MFUMO WA ELIMU YETU NDIYO CHANZO CHA WAHIMU KUTOKIDHI VIGEZO VYA SOKO LA AJIRA
Na,
BARAKA NGOFIRA
0763580901,
0716216249
Tanzania
ni moja ya nchi ambayo asilimia kubwa ya vijana wanaohitamu masomo yao kutoka
vyuo mbalimbali vya elimu ya juu, na vile vya elimu ya kati ni wengi ukilinganisha
na nafasi za kupata ajira katika fani walizozisomea. Na wengi kutunukiwa vyeti
vya stashada na wengine shahada za juu, lakini pamoja na yote hao mianya ya wao
kupata ajira imekuwa ni migumu ikilinganishwa na miaka kumi au kumi na mitano
iliyopita.
Pamoja
na jitihada mbalimbali zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na wadau wa elimu
kwa kushiriana na serikali pamoja na mashirika binafsi lakini ndivyo tatizo
linazidi kuwa kubwa. Najiuliza maswali mengi ambayo yanayonifanya niumwe kichwa
kila siku hasa pale ninapofikiria juu ya vijana wenzangu waliohitimu na
waliotunikiwa vyeti, stashada, na wale wa shahada mwaka huu na wengine
kunifanya nidondoshe machozi.
Wengi
wakiwa wanafurahi kuvaa majoho na kofia siku ya mahafali yao na kusahau kesho
yao itakuwaje baada ya kuvua majoho na kuachana na mitihani ya darasani, huku
mtaa na msoto wa ajira ukiwaita na kuwangojea kwa hamu kubwa baada tu ya
kuachana na maisha ya vyuoni.
Na pengine huwa natoa machozi kwa kuona
tangazo la kazi likihitaji mtu mmoja, lakini maombi zaidi ya elfu mbili
yakitumwa ili mmoja wao achaguliwe. Na chakusikitisha sana huenda hata hao 2000
na zaidi asipatikane hata mmoja anayehitajika. Hapo ndipo najawa na maswali
yafanyayo kichwa changu kiendelee kuniuma.
Sijasahau
zile nafasi chache za kazi zilizotangazwa na uhamiaji zizofanya watu wakafanye
mtihani wa kazi uwanja wa taifa, na kuudhihilishia ulimwengu kuwa vijana wengi
wa kitanzania hawana ajira. Pia nahisi ni tukio ambalo liliandikwa kwenye
vitabu vya kumbukumbu maarufu kama encyopedia kwani ilikuwa inauma na kusikitisha
sana kuona vijana wengi zaidi ya elfu kumi wanagombania nafasi zisizozidi 100
za ajira.
Inaniuma
sana hasa kwa hawa waliohitimu mwaka huu na wao wanaenda kuongeza idadi tena ya
wale waliosota mtaani kwa miaka zaidi ya kumi, huku bahasha zao za kaki
zilizochakaa na CV zao kuchafuka na wengine viatu vikiwa vimewaisha soli kwa
sababu tu ya kutafuta kazi katika ofisi mbalimbali za kiuserikali na zile za binafsi.
Kinachonishangaza
pia ni kuona wengine wanapata kazi tena kwenye makampuni makubwa ya kitaifa na
kimataifa huku wakiwa bado shule. Hapa napo najiuliza maswali mengine tena
mengi tu kuhusu wao, kuwa wanatumia njia gani kupata kazi hizo au kwa nin I wao
wanaosoma wapate kazi mapema huku wengine wakihangaika kutafuta kazi kwa zaidi
ya miaka mitano na wengine kukata tama na kuweka vyeti chini na kutafuta njia
ya pili au kujiingiza kwenye vitendo viovu na uporaji wa kutumia silaha, na
wengine kuamua kujiingiza kwenye uuzaji wa madwa ya kulevya na ujangiri wa
wanyamapori wetu pasipo hata kujali athari zake.
Siishii
hapo tu huwa naenda mbali zaidi kwenda kuwauliza baadhi ya wakurugenzi ambao
utangaza nafasi za kazi na vijana wengi wa kitanzania kujitokeza na kazi
wakakosa kwa kutotimiza vigezo. Huwa wananipa majibu ambayo kwa namna moja ama
nyingine nakubaliana nayo lakini mengine inanibidi nikubaliane nao kwa shingo upande.
Mmoja
wapo wa waajiri wa kampuni kubwa tu ya hapa nchini aliniaambia kuwa maombi
mengi ya kazi hutumwa ofisini kwake tena na watu waliopata ufauli mkubwa katika
vyuo vya walivyosoma, lakini wanapoajiriwa kiwango cha ufanyaji kazi wake na
ufaulu alioupata na kutunukiwa na chuo chake ni vitu viwili tofauti.
Kwani
utendaji kazi wake ni hafifu mno ukilinganisha na kiwango chake cha elimu na
ufaulu ambao yeye alinambia walimu wake ni kama walimzawadia au kuukadilia,
aliniambia vijana wengi wa kitanzania hususan wanaohitimu vyuo vikuu kwa sasa ni
aibu hata kusema kazi wazifanyazo ofisini ukilinganishwa na kiwango cha elimu
na ufaulu wao.
Akanipa
mfano kuwa mwezi novemba aliitwa kwenda kusimamia mahojiano ya kutafuta watu 3
kutoka Afrika mashariki ili wakafanye kazi katika Benki ya Dunia. Lakini pamoja
na kupata maombi zaidi ya 700 kutoka Tanzania na yeye mwenyewe kukaa chini na
kupoitia ombi moja baada ya jingine, lakini cha kusikitisha alikosekana kijana
hata mmoja wa kitanzania ambaye alikitimiza vigezo vya kufanya kazi katika
shirika hilo la umoja wa kimataifa.
Nilijiuliza
sana shida iko wapi na kwa nini iwe kwa watanzania tu, mbona kwa wenzetu
wakenya, wanyarwanda, warundi na waganda wanafanya kazi tena kubwa tu kwenye
mashirika binafsi yanayomilikiwa na watanzania wenyewe. Hapo ndo nikapata jibu
kubwa kuna shida kwenye mifumo yetu ya elimu aiwaandai vijana wa kitanzania
kuingia sokoni mara tu wanapohitimu masomo yao
hasa ya juu.
Ukilinganishwa
na miaka ya 1990 kurudi nyuma mfumo wa elimu yetu ulikuwa mzuri na masomo
yalilenga kumwandaa kijana wa kitanzania kuajirika na kujiajiri mwenyewe na si
kutegemea ajira ya serikali au kutoka kwenye sekta binafsi.
Nilipomuuliza
baba yangu kuwa kwa nini kipindi chao walikuwa hawasoti mtaani kama sasa
alinambia kipindi chao, walikuwa na mumo ambao ulikuwa unawafanya wao wajiajiri
na si kutengemea ajira na ndiyo maana walijituma na wengi wao kugombaniwa
wakiwa bado masomoni ,tofauti na leo wasomi wanavyogombania kazi.
Hapo
ndipo nilipokumbuka ile falsafa ya elimu ya kujitegemea iliyoanzishwa na Hayati
Baba wa Taifa mwalimu JK Nyerere baada ya azimio la Arusha ambapo elimu hii
ilimjenga mtanzania aliyekuwa anasoma kwa kipindi hicho aweze kuwa wa uwanja
mkubwa wa kujiajiri na sio kuajiriwa hapo ndipo masomo kama ya kilimo, ufugaji,
muziki, sanaa na mengine mengi ya ufundi kama stadi za kazi yalianzishwa ili tu
kumjenga mtoto wa kitanzania aweze kijiajiri na si kutegemea ajira.
Chakunishangaza
mpaka sasa maadui hawa bado hawajaisha kwani pamoja na watanzania wengi kwa
sasa kujidai kuwa sisi si wajinga lakini bado hatujaweza kutengeneza kitu
ambacho tunaweza kujivunia tuendapo popote pale ulimwenguni. Ebu jiulize wembe
tunaletewa na wachina, sabuni, chumvi, viberiti na vinginevyo vingi tunaletewa
na wakenya, nguo tunaagiza nje sasa
welevu wetu huko wapi? Au tunajivunia nini, Tanzanite, Dhahabu au Almasi ambazo
kila mwaka Afrika Kusini na Kenya wanapewa tuzo na zawadi kubwa na mataifa
makubwa duniani kwa uuzaji wa maduni hayo nje. Huku dunia yote inatambua kuwa
Tanzanite inapatikana Tanzania tu.
Tusiongelee
hayo kwa leo lakini tuangalie sera yetu ya elimu iko wapi? Nawaulizeni nyie
wakubwa mlioko huko juu ambao wengine wenu mnatutia aibu kama nchi mnashindwa
kuelewa hata historia ya nchi yetu, na kusema vitu ambavyo ni aibu tupu kwa
nchi yetu. Na ndiyo maana hata sishangai
kumwona anayejiita msomi wa chuo kikuu ukimuuliza kirefu cha TANU ni nini anajibu
madudu ambayo hata hayapo.
Tatizo
ni mfumo wetu wa elimu na si vinginevyo, inamjenga kijana wa kitanzania
kutegemea kazi za ofisini. pia kutokana na utandawazi pasipo hata kujiuliza
mara mbilimbili juu ya utoaji wa elimu ya juu na ya kati kwa Kuruhusu umilikaji
wa vyuo vingi ambavyo kiukweli vingi vikiwa havina hata sifa ya kutoa hata
elimu ya sekondari na kuongeza aibu kwa taifa,kwa kuwa na wasomi wengi
wasioweza hata kutengeneza hata kiberiti au kalamu.
Huku wakitangaza matangazo yanayovutia wateja
wao na kuhakikishiwa ajira za uhakika mara tu wamalizapo elimu katika vyuo
hivyo. Na wanafunzi pasipo hata kutazama na kufikri kwa kina tangazo ilo
lililojaa ushawishi mkubwa na wao kujirundika na kulipa ada kubwa na mwisho wa
siku kumaliza na kazi kukosa na kuongeza idadi ya wale tegemezi wa ajira.
Nimalize
kwa kuwaomba wadau wa elimu,walimu, wizara ya elimu na wakufunzi wa elimu kutengeneza falsafa na motto wa elimu ya
kitanzania ili tuendapo popote pale nasi tuseme falsafa ya elimu ya mtanzania
ni hii. Na si kubaki kujing’atang’ata pale wageni watuulizapo sera na falsafa
ya elimu ya Tanzania ni ipi tupate cha kujibu pasipo hata kufikiri sana.
Kwa leo naweka kalamu yangu chini kuashiria
nimemaliza na kuwaachia wahusika mtafakari ili elimu itakayotolewa iweze
kumfanya kijana wa kitanzania kuajirika popote pale kama walivyo wenzetu
Wakenya, Warundi,Warwanda na mataifa mengine ya kiafrika na duniani kwa ujumla.
Makala
haya yameandikwa na mwanafunzi wa mwaka wa pili anayesomea fani ya Mawasiliano kwa
Umma katika Shule Kuu ya Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo kikuu cha Dar
es salaam. Anapatikana kwa mawasiliano ya 0763580901, 0716216249 au e-mail
barakangofira@gmail.com.
MFUMO WA ELIMU YETU NDIYO CHANZO CHA WAHIMU KUTOKIDHI VIGEZO VYA SOKO LA AJIRA
Reviewed by WANGOFIRA
on
01:52:00
Rating:
No comments: