KARIBU PROF. NDARICHAKO TULIKUNGOJA KWA HAMU KUBWA, UINUE ELIMU YETU.



Image result for dr joyce ndalichako
 waziri wa Elimu, sayansi, teknolojia na mafunzo ya ufundi, Dr. Joyce Ndarichako

Na, BARAKA NGOFIRA

0763580901, 0716216249

Ni ukweli usiofichika kuwa elimu yetu ilikuwa imepoteza dira na mwelekeo, watu wengi walikuwa wameka tamaa na namna mfumo wa elimu yetu ulivyokuwa unaendeshwa na baadhi ya watendaji wengi waliopita kwenye wizara hii pasipo kujali  unyeti wake. Kwa kusahau kuwa pasipo msingi wa elimu bora ni sawa na utumwa na ujinga ambao uasababisha baadhi ya watu kushindwa kujua wapi watokapo na wapi waendapo.

Kwanza nikupongeze sana maana nilitamani sana siku moja uje uwe mkuu kwenye wizara hii nyeti ambayo ni kiwanda na injini ya nchi ya kuzalisha na kupika wasomi na wataalam katika fani mbalimbali. Hii pia ilikuwa ni hamu kubwa wa wanaopenda maendeleo ya sekta ya elimu hapa nchini.

Pia, Nimpongeze Rais Dk. Magufuli kwa kukuona na kukuchagua uwe jembe letu kwenye wizara hii nyeti ya elimu, naamini wewe ni jembe na hilo hakuna anayebisha, na kama yupo basi atakuwa na matatizo yake binafsi katika lile ulilokuwa unalisimamia kabla haujapewa wadhifa huu mkubwa wa kutekeleza kauli mbiu ya hapa kazi tu, ambayo naamini ni kazi kwelikweli.

Nafahamu ni wizara kubwa kwako lakini naamini unaweza kwani wadau wa elimu tunakuombea ili upambane vilivyo ili uwashinde wale wanaotaka elimu yetu isiwe na thamani, wasomi wengi kuzurura mitaani na vyeti vyao huku wakitafuta ajira pasipo mafanikio. Na kubezwa na waajiri kuwa  hawana sifa na hawajui lolote na vyeti wamegawiwa tu. Naamini litapungua au kuisha kabisa.

Nakumbuka utendaji kazi wako uliotukuka ulipokuwa Baraza la Mitihani, umeandika historia kama kiongozi shupavu tena mwanamama ambapo kila apendaye maendeleo ya elimu atosita kukuita jasiri, kwa hili unastahili pongezi nyingi za dhati kwa kutokubali kuyumbishwa na wasioitakia mema nchi yetu, na kusimama na msimamo wako kwa kusimamia kile ulichokiamini kinajenga na kuimairisha elimu yetu.

Na sasa umekuwa waziri baada ya kuteuliwa na Dr. Magufuli, kwa niaba ya wengine wote niseme karibu sana kwenye wizara ya elimu. Lakini ni imani yangu kuwa unayajua mapungufu yaliyopo kwenye wizara uliyokabithiwa. Mapungufu na matatizo yamekuwa ni ya muda mrefu ambayo mengine kwa kiasi fulani yamesababishwa na viongozi wetu lakini mengine ni masuala tu ya muda na fedha ndio chanzo kikubwa cha matatizo hayo.

Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambayo imekuwa ikitolewa kiubaguzi kwa kuzingatia fani na masomo wasomayo wanafunzi imekuwa ni tatizo kubwa ambalo limesabibisha vijana wengi kukimbilia ualimu. Jambo ambalo limesababisha kuwa na idadi kubwa ya walimu ambao wamewageuza wanafunzi vitega uchumi vyao kwa kuwaongezea michango mingi na isiyo na maana, ni kwa sababu ndoto zao hazikuwa kuwa waalimu bali kitu kingine tofauti, lakini kwa sababu tu ya kuogopa kusota mtaani pila kusoma au kulima kwa sabababu ya kukosa mkopo ndiyo maana wameamua kukimbilia huko kwenye ualimu.

Siku hizi ualimu umekuwa dili la haraka na ambalo wanajifariji kuwa halikosi mteja maana shule ni nyingi na wanafunzi kila mwaka wanaongezeka. Hiyo ni hoja lakini jiulize kila mwaka wanaajiliwa waalimu wangapi kwenda kufundisha wanafunzi hawa?

Je ufaulu umeongezeka au umepungua ukiringanisha na miaka kumi ya nyuma? Msomaji wangu ukisha jiuliza maswali hayo njoo uwaone waalimu hawa nyumba waishizo je zina hadhi ya wao kuishi? Nyingine zimejazana vichuguu na mchwa ambao wameamua kuishi ili wakiacha karatasi za wanafunzi wawasaidie kutunza.

Jiulize tena ni dada zetu wangapi walikuwa wanashindwa kumaliza masomo yao ya msingi ama sekondari kwa sababu ya kupata ujauzito kwa miaka kumi au 20 iliyopita na ukiringanisha na leo ni wanafunzi wangapi wameshindwa kuhitimu masomo yao kwa sababu ya mimba walizopewa na walimu wao? Jibu unalo mwenyewe msomaji.

Sijui nielezeje, lakini kwa kifupi ni kuwa imewabidi wawe waalimu wasio na nidhamu na kuondokewa na hofu ya kazi kwa sababu tu iliwalazimu wakasomee ualimu kwa sababu ni kipaumbele cha wao kupata mkopo na ajira kwa urahisi. Ukiringanishwa na fani nyingine ambazo wengine wanazisoma.

Waswahili wanasema utavuna ulichopanda, na ndicho sasa tunakivuna kwenye elimu yetu kuanzia msingi hadi vyuo vikuu, ni aibu tena aibu ambayo tena ni aibu hata kuiongelea. Serikali ilianzisha mikakati mingi tu ili kuwafanya watu wengi wapende kusoma ualimu lakini kwa hili la kuwabagua wanafunzi kwenye mikopo iliharibu kabisa.

Japo kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kuwapata walimu wengi lakini walimu wasio na ualimu na maadili ya kazi, waliojika mavazi ya ualimu lakini roho zao wakiwa wajasiriamali wakubwa kwa kugeuza bidhaa ambazo ni michango isiyo na kichwa wala miguu kwa wanafunzi wawafundishao.

Utasikia mtoto wa darasa la kwanza akimuomba mzazi wake pesa kwa ajili ya masomo ya ziada ambayo hata mzazi mwenyewe unachanganyikiwa, na kujiuliza maswali kuwa huyu mtoto anasoma masomo yapi ya ziada ambayo tena ni lazima awapelekee walimu walewale wanaomfundisha? Ndo jibu unalipata kuwa ni miradi au wanafunzi wamegeuzwa vitega uchumi vya walimu.

Nina imani Dr. Ndarichako uozo kwenye elimu kamwe hautoufumbia macho kabisa, tunaitaji elimu yetu iimarike ili ituwezeshe kurimudu vyema soko la ajira kama vijana wa nchi nyingine zinazonguka wanavyotushinda sokoni. Kwako watanzania wana imani kubwa kuwa hautotuangusha maana wewe ni jembe haushindwi kitu, tunakuombea uweze kutumbua majipu na wale wajifanyao miungu watu huku wakivuruga na kutuharibia elimu yetu.

Zaidi ya yote Mungu akulinde na kukuongoza ili uwe na akili fikra na uwezo mkubwa wa kupambana na matatizo yaliopo kwenye wizara hii nyeti na muhimu kwenye ukuaji wa taifa letu. Hapa ni kazi tu na iwe kazi kweli kweli.

 Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki wizara ya elimu, sayansi na maendeleo ya jamii ili iweze kuwa mwangaza na taa ya wataanzania kututoa kwenye wimbi la umaskini, magonjwa na ujinga. Pia mbariki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. magufuli na watendaji wake katika kutuletea mabaadiliko ya kweli nchini kwetu.


Makala haya yameandikwa na Baraka Ngofira, mwanafunzi wa Mawasiliano kwa Umma (mwaka wa pili) katika shule kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM-SJMC). Anapatikana kwa mawasiliano ya 0763580901, 0716216249 au e mail ya  barakangofira@gmail.com.
KARIBU PROF. NDARICHAKO TULIKUNGOJA KWA HAMU KUBWA, UINUE ELIMU YETU.   KARIBU PROF. NDARICHAKO TULIKUNGOJA KWA HAMU KUBWA, UINUE ELIMU YETU. Reviewed by WANGOFIRA on 08:38:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.