NEC yaandikisha 94% Dar


WATU 2,634,942 wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura mkoani Dar es Salaam katika mfumo wa BVR, sawa na asilimia 93.76. Mkuu wa Idara ya Elimu ya Mpigakura na Habari wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ruth Masham alisema hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya uandikishwaji huo katika Jiji la Dar es Salaam.
Alisema idadi hiyo ya walioandikishwa ni ya hadi juzi. Alifafanua kuwa katika wilaya ya Ilala, tume ilikadiria kuandikisha watu 811,716, lakini walioandikishwa ni 743,782, sawa na asilimia 91.63. Alisema wilaya ya Kinondoni, tume ilikadiria kuandikisha watu 1,102,565 na hadi juzi walioandikishwa walikuwa 1,075,946, sawa na asilimia 97.58.
Katika wilaya ya Temeke, watu 896,142 walitarajiwa kuandikishwa na walioandikishwa walikuwa 815,214, sawa na asilimia 90.96. Uandikishaji huo unatarajiwa kumalizika leo baada ya tume hiyo kuongeza siku nne kuanzia Agosti mosi.
Awali, uandikishaji huo katika mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa uishe Julai 31. Ulianza Julai 22 mwaka huu.
Reviewed by WANGOFIRA on 07:39:00 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.