hii ni ndoa ambayo tangu mwanzo ilikuwa ni haramu katika jicho la sheria; wakati aina ya pili ya ndoa isiyo haramu ila imekosa kutimiza masharti kadhaa ya kisheria kuifanya iwe halali na hivyo kuifanya batili.
Kwa mfano kwa mwanamme asieweza kufanya tendo la ndoa na mkewe, ndoa yake itakuwa batili kama mkewe atakwenda mahakamani kuomba ndoa yake ibatilishwe kwa kuwa mumewe hawezi kufanya tendo hilo ambalo ni hitaji la kisheria ili ndoa iwe halali; lakini kama mwanamke huyo atavumilia hali hiyo, ndoa yao itakuwa ni halali.
Hivyo basi, kwa mujibu wa kifungu cha 39 na 49 vya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, kuna sababu mbalimbali ambazo zinaweza kusababisha ndoa isiwe halali, kwa sababu hizo mume au mke anaweza kuomba mahakama itoe tamko la kubatilisha ndoa yake. Sababu hizi ni kama zifuatavyo;
Kwanza, kwa wanandoa kushindwa kufanya tendo la ndoa wakati wameoana, kwa mujibu wa kifungu cha 39(e) cha Sheria hii, pindi mwanandoa yeyote (mwanamme au mwanamke) wakati wameshafunga ndoa na mwenzake atashindwa kufanya tendo la ndoa hiyo itakuwa sababu kwa mmojawapo kuomba tamko la kubatilisha ndoa hiyo.
Huu pia ni uamuzi uliotolewa katika shauri la Dralge dhidi ya Dralge , (1947)1 All.ER 29), la nchini Uingereza,ambapo mahakama ilitafsiri kimantiki kwamba tendo la ndoa ndilo haswa linalomaanishwa katika kile ambacho kifungu cha 39 cha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inamaanisha.
Ndoa kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 Ndoa kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 Reviewed by WANGOFIRA on 09:14:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.