HIFADHI YA TAIFA YA MKOMAZI
HIFADHI YA WANYAMAPORI
YA MKOMAZI
NA, Baraka Ngofira
0763580901, 0716216249
Kipindi fulani nikiwa mdogo nilizoea kusikia wimbo ukiimbwa “mbuga
za wanyama Tanzania ya
kwanza ni Serengeti, ngorongoro, manyara na mikumi ooooh Tanzania oyeeee” kwangu ni wimbo uliokuwa
ukinikaririsha mbuga za wanyama zenye kuvutia zipatikanazo nchini Tanzania .
Niliupenda huu wimbo kwani hata nilipokuwa darasa la nne,
nakumbuka moja ya swali liliuliza taja mbuga nne za wanyama zipatikanazo nchini
Tanzania .
Kwangu sikuwa na haja ya kuangaika ninachokumbuka nikiwa ndani ya chumba cha
mtihani, nilisikia wimbo huu ukuibwa akilini mwangu ndipo pasipo kupoteza muda
nilijaza mbuga hizo.
Lakini kadri nilivyozidi kusoma madarasa ya juu
nikafundishwa mbuga na hifadhi nyingine za wanyama pori
zinazopatikana Tanzania .
Nilitaka kumbishia mwalimu wangu kuwa nikiwa mdogo nilifundishwa na kuimbiwa
wimbo ambao kila siku nilipaswa kuuimba kabla sijaingia darasani. Kuwa “mbuga
za wanyama Tanzania ya
kwanza ni Serengeti, Ngorongoro, Manyara na Mikumi ooh Tanzania oyeee”.
Sikubishana na mwalimu kwani hata wazazi wangu ni walimu nao
walishiriki kunifundisha na kunikaririsha hivyo. Lakini walinambia mwanangu
uendeleapo na masomo yako usiwe mbishi kwa walimu wako hata kama
wakikufundisha jambo ambalo unalifahamu kwani mwalimu amekutangulia na
anafahamu mengi kuliko wewe.
Na pia waliniiambia ukiona kama
anakudanganya wewe nenda maktaba au muombe mwalimu wa somo husika akuazime
kitabu ukajisomee mwenyewe, kwani pia ni mbinu mojawapo na ndiyo nguzo kuu ya
kujifunza mambo usiyoyajua.
Nilipokumbuka kauli hii ya wazazi wangu nilienda maktaba
nikaanza kusoma kwa undani kuhusu vivutio vya kitalii vinavyopatikana hapa Tanzania , kwa kweli nikashangaa kuwa karibu kila
mkoa wa hapa Tanzania
una mbuga au hifadhi ya wanyamapori ambao ni tuzo kubwa kwa taifa letu.
Niliporudi likizo niliwauliza wazazi wangu kuwa hivi Tanzania kuna
mbuga ngapi za wanyama? Nao walinambia mwanangu kuna mbuga nyiiiingi lakini
kubwa ni kama tano ambazo ni Serengeti,
Manyara, Mikumi, Ngorongoro na Selous
iliyopo mkoani morogoro.
Waliponimbia hivyo nikasema kumbe ndiyo maana wimbo
walionifundisha ulikuwa unataja mbuga hizo, kwa sababu ya ukubwa na wingi wa
vivutio vya kitalii vipatikanavyo katika mbuga hizo? Nijisemea moyoni mwangu
nitakapokuwa nitajitahidi kwa kadri ya
uwezo wangu nitembee nijionee kwa macho yangu hao wanyama wa asili
wanaopatikana katika mbuga tulizonazo nchini.
Lakini sikuishia hapo nilidhamilia kuwaelimisha watanzania
kutembelea na kujifunza ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza nchi yetu
kimataifa kuhusu vivutio vya kitalii vilivyopo nchini kwetu.
Safari yangu ilianzia Serengeti, Ngorongoro, kisha nikaenda
Manyara kujionea wanyama pori
hawa ambao ni tuzo kubwa tuliyojaliwa kupewa na mwenyezi Mungu. Lakini pia
nilipata fursa ya kusoma katika shule kongwe ya sekondari iliyopo mkoani Kilimanjaro
katika wilaya ya Hai, si nyingine ni shule ya wavulana ya Lyamungo sekondari. Nikiwa
hapa kila siku mchana na jioni nilifurahia kutazama kilele cha mlima wa Kilimanjaro
ambao ni mrefu Afrika na wa pili duniani.
Kwangu nilidhamiria kuupanda nikiwa sijamaliza masomo yangu
katika mkoa huo na kurudi kwetu Musoma. Lakini kwa bahati mbaya sikupata fursa
hiyo hadhimu, lakini ninachokifurahia nilipokuwa nikipata nafasi mimi na
marafiki zangu tulienda kutembea walau Machame mahali lilipo lango kuu la
kupandia mlima huu mlefu na wa ajabu.
Tulipokuwa tukifika tulipokelewa vizuri na walau kutembezwa
mita kama mia mbili hivi kutoka lango kuu hilo ,
huku tukipewa maelekezo muhimu ya jinsi gain ya kupanda mlima huo na ni vitu gani
vya msingi vya kuzingatia kabla ya kupanga safari ya kwenda kupanda mlima huo.
Lakini pia katika safari zangu nikagundua kuwa nchini Tanzania kati
ya mikoa iliyobarikiwa mmoja wapo ni mkoa wa Kilimanjaro. Kwani hata hali yake
ya hewa ni Baraka tosha kuruhusu matunda ikiwemo ndizi ambazo kwao mara nyingi
hutumika kutengenezea pombe maarufu kama
mbege, maparachichi au kwa lugha ya kigeni “Ovacado”.
Lakini pia bila kusahau mikahawa ambayo hulimwa kwa wingi
karibu wilaya zote za mkoa huu, ukitoa mwanga na same ambapo kwazo hulima kwa
wingi katani ambazo kwa sasa zinaonekana kukosa soko na viwanda vyake kufa.
Pia, kuna mbuga za wanyama ambazo si maarufu lakini zikiwa
na wanyama wa ajabu ambao kama wakitangazwa na
vyombo au idara husika zinaweza kutuletea faida kubwa katika sekta ya utalii. Si
nyingine bali ni hifadhi ya wanyapori ya Kilimanjaro maarufu kama
KINAPA na nyingine ni MKOMAZI ambayo ndiyo lengo langu la kuandika makala haya.
Hifadhi hii ya Mkomazi ina historia ndefu kama
zilivyo hifadhi nyingine lakini pia naweza sema ni hifadhi yenye historia ndefu
kuliko hata hifadhi nyingine zenye majina makubwa hapa nchini.
Ni hifadhi iliyoanzishwa mwaka 1951 hata kabla ya nchi yetu
kupata uhuru, lakini haikuwa hifadhi kama ilivyo leo bali lilikuwa ni pori la akiba la Ruvu. Ikiwa
na ukubwa wa kilomita za mraba 2010.4 na huku nyingine 1224.1 za pori la akiba la Umba ambalo
jumla kuu ya kilomita za mraba ni 3245. inapatikana katika wilaya ya Same
mkoani Kilimanjaro kilomita 6 kutoka Same mjini, 120 kutoka Moshi mjini , 155
kutoka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro maarufu kama KIA na 200 kutoka jijini
Arusha.
Imepakana na mkoa wa Tanga pia
mbuga ya Tsavo iliyopo nchini Kenya
ambapo wanyama wengi hususani tembo, nyati na swala hukimbilia wakati wa
kiangazi na kurudi wakati wa masika. Kuhama huku kwa wanyama hawa husaidia
kuweka ikolojia sawa . ndani ya hifadhi hiyo.
Ilianzishwa rasmi na kupewa mamlaka kama
hifadhi ya wanyama mwaka 2007 ambapo mamlaka zinazohusika zikisaidiana na
tanapa na wizara ya utalii zimejitahidi kuifanya hifadhi hii kujulikana
miongoni mwa watanzania hata na nchi jirani.
Asili ya mbuga hii ni kabila la wapare ambayo inamaanisha kijiko
cha tone lolote la maji yaani MKO ni kijiko na MAZI ni tone lolote la maji. Hapo kidogo nahisi
umeelewa jinsi maneno ya kipare yalivyo mafupi lakini yakibeba maana na ujumbe
mkubwa. Iliitwa hivi kutokana na maeneo ipatikanapo mbuga hii kuwa maeneo
makame sana
ambapo upatikanaji wa maji ni wa shida.
Kutokana na jiografia ya wilaya ya same kuwa na vimilima
vingi vilivyo jaa miamba na hivyo kusababisha upatikanaji wa maji kuwa wa shida lakini mbali na shida hiyo
wanyama wanaopatikana hifadhini hapa uishi kwa kutegemea vidimbi vidogo vidogo
ambavyo uhifadhi maji wakati wa mvua na
kukauka wakati wa jua kali.
Wakati mzuri wa kutembelea hifadhi hii, ni kuanzia mwezi
juni mpaka januari ambapo wanyama wengi huwa wamerudi kutoka mbuga ya Tsavo
ambapo uenda kipindi cha kiangazi na kurejea wakati wa masika ambapo maji na
chakula kama nyasi huwa ni nyingi hifadhini
humo.
Vivutio vya kitalii vipatikanavyo ndani ya hifadhi hii ni kama vingine vinavyopatikana katika hifadhi nyingine za
hapa nchini lakini vipo vingine ambavyo ni tofauti kabisa na hupatikana ndani
ya hifadhi hii pekee ambavyo ni vifaru weusi ambao walitolewa nchi Afrika
Kusini mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Faru hawa ni wa ajabu kutokana na kuwa na rangi tofauti na
faru wengine wapatikanao katika mbuga nyingine za hapa nchini. Na hivyo kuwa kivutio
kikubwa kwa watalii wengi kwenda kutembelea hifadhini hapa, ili kujionea kwa
macho yao jinsi
faru hawa walivyo na wanavyoipamba mbuga hii ambayo wengi wa watanzania
hawaifahamu.
Pia, kuna ndege aina mbalimbali wakiwemo Tai, na mbuni na
wenginewo wengi ambao hupamba na kuing’arisha hifadhi hii. Ndege hawa hususani
Tai na mbuni husifika kwa ujasiri wao wa kuweza kupambana na kuwamudu vyema
maadui na wanyama wengine hatari wanatakao kufupisha maisha yao .
Ndege hawa ni wa ajabu sana, na hivyo kuwa kivutio kikubwa
sana kwa watalii japo huwa ni adhimu sana kuwaona kutokana na wao kupenda
kujificha kwenye mapori na vichaka vidogo vidogo. Ni mara chache sana kuonekana kwa watalii wengi, hivyo wewe kama mtanzania unapaswa kwenda kujionea kwa macho yako
jinsi gani ndege hawa wa ajabu wafananavyo.
Pia, ndani ya hifadhi hii utawaona mbwa nap aka mwitu ambao
wanapendezesha mbuga hii. Mbwa na paka mwitu hawa ni wanyama kama wale
tuwafugao majumbani lakini tofauti yao ni kwamba, mbwa nap aka hawa wana rangi
nyeusi na nyuso zao zimechong’oka na uwezo wao wa kukimbia na kupambana na
maadui ni mkubwa kuliko paka na mbwa mwitu wa kufuga.
Wengine ni wanyama wa kawaida ambao karibu kila hifadhi
upatikana kama vile tembo, swala, digidigi, twiga, nyati na wengine wengi,
hivyo ni jukumu lako wewe kama mtanzania
kupenda chako na kuthamini maliasili zetu tulizonazo hapa nchini. Jiulize ni
wageni wangapi wamekuja kutazama wanyama hawa tena kwa gharama kubwa lakini
sisi wazawa walio wengi hawaoni haja ya kutembelea hifadhi hizi. Ebu tuchangamkie
fursa wakati ndiyo huu.
Mbali na wanyama hawa kuna milima ya upare na usambala
ambayo imekuwa kivutio kikubwa cha kitalii hasa kwa wageni waendao kutembelea
hifadhini hapa. Milima hii imekewa maarufu kwa ilivyojengeka, miamba yake na
udongo wake ambapo maporomoko ya milima hii ndiyo uwaacha watalii hoi kwani,
ilivyojengeka ni vigumu kuadithia ili mtu aelewe kwa urahisi. Lakini kwa wengi
waliowahi kufika na kujionea mlima hii wanaweza kuelezea ni jinsi gani milima
hii ya ajabu.
Mbali na vivutio hivyo hifadhi hii bado unakabiliwa na
changamoto kubwa ya kukosa hoteli na nyumba za malazi za kutosha kwa wageni na
watalii hawa na hivyo kutumia muda mwingi na mrefu kwenda kujipumzisha mjini
Same. Tofauti na ilivyo hifadhi ya taifa ya Serengeti na Ngorongoro.
Hivi ushawahi kujiuliza ni kwa nini wageni hawa au wazungu
wengi hutoka ulaya, Marekani na sehemu nyingine duniani kuja Tanzania kuona
wanyama? Huku wewe umekaa na kuwashangaa tu, utadhani wanapoteza muda wao.
Hivyo basi chonde chonde mtanzania mwenzangu panga
kutembelea mbuga na vivutio vyetu vya kitalii vipatikanavyo hapa nchini kwetu,
ili ujionee mwenyewe na ufurahie utanzania wako.
Makala haya yameandikwa na
mwanafunzi wa mwaka wa pili wa shahada ya kwanza ya Mawasiliano kwa Umma ya
Shule Kuu ya Uhandishi wa Habari na Mawasiliano kwa umma ya Chuo Kikuu cha Dar
es salaam (UDSM-SJMC) anapatikana kwa mawasiliano ya email ya barakangofira@gmail.com au simu namba
0763580901 au 0716216249
HIFADHI YA TAIFA YA MKOMAZI
Reviewed by WANGOFIRA
on
06:34:00
Rating:
No comments: