NASEMA NAWE MAGUFULI

NASEMA NAWE RAIS  DR. JOHN MAGUFULI.

Na, Baraka Ngofira
0763580901, 0716216249

Baada ya pilikapilika nyingi za kampeni na harakati za uchaguzi mkuu uliofanyika hapo oktoba 25. Ambapo wananchi waliwachagua viongozi wao wanaowapenda kuanzia nafasi ya  udiwani, ubunge na hata Urais wa jamhuri wa muungano wa Tanzania.

Kwangu ulikuwa uchaguzi wa kwanza kushiriki kwa kupiga kura, kama katiba inavyoruhusu kuwa ni haki ya kila raia wa Tanzania kupiga kura mara tu afikishapo umri wa miaka 18 na pia awe na akili timamu.
Kama mtanzania nilitimiza jukumu na wajibu huo oktoba 25.

Uchaguzi wa mwaka huu  ulikuwa wa ushindani mkubwa hasa kwenye nafasi ya Urais na kwenye baadhi ya majimbo kama vile Moshi mjini, Kawe, Kibamba, Ilemela, Musoma mjini na mengineyo mengi, mpaka watu wengine wakaogopa na kuwa na hofu kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vyaweza kutokea  kama kwa wenzetu wakenya ilivyotokea 2007. Lakini kwa kilichofanyika Tanzania kimedhiilishia ulimwengu kuwa, nchi yetu ni kisiwa cha amani.
Na hivyo kufanya nchi yetu kuonekana ya kistaarabu, hapo wapo baadhi ya watu wanaotaka kutufanya tuvuruge amani tuliyo nayo.

Ushindani huu mkali ulikuwa kati ya chama tawala na vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi yaani UKAWA. Lakini mwisho ulifika na wananchi wakaamua na kuwachagua viongozi wao pasipo hata woga wowote. Kwani wao ndiyo wana dhamana hiyo kwa kutumia kadi zao za kupigia kura walizoziita kichinjio.

Niwapongeza wale wote waliochaguliwa katika uchaguzi huu, katika nafasi ya udiwani, ubunge na hata Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania. Nawapongeza kwa sababu ya uthubutu wenu mkubwa mliouonyesha kwa wananchi na kuwa ahidi mambo mbalimbali ambayo yaliwashawishi wananchi kuwachagua kwa kuwapa kura nyingi.

Naamini majukumu yenu mnayafahamu vyema na ndiyo maana mliomba nafasi hizo za uongozi kwa kipindi cha miaka mitano. Maana msipowatimizia wanachi wenu mlichoahidi ni bora mkimbie mapema na 2020 hata msithubutu kuomba ridhaa kwa wananchi maana mtaangukia pua, pia kumbukeni wengine mmepita kwa kuwazidi wapinzani wenu kura chache tu. Kwa hiyo mfahamu fika kuwa mna kazi kubwa ya kufanya kwa wananchi wenu kwani wamechoka kudanganywa.

Lakini nataka niseme nawe Rais wangu Dr. John Magufuli najua unayofuraha kubwa sana kupokea kijiti cha Urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kutoka kwa JK. Kwangu mimi naamini kuwa u hodari na kazi ya uliyoiomba unaikidhi na kuimudu vyema. Na
Kama ungekuwa ni mchezo wa miguu basi ungeitwa kiungo mkabaji.

Nasema nawe Magufuli Rais wangu na wa watanzania wote, tarehe 5 mwezi huu uliapishwa na kukabithiwa rasmi kijiti Cha kuongoza watanzania. Lakini leo imenibidi nitumie kalamu yangu kusema nawe.

Nafahamu unajua na uliyaishi maisha yetu ya watanzania wa kawaida  ambao kwao kula mlo mmoja na wengine wakipiga pasi ndefu ni kawaida sana. Na wala hata hawaoni shida kulala na kushinda njaa kwani matumbo yao yamezoea hivyo.

Nafahamu vyema ulizaliwa na kukulia katika familia ya mkulima na mfugaji mdogo ,ng'ombe, ulichunga, vibarua ulilima na hata chaki ulishika kipindi upo Sengerema sekondari ili tu kuhakikisha mkono unaenda kinywani.

Naamini nawe ulishindia kiporo na maziwa ulipokuwa ukienda kuchunga ng'ombe na hata kama ulipikiwa basi ni mlo mmoja tu ndo ulikula na kwenda zako kuchunga ng'ombe porini na hata mboga za majani kila siku ulikula, chai haukuijua maana pesa ya kununulia sukari na majani haikuwepo na hata ule uji wa mahindi, mtama, uwele na udaga uliunywa pasipo sukari.

Hayo ndiyo yalikuwa maisha yako hapo nyuma kabla ya kuwa mbunge na waziri na sasa Rais wa Tanzania ambaye kwa sasa unatembea na ving'ora vya kutosha na askari wakutosha wanaotukaliza  kwenye foleni na kuunguzwa na jua tukikungoja wewe Rais wetu upite ili ukatutimizie mahitaji yetu uliyotuahidi kipindi cha kampeni.

Nasema hayo si kwa kukusimanga, bali nakukumbusha tu maisha ya watanzania wa kawaida yalivyo Rais wangu mpendwa maana na wewe ni muumini mzuri wa dini pia u msikivu ndiyo maana niliwashawishi watu wakuchague bila kujali matusi niliyotukanwa katika kipindi chote cha kukupigia depe ili uende Magogoni mahali ambapo wapinzani wako wanapatamani na wanakuonea wivu na ndiyo maana walisusia sherehe za kukabithiwa cheti cha ushindi, na hata pale ulipoapishwa kwenye uwanja wa Uhuru walisusa. Si kwamba walikuwa hawataki la hasha lakini nahisi wanajiuliza ni kwa nini wewe uchaguliwe na wao kura zisitoshe huku kipindi chote cha kampeni walikuwa wanagharikisha watu na wengine kutoroka makazini kwenda kuwaona pia wengine iliwalazimu hata kufunga maduka yao kwenda tu kushuhudia waliokuwa wakimuita Rais anayesubiri kuapishwa lakini kura hakikumtosha.

Ikiwa unayajua hao leo nasema nawe pasipo woga wowote na wala hata pasipo kupepesa macho  kwani ni wajibu wangu kama mtanzania na mwanafunzi wa mawasiliano kwa umma. ulisoma katika shule zetu hizi za kayumba, unazijua vyema jinsi gani zilivyo, wadogo zetu na watoto wetu wanakaa chini si kwamba madawati hayapo au serikali imekoswa pesa za kutengeneza madawati la hasha! Ni kwa sababu wao ni wa maisha ya chini yaani kwa kingereza low class, hawana lolote wa usemi wowote kwa wakubwa na hata kama wakisema sauti zao hazisikiki kwani viongozi na wakurugenzi wameweka pamba masikioni, hawasikii hawaambiliki kwani wao ni wa hali ya juu yaani High class na wengine wakijiita eti wao ni VIP. Na ndiyo maana hawaoni haja ya kuwasikiliza na kutekeleza yake ambayo masikini hawa na watanzania hawa wa hali ya chini.

Si kwamba wao hawataki kusoma na kuishi katika mazingira mazuri kama zilivyo shule wanazoziita wenyewe eti SAINT bali wamekubaliana na hali kukaa chini kwao ni kawaida, michango inayozidi ada kwao ni ya kawaida, kutoa madawati kila mwaka kwao ni kawaida kabisa, si kwamba wanakaa kimya bali viongozi wameweka pamba masikioni hawasikii hawaambiliki kwani wao ni VIP.

Mikopo vyuoni wanafunzi kukosa ni kawaida kabisa na unapowauliza wahusika wanakujibu majibu rahisi rahisi tu wakiwa wamelizika kabisa, na huku hata usoni hawakuangalii, eti " serikali haina hela" mara " mkopo siku hizi bahati ya mtu" utadhani mwanafunzi  wanaoomba mkopo wanacheza bahati nasibu.

Nasema hili kwa hasira sana kwani ninafahamu fika maisha wanayoyaishi vyuoni nikiwemo mimi mwenyewe, na maisha yenyewe na jiji hili la Dar, na wale wa maeneo mengine ambao kila kitu kwao ni cha kununua, bado nauli za kila siku kwenye daladala hosteli zenyewe hazitoshi na kuwalazimu wanafunzi hawa kupanga, si kwamba vyumba wanapewa bure, Bali wanapangisha tena kwa gharama  kubwa.

Nikuulize wewe Rais wangu Magufuli hivi kweli hii ni haki, mtoto wa mkulima na huyu wa oye aye, kapuku hana lolote wala chochote kusoma bila mkopo? Na kupanga mtaani au ndo kusema kwamba mnaturudisha enzi zile za ukoloni ambapo watoto wa wenye nazo ndo wanapata haki ya kusoma elimu ya juu? Au kwa sababu hawa watoto wa wakulima ambao wazazi wao ni kapuku hawana lolote wala chochote hawana haja ya kusoma elimu ya juu?

Naamini unajua lakini kwa mwenendo huu hatutafika, mimi naamini kauli mbiu yako ya "Hapa kazi tu", lakini nakumbuka kwenye kampeni zako ulisema utahakikisha suala la mkopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu linakuwa historia, na kama itatokea mtoto wa huyu mkulima na mfugaji akakosa mkopo huku sifa zote anazo basi lazima uwakopoe wahusika katika bodi hii ya mikopo.

Naendelea kukuuliza kama baba wa familia ya watanzania ina maana mwaka huu watanzania 12000 Waliopata mkopo ndo watasoma elimu ya juu? Na hawa 50000 waliobakia ndo wao wakalime na kuchunga ng'ombe?  Kulima kwenyewe hawana hata mtaji wa kulima kilimo cha kisasa kitacho wapa pesa ili waweze kusoma? Au ndo wakakae mitaani wajifunze kukaba maana wengi wao wamepita JKT na wanajiona wameiva vya kutosha kufanya uharifu mtaani japo ni kinyume na kile walichoapa baada ya kumaliza mafunzo yao ya kijeshi.

Bado naendelea kusema na wewe Magufuli rais wa Tanzania ambae nilikuunga mkono mwanzo mwisho tangu mwezi julai mpaka sasa ninakuomba uwaagize viongozi wa wizara ya fedha watoe pesa kwa bodi ya mkopo ili vijana wa kitanzania wasome ili waje wawe watu watakaoendelea kuiweka Tanzania kwenye uso wa dunia ya watu wenye fikra chanya. Nani ajuaye labda huyu mwanafunzi aliyeshindwa kuendelea na masomo ya chuo kikuu ndiye angekuwa Elbert  Estorn wa Tanzania, au Newton wa Tanzania au hata Faraday wa nchi yetu? Mimi sijui lakini kwa kweli mnawanyima fursa watoto wa kapuku na wale wengine wa wenye uwezo wa kawaida ambao chai ya asubuhi kwao ni shida hivi wataweza kusomesha watoto chuo kikuu au mnatania?

Niliumia sana na naendelea kuumia nilipokosa mkopo mwaka Jana na baadae nikasikia wakina Chenge, Tibaijuka na wengine wamegawana mabilioni ya pesa na walipoulizwa mwingine pasipo hata kuangalia maisha ya watanzania na hawa kapuku anajibu kwa kujiamini eti milioni 10 za mboga. Na huku  wanafunzi wakishindia mikate na chai ya 1000 kwa siku kwao millioni 10 ni mboga tu sijui ni mboga gani hii ya pesa yote hii, au ndo kusema kila mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake? Tuambieni tujue jamani.

Sitaki kuwakumbusha watanzania juu ya ili kwani binadamu wote si sawa, wapo walio sawa zaidi na juu kuliko wengine na waswahili wakasema eti aliye juu mngoje chini lakini msemo huu bado mimi haujaniingia akilini mimi naamua kuwafuata huko huko ndiyo maana nasema nawe Magufuli.

Najua u msikivu na ulituahidi ukijua ya kwamba utatutekelezea, sishangai nikienda Hospitali na kutumia zaidi ya wiki mbili ndipo nimalize matibabu yangu na kuonana na daktari huku wenye nazo wakitumia nusu saa tu kukamilisha huduma zao hospitalini. Ni kawaida kwani tumeyazoea maisha hao na ni kawaida yetu tunaishi hivyo hivyo maana wakubwa wanajifanya hawayajui.

Sishangai kwenda mawodini na kuona watu wamelazwa chini huku wakiwa na dripu za maji na damu huku gharama za kulala zikiwa palepale, ni maisha yetu tumeyazoea kuyaishi. Pia sishangai kuona mama zetu wakijifungulia chini huku wakitukanwa matusi ya kila aina na wahudumu wa hospitali zetu ambao hata wewe ulitibiwa na nahisi ndo hayohayo mazingira ambao mamayako alikuzaa kwayo. Lakini leo nakuhasa tuangalie na sisi tunaotibiwa huku ili wake zetu, mama zetu na hata dada zetu wajifungue wakiwa mahali pa usalama. Au ni kwa sababu wakubwa hawatibiwi na kujifungulia huku?

Naamini kabisa makamu wako ni mwanamama, hanaujua na kuufahamu vyema uchungu kwani na yeye alijifungua japo sina uhakika kama alijifungulia kwenye hospitali tulizozaliwa sisi.   Hata kama hakujifungulia huko hata naamini na ni msemo unasema uchungu wa mwana aujuye mama, na si mzazi.

Naamini utawaboreshea mama zetu mazingira mazuri na kutuletea dawa hospitalini ili tuuguapo twende hospitali za serikali tukiwa na uhakika wa kupata matibabu na dawa kwa muda mfupi si mara njoo kesho maabara, mara daktari anapatikana ijumaa tu, hivyo njoo baada ya miezi sita ndiyo utaonana na daktari.

Umetuahidi viwanda ambavyo vitapunguza tatizo la ajira nchini, na kufanya nchi yetu kuwa ya viwanda ambavyo vitaajiri watanzania wengi waliomtaani hawana kazi, hawana ajira. Lakini kama vitajengwa na kufufuliwa vitapunguza tatizo la ajira maana hata maisha ya mtanzania yatapanda hadhi.

Suala la rushwa na ufisadi kwa viongozi wa umma bado ni tatizo kubwa, kama ulivyo ahidi naamini utafanya tatizo ili kuwa historia, kwani watanzania tunaumia na kusononeka sana mioyoni mwetu kuwaona viongozi tuliowaamini na kuwapa ridhaa ya kutuongoza kutuibia Mali zetu tena mchana kweupe na kuja kutuambia eti ni vijisenti tu, huku wengine wakifa njaa! Waingereza wanasema this is non sense, nikiwa na maana haina mashiko.

Umetuahidi kuanzisha mahakama kwa ajili ya kushughulikia masuala ya rushwa, nakuomba ufanye hivyo mapema ili watanzania wawe na imani na wewe. Ili haya mafisadi na majizi yanayotupora na kutuuibia mali zetu kimachomacho na mchana kweupe nayo yakanyee debe kama yule mwizi wa kuku na njiwa na yule aliyeshindwa kulipa shilingi 5000 akahukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.

Makala haya yameandikwa na mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kikuu cha Dar es  saalam anasomea Mawasiliano kwa Umma. Anapatikana kwa email ya barakangofira@gmail.com au simu namba 0763590901 na 0716216249.
NASEMA NAWE MAGUFULI NASEMA NAWE MAGUFULI Reviewed by WANGOFIRA on 05:19:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.