TUNAPASWA TUWALINDE WANYAMA WETU

Twiga wakiwa kwenye moja ya hifadhi za wanyama
Twiga wakiwa kwenye moja ya hifadhi za wanyama pori. 

Licha ya kukinzana, mipango mbalimbali imekuwa ikifanywa ili kudhibiti tatizo hilo ambalo linatishia kumaliza tembo, wanyama ambao ni adimu na walio kivutio kikubwa cha utalii.
Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (Tawiri) na Tanzania Elephant Protection Society (TEPS), mwaka 2012 walitoa taarifa iliyoonyesha kuwa wastani wa tembo 30 hufa kwa siku, kwa mwezi ni 800 na kwa mwaka inakadiriwa kufikia 10,000.
Takwimu hizo za kitafiti zinafuatiwa na zilizofanyika Oktoba hadi Desemba 2013 katika eneo la Selous, pamoja na kuwapo kwa taarifa za ongezeko la tembo katika maeneo ya Serengeti.
Kwenye hotuba ya Rais Jakaya Kikwete Desemba 31,2014 katika salaamu za kufunga mwaka na kukaribisha mwaka mpya 2015 alizungumzia pia juu ya ujangili.
Rais anasema mwaka 2014 ndovu 114 waliuawa ikiwa ni sawa na ndovu 9 kwa mwezi kwa nchi nzima ukilinganisha na 219 waliouawa mwaka 2013 na mwaka 2012 ndovu waliouawa walikuwa 473.
Majangili 1,354 walikamatwa, pembe za ndovu 543 na silaha 184 zilikamatwa kwa kipindi hicho na kuwa ujangili kwa sasa umepungua, ingawa majangili waliofungwa kama kiashiria cha hatua kuchukuliwa hakusema.
Takwimu hizo zinaonyesha kushuka kwa asilimia kubwa kwa kuwa mwaka 2012 taarifa za utafiti wa taasisi za ndani na nje zilibaini kuwa tembo 10,000 kwa mwaka.
Januari 2014, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye wakati huo alikuwa Naibu Waziri, alitoa takwimu za sensa ya wanyama iliyofanyika Oktoba hadi Desemba 2013 katika eneo la Selous kuwa mizoga 6,516 ilihesabiwa ambayo ni zaidi ya mara ishirini na tisa ya takwimu zilizotolewa na Rais Kikwete.
Kwa kipindi hicho Mizoga ilibainika katika eneo la ikolojia ya Selous, Mikumi, Ruaha na Rungwa, tafiti zilibaini asilimia saba hadi nane ya mizoga hiyo ilitokana na vifo vya asili, kama ugonjwa na uzee, lakini asilimia 92 ikiashiria vilisababishwa na ujangili.
Kwa mujibu wa utafiti ulioshirikisha wataalamu wa ndani na nje kwa kufadhiliwa na Shirika la Misaada ya kiufundi la Ujermani (GIZ), Frankfurt Zological Society (FZS) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kupitia Tanapa na Spanest, ulibaini ujangili wa kutisha.
Taarifa hiyo inabainisha kuwa hali ilivyokutwa katika pori tengefu la Kilombero ambalo ni sehemu ya ikolojia ya Selous na Mikumi mwaka 2002 lilikuwa na tembo 2,080 wakati wa sensa ya mwaka 2013 hakukuwa na tembo hata mmoja, lakini taarifa zinazotoka sasa zinaonyesha ujangili umepungua.
Kwa mjibu wa wizara ya Maliasili na Utalii viashiria vingine vya ongezeko la ujangili ni kasi ya kukamatwa kwa meno ya tembo kwa kipindi cha mwaka 2008 hadi septemba 2013 meno yenye uzito wa kilogramu 32,987 yalikamatwa ndani na nje ya nchi.
Uhasama unachochea ujangili
Matokeo ya tafiti hizo zinazoonyesha ukubwa wa tatizo ndiyo chanzo cha kuwekwa mikakati mingi iliyopata misaada ya mataifa mengine ya nje ili kusaidia kukabiliana na ukubwa wa tatizo hilo linalotishia kumaliza rasilimali hizo ni ushirikishwaji wa jamii.
Miongoni mwa mikakati iliyowekwa mjini Gabarone Botswana Desemba mwaka 2013 na Mkutano wa London nchini Uingereza Februari 2014, uliazimiwa kwamba ipo haja ya kushirikisha wananchi waishio kandokando ya maeneo ya hifadhi.
Hii inatokana na ukweli kwamba wanaoishi karibu na hifadhi ndio mara nyingi wamekuwa wakijua baadhi ya wanaojihusisha na biashara hiyo na hata mbinu ambazo wanatumia lakini wamekuwa wakificha taarifa hizo.
Ni ukweli usiopingika kwamba hata hapa nchini, baadhi ya watu wanaoishi jirani na hifadhi wamekuwa hawana uhusiano mzuri na mamlaka zinazosimamia mali hizo asili.
Moja ya tatizo ni unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya askari ambao wanalinda hifadhi. Wengi wao wamekuwa wakionekana jeuri na huwapiga na hata kuwajeruhi baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kwa madai kwamba wameingia maeneo ya hifadhi au wanyama wao, kama vile ng’ombe, walionekana maeneo hayo.
Mtafiti wa Wanyamapori, Mabenga Magonera anasema wakazi wengi wa vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Serengeti wamekuwa hawana uhusiano mzuri na hifadhi kutokana na kasoro kadhaa.
Miongoni mwa kasoro hizo anasema ni tozo za kodi ambazo zinaonekana kuwaongezea gharama bila sababu pamoja na ugomvi wa mara kwa mara hasa pale inapotokea mwanakijiji kaingia kuokota kuni kwenye hifadhi.
Magonera anaelezea tatizo la kodi wakazi wa Serengeti kuwa hutokea pale wanapopita wakitoka au kuingia vijijini kwao wanapokuwa na safari za wilaya au mikoa mingine.
Anasema hata kama ni mgonjwa anapelekwa hospitali, kwa mfano mara nyingi huwapeleka hospitali za Arusha, hulazimika kulipia Sh3,000 wanapokatiza Serengeti na Sh5,000 kwenye Hifadhi ya Ngorongoro.
“Hii ni uonevu na inawanyanyasa wakazi wa Serengeti na hata bidhaa zinazowafikia zinakua aghali kutokana na kodi hizi,” anasema akisisitiza zilipaswa kulipwa na watalii na si wapita njia.
Anahoji ni kwa nini kodi za namna hiyo hazitozwi kwenye Mbuga ya Mikumbi ambamo imepita barabara ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Mambo mengine ambayo yanaonekana ni manyanyaso kwa wakazi wa vijiji vya Wilaya ya Serengeti ni kukamatwa na kushtakiwa wilaya ya jirani ya Bunda inapotokea wamekutwa wakikata nyasi, kuni au miti ya kutengeneza nyumba.
“Wanaenda kuwashtaki Bunda, umbali wa kilomita 150, wakati wilayani Serengeti kuna mahakama za ngazi hiyohiyo ya wilaya. Hii ni kwanyanyasa! Wanafanya hivyo ili wananchi wapate usumbufu wa kwenda mbali kusikiliza kesi, kupoteza muda na wanaathirika kiuchumi kwa sababu kazi zao zinasimama. Hii ni kuwafanyia ukatili ili washindwe kuomba dhamana. hili linapaswa kukomeshwa!” anaonya Magonera.
Tatizo jingine anasema ni la barabara kutokuwa na lami kwa madai ni kutoathiri hali halisi ya hifadhi, jambo ambalo linafanya usafiri kuwa mgumu, wenye gharama kubwa na hata kuongeza gharama za bidhaa.
Anasema Serengeti haijaunganishwa kwa barabara ya lami kama ilivyo wilaya nyingine nchini. Pamoja na kwamba kumekuwepo na shinikizo la kuzuia barabara kujengwa ndani ya eneo la hifadhi, lakini kuna maeneo ya wilaya yanaweza yakatengenezwa ni kupunguza adha.
Mikakati mingine inatajwa kuwa ni utoaji wa elimu ya namna ya kudhibiti vyanzo vya ujangili na kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wengine wa maendeleo, taasisi za uhifadhi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, serikali, watafiti na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.
Ili vita ya kupambana na ujangili iwe na nguvu, takwimu zinatakiwa kuwa sahihi na kuwapo, mkakati makini kukabili ujangili na kuepuka chokochoko na wananchi.
source mwananchi 06 august 2015
TUNAPASWA TUWALINDE WANYAMA WETU TUNAPASWA TUWALINDE WANYAMA WETU Reviewed by WANGOFIRA on 01:29:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.