UJASILIAMALI NI KIPAJI

UKIFUATILIA kinachozungumzwa katika masuala ya uwezeshaji, iwe ni katika ngazi ya familia au ya vikundi, hasa vya kina mama ingawa vijana pia wanahusika, unakuta chembe iliyosambaa kuhusu maana halisi ya uwezeshaji, Maana hii ni tofauti na jinsi mtu anavyopeleka 'mchanganuo' wa mradi fulani kutafuta mkopo benki, au kama tayari ni mjasiriamali, kushiriki mradi fulani kama sehemu ya mpangilio wa mauzo, 'manunuzi,' n.k. Unakuta kuwa kinachoangaliwa zaidi katika miradi hii ya ngazi ya familia, vikundi ni kutaka kufaulisha, kufanikisha, atakacho.

Msingi wa uwezeshaji ni ukaribu wa mtu mmoja na mwingine, au pale inapotokea mamlaka inajivua gamba la umbali, u-serikali na kuanza kuwa karibu kimawazo na wanaohusika, au iliochagua kushirikiana nao. Ni tofauti moja muhimu kati ya idara ya serikali na vikundi huria vya kijamii, kuwa idara hizo (pamoja na baadhi ya taasisi zake ikiwemo vyama vya ushirika, mabenki ya aina tofauti) yanamchuja mtu ili mahitaji yao yafikiwe, wanaangalia kwa undani kama anakidhi matakwa ya kile ambayo taasisi hiyo inataka. Uwezeshaji halisi unaanza na hisia tofauti kabisa.

Katika ngazi ya familia, uwezeshaji unaanzia katika hitaji la riziki au la furaha, pale ambapo riziki ipo lakini upo uwezo wa kujituma na hata kuongeza kipato na kuhakikisha vyema zaidi maisha ya baadaye, na siyo kukaa tu nyumbani. Ni ngazi ambayo hakuna 'mchujo' kwani uhusiano uliopo unatoa tayari majukumu kwa mwenza husika, na ndiyo maana anakuwa na nia ya kuwezesha, bila 'mchujo' kwani anachopima siyo ule mradi, ila ni furaha na kufanikisha uwezo wa yule aliye naye. Na ni hisia kama hiyo ambayo inatawala kuunmdwa kwa makundi ya ujirani.

Katika mazingira kama hayo jambo la msingi ni kuwa wahusika ni majirani, na kila mmoja wao anahitaji kuboresha riziki yake, na wao kama majirani wana lengo la kuwezeshana, siyo kusadiana ambako fedha inatoka kuelekea upande mmoja, ila kuwezesha kwa mzunguko. Ndiyo sababu ya kuunda vikundi vya 'kuangaliana' katika kulipa, na hata kujiridhisha kuhusu mwendo wa biashara, hasda utunzaji wa fedha, ili lengo la pamoja lifanikiwe, mzunguko ule usiingiliwe na kizuizi ambacho hakikutarajiwa. Uwezeshaji unafanana na malezi, tofauti na uchujaji.
Jambo la kushangaza ni kuwa sehemu kubwa ya shughuli za kifedha au za kibenji zilizopo hivi sasa zilianzia katika jitihada ya kuwa na taasisi za fedha wezeshaji, na siyo zile chujaji peke yake. Zile za kuchuja zikawa za hali ya juu zikaitwa ni benki 'za kibiashara,' halafu zile zenye lengo la uwezeshaji angalau kwa kiasi fulani zikaitwa taasisi za mitaji midogo, na baadaye nyingine zikaitwa za jumuia. Hizi za mwisho kwa jumla ni za biashara, zina hulka ile ile ya kuchuja, lakini zinapunguza wigo, wanakuwa ni watu wa eneo linalojulikana, wenye mizizi hapo, ambao kwa jumla wanaweza kufuatiliwa na hata kuangaliwa wanachofanya kwa karibu zaidi.

Hivyo mikusanyiko mingi ya shughuli za kifedha huwa ina miingiliano na hisia za kijamii kwa upande fulani, tofauti na mtazamo wa kibiashara bila kuingiza chembe ya wajibu au jitihada ya aina moja au nyingine. Hii hisia ya wajibu na jitihada ya kufanikisha shughuli za kutafuta kipato katika ngazi moja au nyingine kimsingi ni chembe za uwezeshaji, ila tu zina viwango tufauti vya kuhusika. Kwa mfano benki za jumuia zinalenga tu eneo fulani, lakini hazina uwezo wa kumtambua mtu mmoja mmoja, wakati hiyo ni chembe tangulizi katika uwezeshaji halisi, kianzio chake. Nje ya kumfahamu mtu, kumtakia mema, kuhisi ipo haja ajaribu, dhamira ya uwezeshaji inakosa mashiko, pale inapokuwa ni biashara tu, ianze kwa mchujo.

Tofauti hiyo ya dhamira inaendana vile vile na mtazamo kuhusu mtaji katika maeneo hayo mawili, kuwa mtaji katika uhusiano wa mchujo ni fedha yenye nia ya kuingiza faida, yaani ni biashara kwa yule anayeitoa, na ndiyo maana anahitaji kuwa mwangalifu sana, asije kumpa mtaji huo 'mtu asiyefaa.' Katika dhamira ya uwezeshaji, mtaji ni kama fungu maalum la kuwezesha maendeleo, au kwa lugha tofauti kidogo, la kuongeza kiwango cha furaha pale watu tofauti, iwe ni kati ya wenza au majirani, wanapofaulu kuinua shughuli zinazoingiza kipato, wahakikishe mahitaji ya lazima, maradhi yapungue, na hata uwezekano wa ujambazi mtaani siku za baadaye upungue. Vijana wanaoendelea na masomo hadi ufundi halafu waanze shughuli fulani ni nadra kukaa katika vikundi vya kuvuta bangi, kuiba au kubaka, na binti aliyesheheni mipango ya masomo na shughuli yenye faida huweza zaidi kukaidi fedha rahisi za kuingia, kuzamia mazingira hatarishi ya ukahaba, n.k

UJASILIAMALI NI KIPAJI UJASILIAMALI NI KIPAJI Reviewed by WANGOFIRA on 07:15:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.