Waliopitisha nyara zilizonaswa Uswisi wachunguzwa


WIZARA ya Maliasili na Utalii imeanza kufanya uchunguzi kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali, ikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na vyombo vya ulinzi na usalama ili kubaini waliohusika na upitishwaji wa nyara za serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hivi karibuni.
Wizara hiyo pia imeeleza kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizo za kukamatwa kwa nyara za serikali katika Uwanja wa Ndege wa Zurich nchini Uswisi zikiwa njiani kwenda China kutokea Uwanja huo wa Ndege wa Kimataifa wa JNIA wa jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya wizara hiyo kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Waziri Lazaro Nyalandu ilisema wizara hiyo inaupongeza uongozi wa Uwanja wa Ndege wa Zurich na Serikali ya Uswisi na watu wote walioshiriki kubaini na kukamata nyara hizo.
Kwa mujibu wa Waziri Nyalandu, nyara hizo zinajumuisha meno ya tembo yenye uzito wa kilo 262, kucha na meno ya simba vyenye uzito wa kilo moja. Alisema tukio la kukamatwa kwa nyara hizo lilitokea kwenye uwanja huo Julai 6, mwaka huu zikiwa ndani ya masanduku manane zikiwa njiani kwenda Beijing China kutokea uwanja wa ndege wa Dar es Salaam kupitia Zurich.
“Wizara imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizi na kwamba nyara hizo zimesafirishwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere. Tukio hili linadhihirisha kuwa tatizo la ujangili bado linaendelea ndani na nje ya nchi yetu” alisema.
Waliopitisha nyara zilizonaswa Uswisi wachunguzwa Waliopitisha nyara zilizonaswa Uswisi wachunguzwa Reviewed by WANGOFIRA on 01:41:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.